…………………………………………………………………………………………..
MTANDAO wa Wanawake na Katiba
Tanzania umewapongeza wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba na hasa wajumbe
waliokuwa mstari wa mbele kupigania masuala mbalimbali yaliyokuwa
yanapendekezwa na mtandao huo juu ya uwepo wa Katiba inayopendekezwa
yenye mtazamo wa kijinsia.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini
Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania,
Prof. Ruth Meena akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku moja
baada ya Rasimu ya Katiba inayopendekezwa kuwasilishwa kwenye Bunge
Maalum la Katiba Mjini Dodoma tayari kwa zoezi la kuanza kupigiwa kura
kifungu kwa kifungu na wajumbe wa bunge hilo.
Prof. Meena alisema Mtandao wa
Wanawake na Katiba Tanzania haunabudi kuwapongeza wajumbe wote wa bunge
maalum na hasa wale waliowaunga mkono kupaza sauti juu ya madai ambayo
waliwasilisha kupitia mtandao wao na njia nyingine mbalimbali
kushinikiza katiba inayopendekezwa kuwa na mlengo wa kijinsia ili kutoa
usawa wa kijinsia.
Alisema Rasimu ya Katiba
inayopendekeza imeonesha mwelekeo wa kutoa usawa wa kijinsia jambo
ambalo mtandao huo unaamini ni mafanikio makubwa kwao na kwa jamii
inayojali usawa wa kijinsia. Aliongeza kuwa yapo mambo kadhaa ambayo
walipendekezwa yatajwe kwenye katiba kama umiliki wa ardhi kumtambua
mwanamke na kutajwa kwa umri wa mtoto jambo ambalo wanaamini litapunguza
kilio cha ndoa za utoto suala ambalo wanaharakati wa masuala ya
kijinsia wamekuwa wakilipigia kelele siku zote.
“…Tunapenda kutoa pongezi kwa
wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa moyo waliouonesha kujali
masuala ya kijinsia kwa kiasi chake…tunaunga mkono rasimu ya Katiba
inayopendekezwa kwa kuamini ni mwanzo mzuri wa kuonesha usawa wa
kijinsia…,” alisema Prof. Meena akizungumza na wanahabari.
Kwa upande wake Mjumbe wa Mtandao
wa Wanawake na Katiba Tanzania, Usu Mallya akizungumza alisema licha ya
mafanikio yao kwa mtandao wao wamehoji baadhi ya mapendekezo ambayo
yamekataliwa na wajumbe hao ilhali yanamuelekeo mzuri juu ya uwajibikaji
wa wanasiasa kwa wapigakura wao.
Alisema wameshangazwa na kitendo
cha wajumbe wa bunge la katiba kuruhusu kipengele ambacho kimeweka
utaratibu kuwa Rais wa nchi anaweza kushtakiwa ilhali wamepinga
kipengele za kutoa fursa kwa wapiga kura kumuwajibisha mbunge wao baada
ya kumchagua pale wanapoona ameshindwa kuwawakilisha kama
walivyokubaliana.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment