Serikali wilayani Hai imewaasa
wananchi kuachana na tabia ya unywaji wa pombe uliokithiri ambao unaathiri nguvu
kazi pamoja na maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa hivi
karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Hai Novatus Makunga kufuatia habari iliyochapishwa
na gazeti la Habari Leo toleo Na. 02830 la Ijumaa Septemba mwaka huu yenye
kichwa cha habari “Ulevi kwa wanafunzi wa Hai wamtisha DC”.
“Si kweli, hakuna kitu
kama hicho wala hakuna taarifa za wanafunzi kunywa pombe hizo hali inayopelekea
kuwa tishio katika wilaya yetu” alisema Makunga.
Akiongea kwa njia ya
simu kutoka wilayani Hai Makunga alisema kuwa alichosema wakati wa mazishi ya aliyewahi
kuwa Shehe wa mkoa wa Kilimanjaro Ally Lema alisema wazazi ndio wanaokunywa
pombe aina ya gongo na viroba na sio wanafunzi wa shule za msingi wala
sekondari.
Akifafanua juu ya suala
hilo, Makunga alisema kuwa wazazi pamoja na vijana wengi wanaokaa vijiweni wakiowemo
madereva wa “bodaboda” ndio kundi linalosadikiwa kukithiri katika unywaji wa
pombe aina ya gongo na viroba ambavyo vinatishia kuathiri mfumo wa uzazi.
DC Makunga aliongeza
kuwa pombe hizo ni kali, sio salama na hazina kiwango ndio maana zinapelekea
kupunguza nguvu za uzazi ambapo hata Wachungaji wa dini mbalimbali wamesema
idadi ya watoto wa ubarikio katika makanisa yao pia imepungua.
Vilevile wilaya ya nchi
nzima inaweza kukosa nguvu kazi kutokana na vijana ambao ndio nguvu kazi ya
taifa kupungua au waliopo kutokuwa na nguvu ya kufanya kazi inavyopaswa
kutokana na hali yao ya unywaji wa pombe hizo zisizo salama.
Katika kukabiliana na
hali hiyo, Makunga alisema kuwa tayari wilaya yake ipo katika hatua za mwisho
kukamilisha sheria sheria ndogo ndogo inayopiga marufuku unywaji wa pombe
wakati wa saa za kazi wilayani humo.
Makunga alisema kuwa kwa
sasa Sheria kuu ya Serikali kuhusu unywaji pombe ndiyo inayotumika ambapo
inabainisha kuwa muda wa kunywa pombe siku za kazi yaani Jumatatu hadi Ijumaa
ni kuanzia saa 9: 00 mchana hadi saa 4:00 usiku na siku za Jumamosi, Jumapili
na siku za siku kuu ni kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 5:00 usiku ambapo atakayebainika
kukiuka utaratibu huo atachukuliwa hatua za kisheria.
Sheria hiyo inataja
kuwa anayekunywa pombe saa za kazi atapelekwa mahakamani na kupigwa faini au kifungo
cha miezi sita jela au adhabu zote kwa pamoja.
No comments:
Post a Comment