NA:LUQMAN MALOTO (Dar es Salaam).
JIJI linaitwa Dar es Salaam. Rapa wa Kimasai, marehemu Abel loshilaa
Motika ‘Mr Ebo’ anaita Saridalama. Wenye mikogo wanatamka Das’lam. Watu
na vifupisho, kuokoa nguvu na muda wanaita Dar.
Jiji linaitwa
Bongo, kwamba ukiishi ndani yake lazima ubongo wako uchangamke. Sifa za
jiji ni kubwa mno. Ukizaliwa mikoani katika maisha yetu pangu pakavu tia
mchuzi, kufika Dar ni matamanio makubwa. Kukanyaga Bongo ni ndoto
kugeuka kweli.
Jiji zamani liliitwa Mzizima kabla ya kubadilishwa
na kuitwa Dar es Salaam yenye maana ya Bandari Salama. Ni neno sawa na
Pwani Salama. Ndipo palipo na Ikulu, viongozi wote wa nchi wanaishi,
wafanyabiashara karibu wote wakubwa, wasanii maarufu, warembo wenye
kutikisa, makampuni makubwa.
Kimsingi Dar ndiyo mwanzo wa kila
kitu katika nchi. Hata makao makuu ya serikali imeshindikana kuhamia
Dodoma kwa sababu ya Dar. Viongozi wanaondokaje Dar? Jiji tamu hili.
Marapa Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Joseph Haule ‘Profesa Jay’, kila mmoja
alipata kutoa wimbo wa kuelezea sifa za Dar es Salaam. Wa Sugu unaitwa
Dar es Salaam na wa Profesa Jay ni Bongo Dar es Salaam.
Karibu
Dar, karibu sana. Hata mimi nyakati hizo nilipokuwa naisikia tu,
nilitamani kweli kufika. Baba yangu, marehemu Alhaj Swaleh Nyambo
aliponiambia likizo ile ningesafiri kuja Dar hakika nilifurahi, hata
wanafunzi wenzangu niliwasimulia. Sikumbuki kama kuna ambaye
sikumwambia. Hata walimu walijua. Dar tena!
Una ndoto za kuishi
Dar es Salaam? Karibu sana, njoo tuongeze msongamano. Mimi siyo kama
wale wenye kukataza watu wasije, maana sijui riziki yako ilipo. Pengine
wewe ni bilionea unayekuja, na kitovu cha ubilionea wako ni Dar. Hata
mimi ningekubali makatazo yao ya “usije mjini”, nisingekuwa Dar, wala
nisingekuwa mwandishi niliye leo.
Ukishakaribia Dar utayaona ya
Mwanameka. Kabla ya harusi hupendwi, unaonekana upoupo tu. Ukishaoa au
kuolewa ndiyo wenye kukupenda wanajitokeza, wanakupa mapenzi ya ghiliba
mpaka unachanganyikiwa, ndoa yako ikishavunjika, mchepuko badala ya
kufurahia kupata nafasi nzuri ya kujidai, nao unakimbia.
Wanaita
Pwani ya Kiranga, kuna watu wenyewe wanachotaka ni mapenzi ya wizi tu.
Hawataki kumiliki. Anaiba leo, akishaharibu anakwenda kuiba kwingine.
Maisha yake yote ni hivyo. Ukimuuliza mbona haoi au haolewi, jibu lake
ni woga wa kuibiwa. Mkuki kwa nguruwe bwana!
Yupo ambaye ni mkali
kweli kwa wake au waume wa wenzie. Ila wake hataki aguswe. Ucheke na wa
wenzio tu, wenzio wakicheka na wako ni nongwa. Hajui kuwa kuku akitoka
lazima arudi bandani.
Dar kuna mseto wa mahaba bwana! Jamaa
anaanzisha mapenzi na Mama Lishe (Mama Ntiliye) ili apate uhakika wa
chakula cha bure. Mrembo naye anajigonga kisha anajiweka kwa mwenye
kibanda cha chipsi ili awe anakula chipsi, mayai, kuku na soseji za
bure.
Dar watu wanajua kulenga. Mpangaji anafanya juu chini mpaka
anamgeuza mwenye nyumba mchepuko wake ili asilipe kodi ya pango.
Mwingine anampa mapenzi motomoto dereva wa bodaboda ili apate usafiri wa
bure. Madereva taksi na bajaji ndiyo usiseme.
Watu na magari
barabarani pamoja na mbwembwe za kuajiriwa kwenye maofisi ya maghorofa
marefu, hayo wala yasikutishe. Dar wengi wanaishi kibandiabandia. Wa
magari na ofisini wala hawana pesa, wamachinga, wauza mbogamboga,
madereva bodaboda na bajaji wana vipato vikubwa zaidi.
Mtu
anaamka alfajiri kuwahi kazini, anapanda kigari chake, anasubiri mwisho
wa mwezi mshahara shilingi milioni moja. Dereva wa bodaboda au bajaji
anatengeneza shilingi 100,000 mpaka shilingi 150,000 kwa siku. Hesabu ya
mwezi shilingi milioni tatu mpaka nne na nusu. Wanaendana hao?
Mtu anafanya kazi ofisini, analipwa mshahara shilingi 500,000 mpaka
600,000 kwa mwezi. Ajabu ni kuwa kwa mshahara huohuo, mfanyakazi wa
ofisini anamuona muuza mbogamboga na mchoma mahindi barabarani ana
maisha magumu, wakati anaingiza kwa siku faida ya shilingi 30,000.
Hesabu ya mwezi ni shilingi 900,000.
Kichekesho zaidi cha Dar es
Salaam ni kuwa mwenye kulipwa mshahara wa shilingi 500,000 akinunua
matunda kwenye genge, chenji ikibaki kidogo anamwachia. Wanaita tipu! Wa
shilingi 500,000 anamuongezea wa shilingi 900,000.
Dar es Salaam
vivutio vya utalii ni vingi, mtu ameajiriwa Mlimani City lakini akitaka
chakula anatoka nje kwenda kwa mama ntiliye. Yaani watu wapishana,
wakati wengine wakitoka kwenye maeneo yao kwenda Mlimani City kula,
wenye eneo wanakwenda kutafuta chakula nje. Ni mpishano.
Ukiuliza
wanaokwenda kula Mlimani City wanafuata nini, jibu ni “misosi mitamu”
au “misosi ya Kizungu.” Wengine wanafuata lile jengo, kuwepo pale ni
sifa. Mtu yupo Lufungilo, akiulizwa kwenye simu alipo, anajibu Mlimani
City.
Waulize pia wafanyakazi wa Mlimani City wanaotoka kwenda
kula kwenye migahawa ya nje, jibu lao ni bei. Mishahara midogo
kulinganisha na bei za chakula na mahitaji mengine. Nguo na viatu vipo
Mlimani City kwa ubora mkubwa lakini mfanyakazi wa hapo anakwenda
kufanya manunuzi Mwenge na Kariakoo.
Hali hiyohiyo, ibebe pia kwa
maeneo kama Quality Centre, Pugu Mall, City Mall, Dar Free Market na
vituo vikubwa vyote vya manunuzi Dar. Ni mfanyakazi lakini vilivyomo
ndani yake havimhusu kimatumizi.
Inatokea Dar, mke, mume na
watoto wote ombaomba. Kwao hiyo ni fursa. Wanagawana maeneo ya kuomba.
Mchana wakikutana kama vile hawajuani. Usiku wakiwa nyumbani hesabu
inafanyika. Ombaomba wana maisha mazuri kuliko wanaowasaidia.
Kuna watu Dar es Salaam maisha yao yana matokeo makubwa kuliko vipato
vyao. Magari wanayoendesha na maghorofa wanayomiliki. Hata hivyo, hakuna
wa kuwauliza fedha wanapata wapi.
Thubutu wewe upate mafao yako
kisha ufanye matokeo ya harakaharaka, uone jinsi utakavyoandamwa na
vyombo vya ulinzi na usalama, jumlisha maofisa wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA).
Dar ndipo hasa kwenye kuonekana tofauti ya
maskini na tajiri. Wakati mwizi wa TRA akimnunulia hawara yake Mercedes
Benz C Class ya kutembelea na kumjengea nyumba ya ghorofa mbili Goba,
mwalimu wa serikali ananyanyasika kwenye nyumba ya kupanga Tandale kwa
Bibi Nyau.
Hakuna watu wa uchumi wa kati, ukiwaondoa matajiri,
wote wanaobaki ni maskini. Hata hivyo, kundi hili la watu maskini ndilo
lenye kelele kuliko, watu wanatambiana, kutishana na kuoneshana umwamba.
Njoo Dar kisha pitiliza maeneo yetu yenye kuitwa Uswahilini ujionee
jinsi ambavyo michuano yetu maskini ilivyo. Watu wanashindana kununua TV
mpya, wanaoneshana umwamba kwa kufungulia sauti kubwa ya muziki.
Mikwara yetu nguo mpya. Wanasahau kuchanga karata za kuondoka kwenye
lindi la umaskini, wao wanajikita kwenye mashindano ya kuimbiana
Taarabu!
Nikujulishe mapema, Dar haina wabunifu. Ukija na wazo
lako la kufungua duka la kuuza kucha za kuku, miezi mitatu mingi, katika
huohuo mtaa wako kutakuwa na maduka arobaini ya biashara hiyohiyo. Nao
wanauza kucha za kuku! Dar watu wanaishi kwa kutegemea vichwa vya
wenzao.
Dar ya kamari. Siku hizi limeibuka la kubahatisha matokeo
ya mpira basi kila kona ni kubeti. Ni kama ambavyo watu walivyovamia
biashara ya maduka ya nguo. Tena asikwambie mtu, anayeiga anaweza
kufanikiwa kuliko mwasisi.
Siku hizi hatupumui na dawa za
kupunguza unene. Wataalamu wamekuwa wengi kwenye mitandao ya kijamii.
Mara dawa kutoka China. Siku akifa mtu ndiyo tutasikia makatazo ya
kutotumia dawa za kupunguza unene ambazo hazina TBS, lakini sasa hivi
kimya kimetanda. Watu wanendelea kutengeneza pesa kienyeji.
Ndani
ya Dar, mbunifu wa dawa ya asili ya kuongeza makalio atapata utajiri
mkubwa. Sijui watu huwa wanatafuta nini? Makalio makubwa, hipsi pana!
Eti awe na mvuto, mwisho ni kutaka tu kuvutia wanaume. Achana na Dar,
siku hizi mpaka mashoga wanatumia dawa za kukuza makalio na hipsi.
Wanasema Dar njoo na akili tu, tabia utazikuta hukuhuku. Jiji limejaa
watu wachafu kupata kuona. Mvua inyeshe, jiji zima linanuka kinyesi.
Magari ya kufyoza maji taka yapo lakini wanaona gharama, mvua ikinyesha
kidogo tu chemba zinafunguliwa.
Hujiulizi kwa nini Dar ndiyo
kiongozi wa kila kitu? Ukahaba, ushoga, uvivu, utapeli, majungu,
ufisadi, uchawi, ulevi, foleni na mengine mengi ya ajabu, ila utafanya
kosa kubwa kama utasahau kuhusu kipindupindu na utitiri wa waganga wa
kienyeji.
Ukiwa mganga wa kienyeji Dar unakuwa na nguvu kubwa.
Viongozi wa kitaifa watakuheshimu na kuja kukupigia magoti utafikiri
wewe ni Mungu. Mganga wa kienyeji anaaminika kuwa anatoa vyeo, anampa
mtu pesa, anampa mtu nguvu za kiume, anampa mtu mume, anatuliza nyumba
isiyumbe, anamfanya mlevi aache pombe. Kama unaijua mizizi japo miwili,
njoo Dar soko ni rahisi mno.
Watu wengi Dar wanaamini fedha za
kulala na kuamka tajiri zinapatikana. Ukifika Dar jitangaze wewe ni
Freemason na unagawa pesa. Weka wazi namba zako za simu. Mwenyewe
utatamani kuzima simu jinsi utakavyosumbuliwa. Na pesa utawalia.
Wapo waganga wa kienyeji matapeli na wanajulikana. Ni matajiri hasa,
utajiri wao unamaanisha kuumizwa na kufilisiwa wengine walioamini
wangefanikiwa kupitia mganga. Wanaendelea kuwepo. Ila kuwa makini,
ukijifanya kama wao ukaingia kichwakichwa utafungwa, wenzako wana
mitandao. Humuoni Manyaunyau yupo jela?
Najua una hamu ya kuja
Dar, karibu sana ila ukifika, ukiona watu wanafanya mazoezi usiku au
alfajiri, jifiche, wengi ni vibaka, watakupora kila kitu. Ukiwa
pembezoni mwa barabara na ukaona pikipiki inakukaribia, shtuka mapema,
ni vibaka hao.
Ukiwa Dar ndani ya gari dirishani unachati na simu
ama unaongea kwenye foleni au eneo ambalo barabara ni mbovu, moja kwa
moja vibaka hupiga mahesabu ya sehemu ya kukimbilia baada ya kukupora,
maana tayari wanahesabu simu yako ni mali yao. Vibaka wa Dar wana mikono
myepesi utadhani mshale wa sekunde.
Unaijua Mahakama ya Simu
wewe? Eneo linaitwa Tandale Kwamtogole. Wapo vijana wanajua kupora simu
utadhani walisoma kozi maalum. Wanaweza kuiba simu kwenye gari lililo
kwenye mwendo. Funga milango sawasawa, tia loki, vibaka wa Kwamtogole
hawajawahi kuwa watu wema kwa wamiliki wa simu.
Ni Dar ya fursa.
Matapeli wapo ‘bize’ kama mtu mwenye kazi nyingi za kiofisi. Wapo watu
wanapelekwa mpaka Ikulu, wanaoneshwa mlango wa rais, baada ya hapo
wanatapeliwa kwa jina la mkuu wa nchi. Usiulize kuhusu muhuri wa Ikulu
au saini ya rais, hayo ni mambo madogo mno kwa watoto wa mjini.
Fika Dar kisha nunua kiwanja na nyaraka zote uwe nazo, kesho nenda
kaulizie kiwanja, utapelekwa kwenye kilekile kiwanja chako. Utaoneshwa
mmiliki mwingine ambaye yupo tayari kwa biashara. Umeshaambiwa njoo Dar
na akili yako, maana ndiyo itakayokuongoza kuishinda mikikimikiki ya
jiji.
Dar zipo dakika 60 za ajabu mno, zinabadili kabisa mandhari
ya jiji. Ndiyo, ni dakika 60, yaani saa moja tu. Amka saa 10 usiku,
tembea barabarani maeneo mengi utajiona peke yako. Endesha gari,
utajikuta wewe pekee ndiye unaitawala barabara utakavyo.
Ingia
barabarani saa 11 alfajiri uone, tayari foleni za magari kila mahali. Ni
dakika 60 tu lakini tofauti yake ni kubwa. Sijui watu wa Dar huwa
wanaambiana kitu gani kuhusu saa 11.
Barabarani nako kila mtu
mbabe. Ukiwa dereva Dar lazima ujue kutukana. Barabarani Dar hakuna
mnyonge, watu wanaweza kusababisha foleni kwa kubishana tu. Shida ni
kuwa hakuna mtu mvumilivu wala wa kukubali kushindwa.
Mtu
anaendesha gari akiongea na simu matokeo yake anasababisha foleni. Gari
lingine linatembea kama kinyonga, kumbe ndani ni wapenzi wapo kwenye
mapenzi yao. Foleni za Jiji la Dar zinasababishwa na mambo mengi.
Kama utafanikiwa kumiliki gari au hata ukitumia la kazini au la ndugu,
usiku usikimbize sana. Malori na magari ya kuzoa taka yanaharibika hovyo
barabarani na yakiwa kwenye mwendo hutembea taratibu mno. Huwezi
kuliona mbele yako maana huwa hayana alama yoyote, hayana taa wala
‘riflekta’. Ajali nyingi za usiku ni magari madogo kuyavamia malori.
Yote hayo yanatokea kwa sababu barabarani hakuna taa. Mwanga pekee ni
wa taa za gari. Na ukiwa Barabara za Kawawa na Mandela ongeza umakini
usiku. Mandela malori, Kawawa magari ya taka. Ajali nje-nje. Barabara za
Ali Hassan Mwinyi, Nyerere, Bibi Titi na Sam Nujoma, zina upendeleo.
Taa za kuangazia barabarani zipo.
Ndani ya Dar, unaweza kudhani
mwalimu wa madereva wa bodaboda ni memba wa Al Qaeda au Isis. Uendeshaji
wao ni wa kujitoa mhanga. Analiona gari lipo kasi, analikimbiza,
analichomekea kwa mbele halafu anakata kona. Ukiwa na roho ndogo,
ukipanda bodaboda Dar, unaweza kuzimia au pengine kufa bila kugongwa kwa
mshtuko wa matendo ya dereva.
Magari ya Mwendo Kasi yapo Dar na
yalipoanzishwa ukaibuka upinzani wa jadi mwingine mjini. Achana na Simba
dhidi ya Yanga, Ali Kiba dhidi ya Diamond Platnumz, Manji dhidi ya
Mengi, uhasama mkubwa uliopo kwa sasa ni kati ya madereva wa mabasi ya
mwendo kasi dhidi ya bodaboda.
Tangu mradi wa Mabasi ya Mwendo
Kasi uzinduliwe rasmi, vifo vya waendesha bodaboda vimeharakishwa zaidi.
Barabara za mabasi hayo ndizo zinazotumiwa na bodaboda, ni tabu juu ya
shida.
Huwezi kuliona Dar ni jiji la matukio kama hushangazwi na
ajali za magari mengine dhidi ya Mabasi ya Mwendo Kasi. Magari hayo yana
njia zake, sasa ajali inatokea vipi? Watu wabishi Dar, unakuta katikati
ya mabasi ya mwendo kasi kuna gari la kawaida na wala dereva hana
wasiwasi. Anajiona anazo haki zote.
Watu wengi Dar ni ‘jobless’.
Usione msongamano Kariakoo ukadhani watu wapo ‘bize’, wengine wanakwenda
kupoteza muda na kuangalia vya kuokota. Ukitaka kutambua hilo, ona
jinsi tangazo la mabasi ya mwendo kasi, lilipoeleza usafiri ni bure.
Watu kutwa nzima waling’ang’ania magari, vituo vikajaa. Kariakoo watu
walipungua. Vibaka wote walihamia kwenye magari ya mwendo kasi.
Dar ndiyo jiji la watu wenye kuamini vitu vya kufikirika kwa haraka.
Anzisha tu uzushi wako kuwa kuna mtu alikuwa anatembea Kariakoo,
kikatokea kiumbe cha ajabu kikamkwapua na kupaa naye mawinguni. Stori
itaenea hiyo na vyombo vya habari vitaripoti huo uvumi.
Usibishe,
ilishatokea habari ya mwanamke kuota manyoya kwenye mkono baada ya
kumpa pesa ombaomba, Selander Bridge. Eti baada ya muda yule mwanamke
aliyeota manyoya alianza kulia mkono wake kisha naye akatoweka na gari
nalo likatoweka. Watu wakaamini, vyombo vya habari vikaripoti. Dar
usiichezee!
Dar watu wapo bize sana lakini ubize wao ni ngono. Na
kama ingekuwa ni amri yao, wasingekuwa wanafanya kazi. Maofisini utoro
na ruhusa nyingi lakini wakipata pesa ni pombe na ngono zembe. Mishahara
ikishalipwa tu watu hawaonekani kazini. Baa na nyumba za kulala wageni
zinajaa. Akili za watu wa Dar zinawatoshaa wenyewe!
Vituko vya
Dar, kwa kawaida mvua ikinyesha ni ishara ya neema, mashambani mazao
yatastawi, hivyo kuleta matokeo mazuri kipindi cha mavuno. Kwa Dar mvua
ikinyesha tu nyumba za kulala wageni zinajaa. Watu wanakwenda kujifungia
vyumbani kupeana joto nyakati za baridi. Usiseme Dar imelaaniwa!
Wapo watu kuingia gesti ni lazima kuliko kula. Yupo radhi akope pesa au
aende gesti akatumie chumba kwa mkopo. Hata kondomu wanakopa.
Anayefanya yote hayo, nyumbani kwake ana mke ambaye hajagoma kumhudumia.
Akili za baadhi ya watu wa Dar ni kama zimeliwa na mchwa!
Ni Dar
ambako kiongozi wa kanisa anatuhumiwa kupora mke wa mtu na kudhulumu
mali za mume, kisha kesi inafika mahakamani, mwingine ananyooshewa
kidole kumjaza mimba mke wa mtu, lakini Jumapili inayofuata makanisa ya
viongozi hao yanajaa kuliko mwanzo. Vivutio vya utalii ni vingi Dar.
Shehe naye anafumaniwa na kibinti kidogo, anafungishwa ndoa ya mkeka,
asubuhi anaamkia Msikitini, anapita mbele anasalisha kisha anatoa
mawaidha ya kuonya kuhusu zinaa. Ni hapo ndipo unaambiwa achana na
matendo, zingatia maneno.
Dar kila kitu kina upambe. Wapo wapambe
wa biashara, wapo pia wa wanawake. Yupo mtu Dar kazi yake ni kutafuta
wanawake wazuri ili akamshawishi tajiri fulani wapate pesa. Utakuta mtu
yupo ‘bize’ kutafuta warembo utadhani anaandaa shindano la mamisi, kumbe
anahangaikia ugali wake. Kazi za watu wengine Dar, hata kujitambulisha
wanafanya kazi gani wanaona aibu.
Ukishaingia Dar, ukiwa na pesa
wapambe watakufikia tu. Wao wakijua tu pesa ipo lazima waje.
Watakuchunguza kitu unachopendelea na baada ya kukuelewa mahitaji yako,
utategwa mpaka utaingia.
Ukija Dar sitaki maswali ya kijinga.
Usije kuniuliza mzee wangu Reginald Mengi alimpataje Jacqueline
Ntuyabaliwe ‘K-Lynn’. Tutagombana ukinihoji ni kwa nini Wema Sepetu
anaonekana anaishi maisha bei mbaya mjini wakati mapato yake hayaakisi
chochote katika matumizi yake.
Ukitaka nikukatie simu na siku
nyingine ukinipigia nisipokee, basi uniulize ni kwa nini viongozi
serikalini wanawatolea udenda wasanii wa kike Bongo Movie na kwa nini
kila mmoja hujifanya yupo nao karibu ili awasaidie, wakati watu wengi tu
wenye uhitaji mkubwa hawasaidiwi. Ni kawaida yangu tangu kitambo kwamba
huwa sipendi maswali chonganishi.
Usirogwe kuniuliza ni kwa nini
warembo maarufu siku hizi wanakuwa na uswahiba na mashoga. Yaani
kumkuta Kajala au Jokate na shoga ni kitu cha kawaida. Usiniulize kwa
nini kwa sababu sitaki tu kuingilia maisha ya watu. Na ukisema kuwa
mashoga hao wana kazi maalum kwa warembo hao, sitajibu kitu.
Warembo wengi Dar wamechoshwa na wanaume, wanasema ni pasua kichwa,
wamevamia fani ya usagaji. Mwanamke na mwanamke wanavyobembelezana na
kuoneana wivu ni shida! Kama huko ulipo hayajafika njoo Dar uyashuhudie.
Ukifika Dar kama ukitaka kumbi za starehe zenye kuonesha shoo za
wanawake wakiwa watupu, zipo. Na zina leseni. Maonesho ya ngono pia
yapo. Labda tu kama wewe hujui maeneo.
Ukitaka kumbi za starehe
Dar zimejaa. Utapata kila burudani uitakayo. Unafahamu balaa la vituo
vya massage wewe? Ukifika sikushauri uende, vinginevyo utakuwa kila mara
mtaji unakata kwa massage. Ndiyo ni massage na wengi wao siyo massage
tu, ni massage timilifu.
Dar ya vurugu mechi, vigogo wanachepuka
na mabinti wadogo, wake zao nao wanajidai na vijana wadogo. Hakuna kazi
ngumu kwa mtoto wa kiume kama kuwapaka wanawake rangi za kucha na
kuwachua miguu yao. Siku ukiambiwa ukamkande miguu nyumbani kwake
jiandae tu. Usisahau kuhusu uwepo wa maradhi. Kumbuka pia mwenye mali
akikukuta ni kiyama chako.
Akina dada nguo zimekuwa nzito,
hawataki kuvaa. Viguo vifupi vyenye kubana. Mavazi ya kuonesha maungo ya
faragha. Mwanafunzi anavyovaa hana tofauti na changudoa anayejipanga
barabarani.
Machangudoa Dar ni zaidi ya unaowajua. Wapo wanawake
maofisini wanafanya mapenzi kwa pesa. Askari polisi, wanajeshi, viongozi
mbalimbali na kada nyinginezo. Wapo pia wake za watu, makundi yote hayo
yanafanya mapenzi kwa pesa. Ni kujiuza tu!
Hii ndiyo Dar, mke wa
mtu anatoka na gari nyumbani kwake, anafika analipaki Dar Free Market,
kisha anapanda gari la mchepuko, wanakwenda kufanya yao. Mtu akiliona
gari pale, anaamini yupo ndani kwenye manunuzi. Baada ya kazi
anarudishwa palepale, anachukua gari lake, anaendesha kurudi nyumbani.
Dar kwa ubunifu wa ngono watu wamefuzu.
Karibu sana Dar, uje uone
Bismini, yaani ule Mnara wa Askari ambao kama yule mbunge wetu atakuwa
rais siku zijazo, basi utageuzwa kuwa Sanamu la Diamond Platnumz.
Ndimi Luqman Maloto
No comments:
Post a Comment