Na Mwandishi Maalum
Port Moresby - Papua New Guinea
2 June 2016,
Makamu
wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameanzisha majadiliano kuhusu
umuhimu wa kumwezesha mwanamke kiuchumi kwa viongozi wa nchi za Afrika,
Caribbean na Pacific (ACP) wakati wa Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi
hizo uliofanyika Port Moresby, nchini Papua New Guinea.
Katika
mkutano huo wa siku mbili uliomalizika jana nchini humo, Makamu wa Rais
alikuwa mtoa mada mkuu katika majadiliano ya kumwezesha mwanamke
kiuchumi ambayo yalifanyika sambamba na Mkutano wa Wakuu wa nchi na
Serikali.
Makamu wa Rais ni miongoni mwa wajumbe wa Jopo
la Ngazi ya Juu la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon ambalo
liliundwa kusaidia kufanya uchambuzi na kutoa mapendekezo ya namna ya
kuchagiza kasi ya kuwezesha wanawake kiuchumi kupitia Ajenda ya mwaka
2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu. Jopo hilo linakusanya maoni,
uzoefu na miongozo kutoka kwa wadau duniani kote kupitia majadiliano.
Mheshimiwa
Samia aliuambia mkutano huo kuwa uwezo mkubwa walionao wanawake kama
wazalishaji wakuu bado haujatumika kikamilifu kwa miongo yote katika
kuchangia maendeleo ya kiuchumi katika nchi zao licha ya kwamba wao ni
takribani nusu ya nguvu kazi ya dunia na kama wakiwezeshwa mchango wao
unaweza kufikia zaidi ya trilion 20 ya pato la dunia.
Alisema
kuna umuhimu wa serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kuhakikisha
kuwa wanawekeza katika kuwezesha wanawake kiuchumi ili kufanikisha
Ajenda 2030 jambo ambalo litapelekea kupatikana kwa usawa wa kijinsia,
kuondokana na umaskini na hatimaye uchumi kukua.
"Pamoja
na maendeleo yaliyofikiwa, bado uwiano wa kijinsia umebaki kuwa mkubwa
kwa wanawake katika sehemu zote za fursa za kiuchumi na matokeo, katika
nchi zote wanachama," alisema Mheshimiwa Samia.
Makamu
wa Rais alielezea matumaini yake kwamba uchumi imara ambao unaonekana
katika nchi za ACP katika miaka ya hivi karibuni utaendelea kukua na
kusisitiza umuhimu wa kuondoa tofauti za kiuchumi baina ya wanawake na
wanaume ili kujenga uchumi ulio imara.
“Mara
nyingi juhudi zimefanyika za kuleta usawa wa wanawake, kwa mwanamke
mmoja mmoja, katika familia, na kama mwananchi, dunia yetu imeendelea,
na wote tumepata ustawi," alisema na kuongeza
"Kwa
hiyo, tuwe na uhakika wa elimu bora, ajira za uhakika, upatikanaji wa
huduma bora za afya na maisha huru bila ukatili na ubaguzi viwe
vinawafikia kwa urahisi wanawake na wasichana ili kuleta usawa miongoni
mwa jamii. Hivi vigezo vina muunganiko wa moja kwa moja na fursa za
kiuchumi, uwezo wa mlaji wa kufanya manunuzi na hatimaye kukua kwa
uchumi."
Matokeo
ya majadiliano ya katika mkutano huo yatasaidia kushawishi kazi ya Jopo
hilo na kuhakikisha mtazamo wa kikanda unaingizwa katika ripoti ya
kwanza itakayowasilishwa na jopo hilo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa mwezi Septemba 2016
No comments:
Post a Comment