JAMII nchini imehimizwa kujenga utamaduni wa kupanda miti ili
kuirejeshea Zanzibar uoto wa asili na kuiepusha na janga la
kimazingira.Akizindua zoezi la upandaji miti lililofanyika pembezoni mwa
uwanja wa soka wa klabu ya Malindi mjini Zanzibar, mjumbe mstaafu wa
Baraza la Wawakilishi Ali Mzee, amesema miti ni uhai kwa kila binadamu.
Mzee alisema ni jambo la kusikitisha kwamba mazingira ya Zanzibar
yamegeuka kutoka rangi ya kijani iliyokuwepo zamani na kuwa yabisi, hali
inayosababisha kuongezeka kwa joto.“Bila miti, viumbe hutaabika na nchi
inakuwa kavu na maradhi hasa presha huongezeka kila uchao. Lazima
tuzinduke kwani tusipopanda miti, tunakaribisha janga kwa taifa,”
alisema Mzee.
Aidha alivitaka vyombo vya habari kuandaa vipindi na makala
mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa
kupanda miti.
Mapema, Mwenyekiti wa jumuiya ya Green World Family Foundation
iliyodhamini zoezi hilo Nazir Ahmad Bachoo, alisema jumuiya yake
inathamini mazingira na imeamua kulifanya zoezi la upandaji miti kuwa
endelevu.
Alisema ni jambo lililo wazi kwamba dunia nzima sasa inalia na hali
ya joto litokanalo na ongezeko la hewa ukaa (carbon dioxide),
inayosababishwa na upungufu wa miti na kuongezeka kwa vyombo vya usafiri
barabarani vinavyozalisha moshi kwa wingi.“Umefika wakati sasa kila
mmoja ahamasike kupanda na kuitunza miti katika eneo analoishi na yale
yanayomzunguka, ili ilete manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho,”
alisisitiza.
Kwa upande wake, mratibu wa zoezi hilo na mwanaharakati wa mazingira
Mohammed Abdulrahman Bajbeir, alisema Zanzibar imejaaliwa kuwa na
wataalamu wengi wa masuala ya mazingira, lakini bado hawajatumika
kikamilifu kuisaidia nchi.
Kwa hivyo amezishauri mamlaka za juu kutanabahi na janga la
kimazingira linaloinyemelea Zanzibar kutokana na utashi wa binadamu
ambao wamekuwa wakikata miti ovyo bila kupanda mingine.
“Zanzibar ya sasa sio kama ile ya zamani ambayo ilijaa kila aina ya
miti pembezoni mwa barabara na mitaani. Tunafyeka miti kujenga nyumba za
makaazi na maduka tukisahau kwamba miti ni muhimu kwa uhai wetu.
Tubadilike,” alieleza Bajbeir.
Wananchi mbalimbali wa mitaa ya Malindi, Mchangani na Mbuyuni
wakiwemo wanasoka wa zamani wa klabu ya Malindi SC walioshiriki zoezi
hilo, walieleza umuhimu wa kuilinda miti hiyo ili kuunusuru uwanja wa
michezo, kwani umekuwa ukiharibiwa sana na watu wanaoweka magari pamoja
na mifugo.
Jumla ya miti 41 ya aina mbalimbali ilipandwa kuzunguka uwanja huo,
na itakuwa ikilindwa na wananchi kwa kushirikiana na vijana wa ulinzi
shirikishi na polisi jamii wa shehia ya Malindi.
No comments:
Post a Comment