TAN
Bayport
Kikoa
Myway entertainment
FORE PLAN CLINIC
MPINGA CUP 2016
Mashujaa Fm 89.3, Lindi
Friday, June 3, 2016
SHIMUTA wataka wanamuziki wasio na maadili kupuuzwa
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Shirikisho la Muziki Tanzania limewataka wananchi kuwapuuza wanamuziki wasio na maadili ili kuondokana na mmomonyoko wa maadili unaosababishwa na shughuli zao za kimuziki.
Tamko hilo limetolewa leo Jijini Dar es Saalam na Rais wa Shirikisho hilo, Addo November alipokua akimtambulisha Katibu Mkuu wa Shirikisho la muziki ambaye ni John Kitime.“Mchakato wa kumtafuta Katibu Mkuu tumeufanya bila kukurupuka, nimefarijika sana kwa kukubali kwake ili kuhakikisha tunawakwamua wanamuziki kwasababu changamoto za muziki tulizokuwa nazo ni nyingi ikiwemo ya wanamuziki wasio na maadili”, alisema November.
November aliongeza kuwa changamoto kubwa ni Sheria mbovu ya Haki Miliki ambayo mchakato wa kuirekebisha sheria hiyo pamoja na marekebisho ya sera ya utamaduni upo katika hatua za mwisho pia shirikisho limefanya jitihada za kuweka kipengele kinachozungumzia masuala ya sanaa kama haki ya msingi katika mchakato wa katiba mpya.
Aidha, alisisitiza kuwa shirikisho hilo halipo kwa kumsaidia mwanamuziki mmoja mmoja bali ni kuhakikisha mfumo mzima wa muziki nchini unaweza kuwanasua wanamuziki wote na tasnia kiujumla ili muziki uwe na heshima.Naye, Katibu Mkuu mpya wa Shirikisho hilo, John Kitime amesema kuwa anategemea kutoa elimu kwa wanamuziki kuhusu kazi zao kupitia semina mbalimbali pamoja na kuimarisha shirikisho hilo ili vikundi vya wanamuziki viweze kusimama na kukuza muziki ili iwanufaishe wanamuziki wenyewe.
“Sheria ya Haki za Binadamu namba 245 iko wazi kuwa kila mtu anastahili kupata mafao yake yanayotokana na ubunifu wake kwahiyo kutowalipa ni kuvunja haki hiyo ya binadamu, kazi kubwa tuliyonayo ni kuwaelimisha wanamuziki kufahamu haki zao”, alisema Kitime.
Shirikisho la Muziki Tanzania linajumuisha mwanamuziki mmoja mmoja pamoja na vikundi ambalo limeundwa na vyama 7 ambavyo vimesajiliwa na Baraza la Sanaa Tanzania vifuatavyo; Chama cha Muziki wa Taarabu, Chama cha Muziki wa Rhumba, Chama cha Muziki wa Dansi, Chama cha Muziki wa Asili, Chama cha Muziki cha Wapiga Muziki wa Diski, Chama cha Muziki wa Kizazi kipya pamoja Chama cha Muziki wa Injili.
No comments:
Post a Comment
Newer Post
Older Post
Home
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment