TAN
Bayport
Kikoa
Myway entertainment
FORE PLAN CLINIC
MPINGA CUP 2016
Mashujaa Fm 89.3, Lindi
Sunday, May 29, 2016
MAKONDA, MTOTO WA KABWE WOTE WAPO SAWA!
NA:LUQMAN MALOTO
MJADALA ukachukua nafasi. Mtoto wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, marehemu Wilson Kabwe, aligoma kumpa mkono Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, wakati wa tukio la kumuaga baba yake.
Watu na matukio, kitendo hicho cha mwana wa Kabwe kumnyima mkono Makonda kikachukua nafasi pana baada ya tukio la Charles Kitwanga kuondolewa kazini Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kile kilichoelezwa kwamba aliingia bungeni akiwa amelewa.
Ilikuwa kwenye Viwanja vya Karemjee, Dar es Salaam mapema wiki hii. Baada ya kifo cha Kabwe mwenye rekodi ya kuitumikia serikali kwa zaidi ya miongo mitatu, kifo kikamkuta, Jumanne wiki hii akawa anaagwa. Makonda akahudhuria.
Siyo jambo la kupepesa macho kufahamu kuwa Kabwe na Makonda hawakuwa kwenye kipindi kizuri. Hawakuwahi kutamka kuwa na tofauti yoyote, lakini asili ya binadamu inafahamika kuwa hakuna mwenye kupenda kujeruhiwa hata kama ni kwa haki.
Kila mmoja anapofanya makosa ya wazi, hupenda asamehewe. Hakuna mwenye kuridhika kuchukuliwa hatua kali. Ndivyo ilivyo, hata kama ilikuwa kweli kuwa Kabwe alifanya madudu kwenye mikataba ya mabasi, Stendi ya Ubungo, Dar es Salaam, kibinadamu hakufurahia namna alivyochukuliwa hatua.
Aprili 19, mwaka huu, Rais John Magufuli alimsimamisha kazi Kabwe hadharani, ikiwa ni baada ya Makonda kumpa ripoti ya udanganyifu wa mkataba aliosema ulisainiwa na Kabwe, ambao umeisababisha serikali hasara ya shilingi bilioni 42 ndani ya miaka sita.
Rais Magufuli baada ya kupewa taarifa hiyo, aliuliza wananchi afanye nini, wananchi wakajibu: “Mtumbueeee!” Akauliza tena: “Nimtumbue hapahapa?” Nao wakaendelea kusisitiza: “Mtumbueeee!”
Basi, Rais Magufuli akakosa ajizi zaidi ya kutii kauli ya wapiga kura wake waliomuingiza mamlakani, akasema: “Kuanzia leo, namsimamia kazi Kabwe.” Baada ya kauli hiyo, umati ukalipuka kwa shangwe. Naam, maumivu ya mtu yanaweza kuwa sherehe kwa jirani.
Makonda alitangazwa shujaa siku hiyo. Hata Rais Magufuli alimpongeza kweli. Upande wa pili ni kosa kufikiria kuwa Kabwe na familia yake walitabasamu kwa hatua lile.
Zingatia, lilikuwa tukio kubwa lililovuta macho ya watu kila kona ya nchi, maana ndiyo ulikuwa uzinduzi wa daraja la kihistoria jijini Dar es Salaam na Tanzania yote, vilevile Afrika Mashariki na Kati kwa jumla. Daraja la Kigamboni au Daraja la Mwalimu Nyerere.
Nani angependa kutumbuliwa kama alivyotumbuliwa Kabwe katika mazingira yale? Kabwe hakuwahi kuhukumiwa, zilikuwa ni tuhuma tu lakini hata kama nafsi yake inamwambia alichokifanya ndicho kilichoelezwa na Makonda bado hawezi kuona sawa kutenguliwa mbele ya kadamnasi namna ile.
Mwananchi wa kawaida ambaye anachukia rushwa na kwa muda mrefu amekuwa akiumizwa na matendo ya ufisadi, lazima afurahie jinsi ambavyo Kabwe alitumbuliwa. “Jipu dawa yake ni kulitumbua, siyo kulipapasa,” sauti ya Dk Magufuli hiyo.
Vilevile, ukweli utambulike kuwa Makonda alikuwa sahihi kuyasema aliyoyasema hadharani mbele ya Rais Magufuli kwa sababu yeye ndiye alishuhudia uozo alioamua kuusemea. Wanahitajika viongozi ambao wanaweza kuyasema madudu ya watu bila hofu ili taifa liendelee.
Makonda pia alikuwa sahihi kuhudhuria tukio la kumuaga Kabwe baada ya kufariki. Uhudhuriaji wake ulikuwa na majibu kuwa nje ya kazi zake hana chuki binafsi na Kabwe. Na kwamba hata kitendo chake cha kumwanika hadharani madudu aliyoyaona, hakikusukumwa na mapambano binafsi.
Kwamba alisukumwa na kazi, hicho ndicho alichokisimamia. Asingehudhuria mazishi ya Kabwe, ingeonekana ana vitu vingine pembeni. Kiongozi hatakiwi kuhisiwa, kuonekana wa kuthibitika kufanya uamuzi kwa msukumo wa hisia binafsi.
Zaidi ya hapo Makonda alionesha ukomavu wa kiuongozi kwa kuhudhuria kwake. Awali lilishatoka tangazo la kumkataza asiende kumuaga Kabwe. Upande wa pili mwenyewe alisema alitumiwa ujumbe wa kumkataza, lakini akatanguliza ubinadamu mbele, akaenda.
Siyo uongo kuwa baada ya tukio la kifo cha Kabwe, macho ya wengi yalimwelekea Makonda. Na alitazamwa kwa kile ambacho angetenda au kukisema. Wapo watu walitengeneza ujumbe wa kejeli za kufikirisha, kuyatangulia matendo au matamshi ya Makonda juu ya kifo cha Kabwe.
Hivyo, ni kweli kuwa Makonda alikabiliwa na presha kubwa lakini mwisho alihudhuria. Angeongozwa na hofu inayotokana na macho ya watu asingekwenda Karemjee. Nasisitiza Makonda alikuwa sahihi kabisa.
Kuhusu mtoto wa Kabwe kumnyima mkono Makonda, wakati mkuu huyo wa mkoa alipokwenda kuwapa mkono wa pole familia ya marehemu, naye pia alikuwa sahihi kabisa. Nasisitiza mtoto wa Kabwe alikuwa sawa kwa uamuzi wake.
Kuna mambo ambayo watu hushindwa kuyaweka akilini, kwamba yapo maisha ya mtu kikazi, uhalifu wake au dhambi zake na mtazamo wa jamii. Vilevile yapo maisha ya kifamilia kwa mhalifu na mtazamo wa wanafamilia kwa mtu wao.
Kibaka anaweza kuwa msumbufu mtaani na watu wakataka kumuua lakini wazazi wake wakamlinda. Watamficha asipatwe na madhara yoyote. Ni kibaka kwa jamii lakini ni mtoto ndani ya familia. Damu ni nzito mno!
Baba anaweza kuwa jambazi lakini ukimwambia mtoto kuwa mzazi wake ni jambazi kama ana nguvu atakupiga, ikiwa hana atachukia au atalia. Uhalifu wa mtu, hata kama utakuwa unathibitika, ni vigumu kumfanya achukiwe na ndugu zake.
Nimelazimika kusema hivyo kwa sababu watu wengi wamekuwa wakitoa maoni mbalimbali. Wanaomtetea Makonda wanamponda mtoto wa Kabwe kuwa hajui kutofautisha maisha ya kazi za serikali na mambo binafsi.
Wanaomponda mtoto wa Kabwe, nao wanashindwa kupata picha kuwa siku ya tukio, mtoto huyo hakumuona Makonda akitumbua jipu, bali alimshuhudia akimdhalilisha kama siyo kumharibia maisha ya kikazi baba yake.
Unaweza kumuona Kabwe ni jipu au vyovyote unavyotaka lakini huwezi kupinga ukweli kuwa ni baba wa watu. Makonda atakuwa alifikiri vibaya kama kwa kile alichokifanya, hakutarajia mapokeo hasi kutoka kwa familia ya Kabwe.
Watu wanaweza kumuona Kabwe ni mtu mbaya, aliyeisababishia hasara serikali, lakini kwa mtoto wa Kabwe hawezi kumuona hivyo. Kwake Kabwe alikuwa baba bora. Kama wewe unaye baba yako bora, basi naye wake ni huyo Kabwe.
Nani ambaye anaweza kushangilia baba yake kutumbuliwa? Fikiria ndani kabisa, uulize moyo wako kama hutakuwa tayari kumlinda baba yako kwa makosa yake. Bila shaka unakiri kuwa baba ni baba tu.
Wangapi wanao wazazi pasua kichwa lakini wanawalinda? Wazazi wasiotambua hata wajibu wao lakini watoto wanawalinda kadiri inavyowezekana. Hiyo ndiyo tabia ya damu. Uzito wake ni mkubwa mno.
Hivyo basi, mtoto wa Kabwe alikuwa sahihi kabisa. Alituma ujumbe kwa jamii kuwa Kabwe ni baba yake na yupo tayari kumfia kwa chochote.
Vilevile tambua kuwa Kabwe kama alipata nafasi kuzungumza na familia yake kuhusu tukio la kutumbuliwa kwake kabla hajafa, hakuwaambia wanaye kuwa alichokisema Makonda ni sahihi. Nani anaweza kusema hivyo.
Bila shaka alisema alisingiziwa, hivyo ulitaka mtoto wa Kabwe achekelee wakati ndani yake anajua baba yake alisingiziwa? Kuna elimu kubwa ndani yake kama utaifikirisha akili.
Ndimi Luqman Maloto
No comments:
Post a Comment
Newer Post
Older Post
Home
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment