Na Anna Nkinda – Maelezo, Kagera
…………………………………………
 Serikali Mkoani Kagera 
imevikopesha vikundi  mbalimbali vya maendeleo vya vijana kupitia Vyama 
Vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) zaidi ya shilingi milioni 83 katika 
kipindi cha miaka mitano iliyopita ilikuwawezesha vijana waweze  kujiajiri wenyewe na kujikwamua  kiuchumi .
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa
 huo Kanali Mstaafu Fabian Massawe wakati akisoma taarifa fupi ya mkoa 
 kwa  Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella 
Mukangara aliyepo mkoani humo kwa ajili ya kuangalia jinsi  fedha za 
mkopo kutoka mfuko wa vijana  zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua 
kimaisha.
Kanali Mstaafu Massawe alisema 
kuwa Serikali  inasimamia utekelezaji wa sera ya maendeleo ya vijana kwa
 kuratibu shughuli za mifuko ya vijana na kufuatilia utoaji na 
urejeshaji wa mikopo, kuhamasisha vijana na kufufua moyo wa kujitolea na
 kukuza na kuendeleza vipaji mbalimbali walivyonavyo vijana ili 
kuwawezesha kujiajiri kupitia mafunzo yanayohusu stadi za kazi na maisha
“Changamoto tunazokabiliana  nazo 
katika kuwakopesha vijana ni mahitaji makubwa ya mkopo ukilinganisha na 
uwezo wa SACCOS au wakopeshaji wengine, urejeshaji hafifu wa mikopo 
kutoka kwa wakopaji, ukosefu wa ajira, uvivu na uzurulaji, vijana kutaka
 mafanikio kwa haraka  na matumizi ya madawa ya kulevya kwa baadhi ya 
vijana”, alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Aliendelea kusema kuwa ili 
kukabiliana na changamoto hizo Serikali ngazi ya mkoa inafuatilia kwa 
karibu ili kuona kwamba matamko ya sera ya Taifa ya Maendeleo ya vijana 
yanazingatiwa na kuingizwa katika  maendeleo ya Halmashauri lengo kuu ni
 mkoa kuwa na vijana wenye ari ya kuwajibika na kushiriki kikamilifu 
katika maendeleo ya jamii, wazalendo, wenye maadili na kupenda nchi yao.
Kwa upande wake waziri Dk. 
Mukangara alisema kuwa hivi sasa Serikali inaangalia uwezekano wa 
kuongea mkopo kwa SACCOS zinazolenga shughuli za maendeleo ya vijana 
 kutoka shilingi milioni tano hadi kumi kwani mahitaji ni makubwa na 
hayakidhi haja.
 Mkoa wa Kagera unakadiriwa kuwa 
na idadi ya watu 2,739,492 kati ya hao wanawake 1,386,669 na wanaume 
1,353,123 ambapo vijana ni 903,608 wenye umri wa miaka 15 hadi 35 sawa 
na asilimia 33 ya wakazi wote ambapo  kati ya hao wa kike ni 459,867 na 
wa kiume 443,741.

No comments:
Post a Comment