TAN
Bayport
Kikoa
Myway entertainment
FORE PLAN CLINIC
MPINGA CUP 2016
Mashujaa Fm 89.3, Lindi
Sunday, June 5, 2016
VISIMA VINGI DAR VIMECHIMBWA BILA KUFUATA UTARATIBU.
Na Fatma Salum- MAELEZO, Dodoma.
Serikali imesema kuwa visima vingi Jijini Dar es Salaam vimechimbwa bila ya kufuata kanuni na taratibu za uchimbaji hivyo maji yake si salama kwa matumizi ya binadamu.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Mhandisi Gerson Lwenge aliyasema hayo wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake Bungeni mjini Dodoma.
Mhe. Lwenge alibainisha kuwa katika kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu uliotokea mwezi Agosti 2015 Jijini Dar es Salaam na kuenea nchini, Serikali ilifanya uchunguzi wa sampuli za maji ya visima 108 vya jijini humo na matokeo ya uchunguzi huo yalionesha kuwa visima 66 maji yake si salama.
“Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wadau wengine ilifanya ukaguzi na kupima uwepo wa vimelea vya vijidudu vya ugonjwa huo katika visima vya maji vinavyotumika jijini Dar es Salaam na sampuli za maji ya visima 108 zilichukuliwa, kati ya hivyo visima 20 vifupi na visima 46 virefu maji yake yaligundulika kuwa si salama. Kwa ujumla visima vingi vilivyopo kwenye maeneo ya watu vimechimbwa bila ya kufuata kanuni na taratibu.” Alisema Mhe. Lwenge.
Aidha, Waziri Lwenge alisema kuwa Serikali pia ilifanya ukaguzi wa ubora wa maji kwenye vyanzo vya maji katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Mara, Manyara, Kagera, Kigoma, Morogoro na Dodoma ambapo vyanzo vya maji vipatavyo 600 vilikaguliwa na kubaini kuwa maji yaliyo salama ni chini ya asilimia 40.
Mhe. Lwenge alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) imekamilisha uandaaji wa miongozo ya utekelezaji wa Mpango wa Usalama wa Maji (Water Safety Plan) kwa Vyombo vya Watumiaji wa Maji na Mamlaka za Maji.
“Miongozo hiyo inakusudia kuboresha huduma za upatikanaji wa maji safi na salama kwa Mamlaka za Maji na Vyombo vya Watumiaji wa Maji Vijijini (COWSOs) kuanzia kwenye chanzo cha maji hadi kwa mtumiaji.” Alifafanua Mhe. Lwenge.
Kutekelezwa kwa mpango huo kutaboresha usimamizi wa usalama wa maji katika vyombo hivyo na kuwaepusha wananchi kutumia maji yasiyo salama pamoja na kupunguza upotevu wa maji katika mifumo ya kusambaza maji kote nchini.
No comments:
Post a Comment
Newer Post
Older Post
Home
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment