Naibu
Waziri wa Maji, Amos Makalla mara akiwa amesimama pembeni ya mradi wa
Kijiji cha Managhat, Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara,pamoja na Katibu
Tawala wa Mkoa wa Manyara, Omari Chambo na Mkurugenzi wa Mji wa Babati,
Omari Mkombole mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huo.
Naibu
Waziri wa Maji, Amos Makalla na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera
wakikata rasmi utepe, kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye jengo jipya
la Mamlaka ya Mji wa Babati.
Naibu
Waziri wa Maji, Amos Makalla, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera,
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Omari Chambo (mwisho kushoto) na
Mwenyekiti wa Bodi ya BAWASA, Mashughuli Minja (anayefuatia)
wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Babati (BAWASA),
Iddi Msuya ndani ya jengo jipya la Mamlaka ya Maji Babati.
Naibu Waziri wa Maji akikagua pampu ya kusukumia maji kwenye chanzo cha maji cha Masika, Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara.
…………………………………………………………………….
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla
amesema wananchi hawatafaidika na miradi ya maji inayotekelezwa na
Serikali hivi sasa, kama hawatakuwa makini kuvitunza na kuvilinda vyanzo
vya maji.
Mhe. Makalla amezungumza hayo jana katika ziara yake wilaya ya
Babati, mkoa wa Manyara wakati akikagua utekelezaji wa miradi na
kuzindua miradi iliyokamilika katika mkoa huo.
“Miradi hii inayotekelezwa na Serikali hivi sasa, haitakuwa na
maana kama hatutaacha uharibifu wa vyanzo vya maji tulivyonavyo, ambao
unatokana na shughuli za kibinadamu za kila siku ndani au kandokando ya
vyanzo hivyo. Miundombinu tunayoiweka haitakuwa na maana na itabaki kuwa
kama magofu kama hatutakuwa na vyanzo vya maji vya kudumu”, alisema
Mhe. Makalla.
“Imefika wakati wananchi waamue na kuchukua hatua thabiti ya
kutunza na kulinda vyanzo vya maji, la sivyo juhudi kubwa zinazofanywa
na Serikali zitakuwa bure na kuingia gharama kubwa bila faida yoyote.
Wananchi naomba mtupe ushirikiano katika hili, ili sisi tuweze
kuhakikisha tatizo la maji katika nchi yetu linafikia kikomo”, aliongeza
Mhe. Makalla.
Naibu Waziri alisema kuwa miradi hii inagharimu mamilioni ya
shilingi na Serikali imedhamiria kuwapa wananchi maji na si vinginevyo,
lakini bila ushirikiano wao lengo letu halitafanikiwa. Hasa ukichukulia
maeneo mengi ambapo miradi imetekelezwa kwa ufanisi, imechangiwa na
ushirikiano mzuri unaopata Serikali kutoka kwa wananchi wake.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera alishukuru jitihada za
Serikali za kutatua tatizo la maji nchini kote, na alitoa agizo kwa
viongozi wa mkoa mpaka vijijini, kuhakikisha kuwa wanachukua sheria kali
na kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa dhidi ya uharibifu wa vyanzo
vya maji. Huku akisisitiza sheria ya kutofanya shughuli zozote za
kibinadamu umbali wa mita 60 kutoka chanzo cha maji izingatiwe na
kuahidi kama Mkuu wa Mkoa atalifanyia kazi ipasavyo.
Hii imetokana na maeneo mengi ya vyanzo vya maji vya miradi
mingi kuonekana haitunzwi vizuri katika wilaya za Hanang na Babati, huku
shughuli nyingi za kibinadamu hasa kilimo zikionekana kushamiri katika
vyanzo hivyo na kuleta changamoto kubwa katika utekelezaji wa miradi ya
maji mkoani Manyara.
No comments:
Post a Comment