NA BASHIR YAKUB-
Upo wakati kwenye
ndoa
ambapo mmoja wanandoa anaweza akawa anataka kuuza au kubadili jina la
nyumba/kiwanja bila ridhaa ya mwenzake ilihali nyumba
hiyo ni ya familia. Lakini pia
nje ya hilo kuna mazingira
ambayo mtu anaweza kuwa si mwanandoa lakini ana maslahi katika
nyumba au kiwanja cha mtu fulani na anataka
kuzuia nyumba/ kiwanja hicho kisibadilishwe jina au kisiuzwe.
Kisheria jambo hilo linaruhusiwa na huitwa zuio( Caveat).
Hili sio zuio la kwenda mahakamani kama
mazuio tuliyoyazoea.Hili ni zuio
jingine kama nitakavyolieleza. Aidha kuzuia hati
isibadilishwe kimsingi ni sawa
na kuzuia nyumba isiuzwe. Hii ni kwakuwa hakuna namna ambavyo mnunuzi anaweza kununua kitu ambacho
hakiwezi kubadilika na kuingia
katika jina lake. Ikiwa
mke ana wasiwasi kuwa mume anaweza
kumzunguka na kuuza mali ya familia au mume ana wasi wasi juu ya uwezekano wa mke kuuza basi wanayo ruhusa
ya kuweka zuio ili hati ya nyumba
isibadilishwe. Yapo mambo mengi
kuhusu hili nitaeleza baadhi.
1. NINI MAANA
YA ZUIO.
Zuio
ni usitishwaji wa muda ambao huwekwa ili kuzuia mabadiliko yoyote katika hati.
Kama maana yenyewe inavyojieleza huu unakuwa ni usitishwaji wa muda ambao unalenga kulinda
maslahi ya mtu aliyeomba zuio.Kuitwa
zuio la muda haimaanishi kuwa
mtu akizuia itakuwa ni mwezi mmoja au
miwili basi, hapana. Ni zuio la
muda kwakuwa haliwezi kukaa milele lakini
mtu akishaliweka linaweza kukaa
hata miaka mingi kutegemea
na sababu za zuio hilo.
2. MWANANDOA KUZUIA HATI
ISIBADILISHWE.
Lazima ieleweke
wazi kuwa si kila mtu anaweza
kuamua na akazuia hati ya
mtu isibadilishwe . Wapo watu ambao kwa mujibu
wa sheria wanayo
haki ya kuomba
hati isibadilishwe. Kwanza mke au mume mmoja
kati yao anaweza kuweka kizuizi katika nyumba ya ndoa (matrimonial home) iwapo kuna dalili kuwa
mmiliki aliyeandikishwa anaweza kuiuza
au kuiweka rehani bila ya ridhaa ya mwingine. Mara nyingi migongano katika
familia inapoanza mmoja
kati ya wanandoa hukimbilia
kuuza baadhi ya
mali kwa aidha kumkomoa mwenzake au
sababu nyingine yoyote. Kwa
hiyo ili kuliepuka hilo unapogundua kuwa
kuna uwezekano huo
basi sheria imekuruhusu
mwanandoa kuweka zuio
ili hati isibadilishwe
na hivyo kuepuka kuuzwa kwa mali.
3. HATA MKOPESHAJI NAYE
ANAWEZA KUWEKA ZUIO
KWENYE HATI YAKO.
Nimezungumzia
zaidi
wanandoa kuzuia lakini
pia ieleweke wazi kuwa suala la
kuzuia si tu la wanandoa. Kampuni, shirika, mtu binafsi au taasisi ya
fedha iwapo imemkopa mtu
na akaweka nyumba/kiwanja kama
dhamana ambacho kina
hati basi wanayo ruhusa
ya kisheria ya
kuomba zuio liwekwe
kwenye hati ile ili dhamana
isije kutumiwa kukopea pesa
katika taasisi nyingine
au kuuzwa wakati ipo
kulinda deni. Kwa hiyo iwapo
mtu ana maslahi ya namna
hii kwenye ardhi inayomilikiwa
na mwingine basi ni haki
kwake kuweka zuio hili
ili kulinda maslahi yake.
4. WAPI UPELEKE MAOMBI YA KUZUIA HATI ISIBADILISHWE.
Mamlaka za ardhi
ni mamlaka ambazo hutakiwa
kupelekewa maombi haya
ya zuio. Mara nyingi
mamlaka za ardhi huwa zipo
katika ofisi za wilaya
au manispaa katika mkoa wako isipokuwa kwa walio
Dar es salaam maombi
hupelekwa makao makuu
pale wizara ya ardhi
kama ni hati.
5. MAOMBI YA KUZUIA HATI ISIBADILISHWE HUANDALIWAJE.
Maombi haya
si maombi kama maombi
mengine yalivyo. Maombi haya ni maombi ya kisheria na
huandaliwa katika ofisi
za wanasheria na hupelekwa
yakiwa na muhuri
wa mwanasheria. Karika
maombi hayo mwombaji
hueleza jina lake
kwa urefu, anuani yake, uhusiano
wake na yule ambaye
jina lake ndilo
liko kwenye hati yaani
anayemwekea zuio huku akieleza
sababu za msingi
kwanini anataka kuzuia
hati isibadilishwe.
6. LAZIMA
MAOMBI YAAMBATANE NA
NYARAKA HIZI.
Kwanza, picha 2 za
mwombaji huku kila picha moja ikibandikwa
kwenye nyaraka moja.
Pili, risiti za malipo ya
ada ya usajili. Maombi haya hulipiwa kiasi
cha fedha lakini si kikubwa sana
kwahiyo lazima uambatanishe na risiti
za malipo.
Tatu, mwombaji aambatanishe vielelezo vinavyompa haki juu ya
kiwanja husika kwa mfano cheti
cha ndoa, mkataba wa mkopo n.k.
Kwa leo ni hayo.
MWANDISHI
WA MAKALA HAYA
NI MWANASHERIA NA
MSHAURI WA SHERIA
KUPITIA GAZETI LA
SERIKALI LA HABARI
LEO KILA JUMANNE
, GAZETI JAMHURI KILA
JUMANNE NA GAZETI
NIPASHE KILA JUMATANO. PIA NI KATI YA WANASHERIA WAANZILISHI WA
BLOG HII. 0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
No comments:
Post a Comment