Na Miza Kona Maelezo-Zanzibar
Wananchi wametakiwa kuwa na mwamko
wa kuisoma sheria ili waweze kuijua na kupata haki zao pamoja na
kuepukana na vitendo mbali mbali vinavyokwenda kinyume na sheria.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi
mtendaji wa Kituo cha Huduma za Sheria Bi Harusi Miraji Mpatani wakati
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake
Migombani Zanzibar.
Amesema wananchi wamekuwa ni
wagumu wa kufuata sheria kutokana na uelewa mdogo waliokuwa nao wa
kutojua haki zao za msingi jambo linalopelekea kwenda kinyume na sheria
hizo pamoja na kuwepo kwa kesi nyingi zikiwemo za udhalilishaji na
ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Amesema kituo cha Huduma za Sheria
kipo kwa ajili ya kuwasaidia Wazanzibar kuweza kuelewa na kujua haki
zao pamoja na masuala ya sheria na haki za binadamu kwa kuwapatia elimu
sahihi na ufafanuzi wa sheria hizo.
Amefahamisha kuwa kituo pia
kinatoa msaada wa sheria na huduma kwa wananchi wasiojiweza wakiwemo
Walemavu, Masikini ,Wanawake na Watoto pamoja na kuwaelimisha wananchi
na kutatua migogoro.
“Elimu ya vitendo vya
udhalilishaji wa watoto inaendelea kutolewa lakini bado vitendo hivyo
vinazidi kuongezeka vijijini hivyo jamii iwe na mwamko wa kuwafichua na
kuwachukulia hatua wale wote wanaofanya vitendo hivyo”, ameeleza
Mkurugenzi huyo.
Akizungumzia kuhusu ucheleweshaji
wa kesi mahakani Mkurugenzi huyo amesema kuwa kuna kesi nyingi
mahakamani ambazo bado hazijatolewa hukumu kutokana na kukwama kwa kesi
hizo mahakamni hapo na nyengine kukosa ushahidi hivyo kituo kinafuatilia
tatizo hilo kwa wahusika na kulitafutia ufumbuzi.
Ameeleza kituo kina miradi miwili
inayosimamia haki za watoto katika Wilaya ya Kaskazini A na Wilaya ya
Maghariri Unguja chini ya ufadhili ya Umoja wa Ulaya (EU) pamoja na Save
The Children ambayo inapinga unyanyasaji wa watoto na kusimamia haki za
binadamu.
Bi Harusi amefahamisha kuongezeka
kwa watumiaji wa kituo hicho ni faraja kubwa ambayo inapelekea kupata
matumaini mazuri ya maendeleo ya utoaji wa huduma za kituo kwani katika
mwaka 2013 wateja waliofika kituoni hapo ni 3000 lakini kwa mwaka jana
zaidi ya wateja 4000 walifika kupata huduma katika kituo hicho.
Aidha Bi Harusi amewataka wananchi
kufuatilia Katiba iliyopendekezwa ili waweze kuielewa na kufanya
maamuzi sahihi wakati ukifika pamoja na kutumia kituo hicho cha sheria
kwani kinatoa huduma zake bure ili kuwasaidia wananchi kupata haki zao.
Kituo cha Huduma za Sheria
kinatarajia kuazimisha miaka 23 tangu kuanzishwa kwake na kauli mbiu ni
“Kutojua Sheria Sio Kukaa kimya”.
No comments:
Post a Comment