Tarehe 22 Desemba, 2014, Serikali ya Jamhuri ya Kenya ilitoa amri ya
kuzuia magari ya kitalii yenye usajili wa Tanzania kwenda kuchukua na
kushusha watalii wanaotumia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo
Kenyatta wakiwa njiani kuja kutembelea vivutio vya utalii katika Jamhuri
ya Muungano ya Tanzania.
Baada ya uamuzi huu wa Serikali ya Kenya, Waziri wa Maliasii na Utalii
Mhe. Lazaro Nyalandu alifanya majadiliano na Waziri wa masuala ya utalii
wa Serikali ya Kenya siku ya tarehe 16, Januari, 2015 ili kutafuta
ufumbuzi wa kadhia hii. Matokeo ya mkutano wa Mawaziri hawa yalikuwa ni
kusitishwa kwa muda katazo lililotolewa na Serikali ya Kenya kwa
makubaliano kuwa yafanyike mazungumzo baina ya pande hizi mbili ndani ya
kipindi cha wiki tatu kuanzia tarehe 16 Januari, 2015 ili kurekebisha
Mkataba wa Ushirikiano katika sekta ya utalii wa mwaka 1985 kati ya nchi
zetu mbili.
Kufuatia
makubaliano hayo Wizara ya Maliasili na Utalii iliiomba Wizara ya
Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki iandae kikao hicho cha pamoja katika
muda uliopangwa. Kwa kuzingatia historia na uzito wa suala lenyewe,
Wizara ya Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki iliona umuhimu wa kuhusisha
Wizara zingine husika za Uchukuzi, Mambo ya Nje, Viwanda na Biashara,
Fedha, Ulinzi, Mambo ya Ndani, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira na Viongozi wa Sekta Binafsi ili kupata msimamo
wa nchi wa pamoja kabla ya mkutano na Kenya.
Hivyo,
vikao vya wataalam vimefanyika Dar es Salaam na Arusha hadi wiki ya
kwanza ya mwezi huu wa pili kwa maandalizi ya kikao cha mwisho cha
Mawaziri upande wa Tanzania kabla ya kukutana na wenzetu wa Kenya.
Pamoja na kushauriana na Waziri mhusika wa Kenya (Masuala ya Afrika
Mashariki, Biashara na Utalii, Bi. Phyllis Kandie) kusogeza mbele tarehe
ya mkutano wa pamoja ili kuruhusu muda wa kutosha kwa majadiliano ya
ndani na wadau, Bi. Kandie alimwandikia Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika
ya Mashariki, Dkt. Richard Sezibera na kumnakili Waziri Nyalandu,
kurejesha amri yake ya awali ambayo alisema inaendana na Sheria ya
utalii na kanuni za uchukuzi za Kenya.
Serikali
ya Tanzania kimsingi imesikitishwa na uamuzi huo wa Serikali ya Kenya
kwani haujengi wala hauendani na dhamira njema ya Mkataba wa Kuanzisha
Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kuenzi njia ya mazungumzo, maelewano na
maridhiano katika kufikia maamuzi. Suala la kurekebisha mkataba
ulioingiwa na nchi hizi mbili kwa hiari miaka 30 iliyopita, si jepesi la
kujadiliwa na Mawaziri wawili tu na kuwekeana ukomo wa muda katika
kulipitia. Serikali ya Tanzania itaendelea na mchakato iliouanzisha wa
kuhusisha wadau wote na kufikia uamuzi ambao itauwasilisha kwa Serikali
ya Kenya kupitia vikao rasmi vya Jumuiya.
Pamoja
na kwamba amri hii ya Serikali ya Kenya inaenda nje ya mkataba wa 1985
kwa kuvihusisha hata viwanja vya ndege kuwa sehemu ya vivutio vya
utalii, Serikali ya Tanzania itaheshimu na kuzingatia amri hiyo ili
kulinda undugu na urafiki uliopo kati ya nchi zetu huku tukitafakari
hatua za kuchukua ili kuondoa bughudha kubwa itakayotokea kwa watalii na
wasafiri wetu wanaopitia uwanja huo wa Jomo Kenyatta. Aidha Tanzania
itachukua hatua ya kuwafahamisha watalii na wageni wote wenye nia ya
kutembelea vivutio vya kitalii vya Tanzania kutumia viwanja vingine vya
ndege ili kuepuka kadhia na gharama zisizo za lazima.
Kwa
upande wa Tanzania, viwanja vya ndege hasa vile vya Kimataifa
vitaendelea kuwa sehemu ya malango ya kuingilia na kutokea kwenda kokote
iwe ndani ya Jumuiya au nje ya Jumuiya na havitavichukuliwa kama
vivutio vya utalii. Tanzania haitazuia magari ya Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki au nchi nyingine yoyote kuingia katika
viwanja vyake vya ndege kuleta au kuchukua watalii wanaopitia katika
viwanja hivyo na kwenda katika nchi zao.
Mkataba
wa mwaka 1985 kati ya Tanzania na Kenya ulilenga kutoa mwongozo wa
ushirikiano katika Sekta ya Utalii kati ya nchi zetu mbili. Aidha,
makubaliano hayo yalielekeza maeneo muafaka kwa ajili ya kubadilishana
watalii huku ikizingatiwa kuondoa bugudha kwa watalii. Maeneo hayo ni
pamoja na miji ya mipakani pamoja na miji rasmi iliyopendekezwa na
kukubalika na pande zote mbili ikiwemo Nairobi ambako kiwanja cha ndege
cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta kipo.
Mwisho,
Tanzania itaendelea kuenzi undugu na urafiki uliojengeka kwa zaidi ya
miaka 50 tokea uhuru kati ya nchi zetu mbili na suala dogo kama hili
halitaweza kuteteresha uhusiano wetu mzuri.
WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
10 FEBRUARI, 2015.
No comments:
Post a Comment