Balozi wa
Tanzania nchini Oman Ali Ahmed Saleh kushoto Aliyekaa kwenye kiti akipata
burudani ya Msewe iliyoandaliwa kwa ajili yake na Kikundi cha Sanaa cha Zanzibar
mara baada ya Balozi huyo kumaliza ziara yake ya kuwatembelea Watanzania na
kushauriana nao mambo mbalimbali ya kukuza soko katika Maonesho ya Kimataifa ya
Sanaa Ubunifu na Utamaduni yanayoendelea Mjini Mascut nchini humo. Picha na
Faki Mjaka.
Wasanii wa Kikundi
cha Sanaa cha Zanzibar wakicheza Ngoma aina ya Uringe kwa Balozi wa Tanzania
nchini Oman (hayupo pichani) mara baada ya Balozi huyo kuwatembelea Watanzania na
kushauriana nao mambo mbalimbali ya kukuza soko katika Maonesho ya Kimataifa ya
Sanaa Ubunifu na Utamaduni yanayoendelea Mjini Mascut nchini humo.
Mjasiriamali
wa Mavazi mbalimbali ikiwemo ya Kimasai Bi Anna Matinde akitoa ufafanuzi wa
bidhaa zake kwa Balozi wa Tanzania Nchini Oman Bw. Ali Ahmed Saleh kulia.Balozi
Saleh alifanya ziara ya kuwatembelea Watanzania hao na kushauriana mambo
mbalimbali ya kukuza soko katika Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa Ubunifu na
Utamaduni yanayoendelea Mjini Mascut nchini humo. Picha na Faki Mjaka-Mascut
Oman.
Na Faki Mjaka, Muscat, Oman
Serikali na Wadau binafsi wameshauriwa kuwasaidia
Wajasiriamali wa Kitanzania ili waweze kuziweka bidhaa zao katika Vifungashio (Package)
vyenye mvuto na kiwango cha ubora wa kimataifa.
Kufanya hivyo kutawawezesha Wajasiriamali hao kupata soko la
Bidhaa zao kwa Wateja wadogo na wakubwa katika nchi mbalimbali duniani.
Ushauri huo umetolewa na Balozi wa Tanzania nchini Oman Bw.
Ali Ahmed Saleh alipowatembelea Wajasiriamali wanaoshiriki katika Maeonesho ya
Kimataifa ya Sanaa,Ubunifu na Utamaduni yanayoendelea katika Mji wa Muscat
nchini Oman.
Amesema licha ya Tanzania kufanya vyema katika Maonesho hayo
kuna baadhi ya changamoto ambazo zinahitaji kupatiwa ufumbuzi ili Tanzania
izidi kupata sifa ya bidhaa zake kimataifa.
Changamoto hizo ni pamoja na uwezo mdogo wa kuziweka bidhaa
wanazozitengeneza katika Vifungashio (Package) ambavyo ubora wake haujafikia
kiwango kinachotakiwa cha kimataifa.
Balozi Saleh amefahamisha kuwa mbali na bidhaa hizo ikiwemo
zile za Viungo kupata Soko kutoka kwa Wakaazi wa Oman lakini inakuwa ngumu
kupata Soko kwa Wateja wa Maduka Makubwa (Supermarkets) ambao wangenunua bidhaa
hizo kwa ujumla.
Ameongeza kuwa Wateja wa Maduka Makubwa wanahitaji bidhaa
zilizowekwa katika Package ambazo zinaonesha kuwa zimepitia katika maabara ya
kisayansi na kupata vigezo vyote vinavyohitajika kimatumizi.
“Naamini tukiwa na Package zenye ubora wa kimataifa
zinazoonesha Warrant, muda wa matumizi basi hata Order za Wateja wa
Supermarkets tungepata za kutosha ” Alisema Balozi Saleh
Aidha Balozi Saleh amewashauri Wajasiriamali hao kuziweka
bidhaa zao katika Vifungashio (Package) hata zile ambazo bado hawajafikiria
kuziweka ikiwemo zile za Vinyago na Viatu ili kuvutia zaidi Wateja.
“Tumezoea kwetu kuwa Vinyago haviwekwi kwenye Package ila
navyo vinatakiwa viwekwe pamoja na vitu vingine ili wateja wahamasike na Ubora
wa Bidhaa zetu” Alishauri Balozi Saleh
Hata hivyo Balozi Saleh ameishukuru Serikali ya Oman kwa
mashirikiao yake makubwa na Tanzania na kwamba fursa hiyo iliyopatikana itakuwa
na Matunda mazuri kwa Tanzania kutokana na kujitangaza vyema kwa Wageni na
Wenyeji wa Oman.
Kwa
upande wao Wajasiriamali hao Walimshukuru Balozi Saleh na Ofisi yake
kwa kuwa karibu nao na kushauriana nao kila muda jambo ambalo linawapa
faraja kubwa.
No comments:
Post a Comment