Na
Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar.
Serikali
haitoridhia kuwabakisha Wapangaji na Wafanyabiashara katika jengo la Treni ili kuepusha
maafa na kuokoa maisha ya Wananchi na mali zao.
Hayo
yameelezwa na Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar Mhe. Ramadhan
Abdulla Shaaban wakati wa mkutano wa mzungumzo ya pamoja kati ya Wapangaji na Wafanyabiashara wanaolitumia jengo hilo na Serikali
uliofanyika katika ofisi ya Mamlaka ya Mji Mkongwe iliopo Forodhani Mjini Zanzibar.
Waziri
huyo amesema kuhamishwa kwa Wakaazi na Wafanyabiashara katika jingo hilo sio
jambo la mjadala kama wanavyotaka wao bali ni wajibu wao kufuata maagizo ya
serikali ili kuepukana na vifo visivyo vya lazima na hasara za mali zao pindi jengo
hilo litakapo poromoka na kupelekea kuitupia lawama serikali pale majanga
yatakapotokezea. “Hili
si jambo la majadiliano kama mnavyotaka nyinyi”, alieleza Waziri Ramadhan.
Ametanabahisha
kuwa serikali imeshachukua hatua mbalimbali za kulijenga tena jengo hilo ikiwemo
kutafuta mafundi, wahandisi pamoja na vifaa vya ujenzi na inategemewa hivi
karibuni kuanza rasmi kwa ujenzi huo.
Aidha
waziri ramadhan amewataka Wapangaji na Wafanyabiashara hao kutokaidi agizo la Serikali
kwa usalama wa mali na maisha yao kwani jengo hilo linaonekana halitoweza
kuhimili mvua za Masika zinazotarajiwa kuanza mwezi machi mwaka huu na badala
yake linaweza kuporomoka kutokana na mvua hizo.
Jengo
la Treni liliopo Darajani Mjini Zanzibar lina wakaazi 57 wakiwemo Wapangajia na
Wafanyabiashara ambapo kwa sasa hali yake hairizishi baada ya kupasukapasuka na
kutishia usalama wa maisha ya watu wanaoishi humo pamoja na wapita njia.
IMETOLEWA
NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment