Magdallena Alphonce Shija A K A Dorcas, akiwa kwenye Utunzi wa baadhi ya nyimbo zake. |
Magdallena Alphonce Shija A K A Dorcas, alizaliwa tarehe 5/7/1990, katika familia ya Mzee Alphonce Shija, yenye watoto 11 na yeye akiwa ni mtoto wa tisa (9) kuzaliwa kwa upande wa baba yake lakini pia kwa upande mwingine wa mama yake ni mtoto wa nne (4) kuzaliwa kutokana na kwamba wazazi wake walitengana baada ya yeye kuzaliwa wakati huo Magdallena akiwa ni mtoto mdogo mwenye umri wa Miaka 2.
Historia ya maisha yake inasikitisha kidogo lakini huo ndio ukweli halisi kwani Baada ya maisha ya utengano wa wazazi hao, Magdallena hakuweza tena tena kuishi maisha ya utulivu, hivyo mwanzo aliweza kuishi kwa Mama ambapo ilikuwa ni mwaka 93 kabla ya kuchukuliwa na baba yake aliyeishi naye hadi alipoanza elimu yake ya Msingi kwenye shule ya Nyambubi Wilaya ya Bukombe iliyoko katika Mkoa wa Shinyanga tangu mwaka 2000-2007,
na Elimu ya Sekondari alimalizia katika shule ya Busisi Tangu 2008-2012
huko Sengerema.
Akielezea Maisha hayo Magdallena anasema kuwa" Kwa kweli nimeishi katika maisha ya kulelewa na wazazi wote wawili lakini kila mmoja alikuwa akiishi kivyake baada ya kutengana nikiwa mdogo, ambapo niliweza wakati mwingine kuwa kwa mama na wakati mwingine kuwa kwa baba, sikuwa na njia ingine ya kuishi zaidi ya kuwafuata wazazi wangu nilipokuwa mdogo, lakini mara baada ya kumaliza elimu ya Msingi nilikwenda kuishi kwa mjomba wangu aliyekuwa akiishi Ushirombo Bukombe lakini wakati huo nilikuwa ndiyo kwanza nimeanza elimu ya sekondari ambayo pia nilisoma kwa kuhama hama ambapo wakati fulani pia nikiwa kidato cha tatu nilishindwa kuendelea na masomo kwa kuwa kwenye familia kulitokea matatizo yaliyoniweka kwa muda nje ya masomo kwa kipindi kisichopungua miezi 6 kabla ya mama yangu kuniita tena na kisha kunitafutia shule ya Busisi niliyofanikiwa kumalizia kidato cha nne" anasimulia Magdallena Alphonce.
Safari yake kimziki ilianza wakati akiwa shule ya msingi, ambapo alivutiwa sana na baadhi ya wanamuziki wa Injili, lakini pia anasema kuwa kwa sasa anaishi na Mtoto wa Mjomba(Binamu) ikiwa ni baada ya kuamua kujiingiza kwenye soko la Muziki baada ya kumaliza Elimu yake ya Sekondari.
hajabahatika kupata elimu ya chuo kutokana na kwamba uwezo wake wa kumudu kulipa gharama ni mdogo, lakini hata hivyo anasema kwamba yupo tayari kusoma endapo atapata mfadhili wa kuweza kumwendeleza kielimu kuanzia hapa alipoishia, "lengo langu kubwa ni kujiendeleza kielimu zaidi lakini uwezo ndiyo sina na kama nilivyosema hapo mwanzo, kwamba wazazi wangu kitendo cha kutoishi pamoja ni tatizo kubwa sana kwangu, kwa maana sina tena mwelekeo wa faida ya wazazi, nikipata mtu wa kunisaidia kusoma niko tayari kusoma, lakini kwa wakati huu ambao bado sina mwelekeo nimeamua kumtumikia Mungu kwa kuimba nyimbo zinazomtukuza yeye lakini pia zinazotoa elimu kwa watu wengine, kubwa hapa mimi namuomba Mungu aweze kuniwezesha kufikia malengo yangu kimziki na ndiyo maana nimeamua kujikita zaidi kwenye masuala ya miziki hii ya Dini(Injili" anasimulia Magdallena.
Magdallena Alphonce Shija ni Mwimbaji Chipukizi wa Muziki wa Injili Tanzania, Mwenye nia na lengo la kutaka kuwa Mwanamuziki mkubwa atakayeweza kuwabadilisha watanzania kupitia Muziki wake katika Mambo mbali mbali.
Akizungumza na Vyombo vya habari Magdallena Shija, alisema kuwa kitu kilichomvutia hadi kuamua kuingia kwenye soko la muziki wa injili ni pamoja na kushawishika kutoka kwa wanamuziki mbali mbali waliopo kwenye fani hiyo wakiwemo kina Rose Mhando, Bahati Bukuku, Boni Mwaitege, Christina Shusho na wengine wengi.
hata hivyo anawataja ndugu waliozaliwa pamoja kuwa ni Mathias, Edward, Marry, Leah, Willium, Agnes, Estar na Sephania Alphone ambao ni ndugu wa kuzaliwa kwa baba lakini pia anawataja walioweza kuzaliwa kwa mama kuwa ni pamoja na Angle, Felistar, Recho, na Joyce.
Kuhusu maisha ya Ndoa Magdallena anasema kuwa bado kwa sasa hana huo mpango kutokana na kwamba Mungu ndiye anayepanga kwenye kila njia zake, hivyo endapo akitokea anayeongozwa na mungu kwa ajili yake basi wakati wowote anaweza kumtambulisha na kuwaeleza wazazi wake kuhusu Mtu huyo" kwa sasa sina mpenzi wala mume kutokana na kwamba nipo kwenye hali ngumu na siwezi kuwaza hilo kwa sasa kwani najitaidi sana kumuomba Mungu ili yeye ndiye aweze kuniletea mume mwema na mwenye mapendo ya dhati, akipatikana baada ya mimi pia kumchunguza, basi bila shaka nitampeleka kwa wazazi wangu ili kumtambulisha" anasema
kwa sasa Magdallena yupo kwenye mafunzo ya Muziki, kwenye shule inayotoa mafunzo hayo jijini Dar es salaam, kwa ajili ya kupanua wigo wa utambuzi wa kutumia vifaa vya muziki na baadhi ya miziki iliyopo kwenye mikakati yake ni pamoja na Bwana Yesu anaweza, Baba saidia Taifa, Aman, Lakini ufahamu neno hili, Yesu katika kisima cha Yakobo, Rafiki wa Kweli, Siku za Mwisho, na Wimbo mmoja utakaoibwa kwa lugha ya Kisukuma(SebhaMulungu).
Magdallena anawashauri vijana wengine kuishi kwa kumtegemea mungu zaidi kuliko kumtegemea mwanadamu na kwamba kila jambo tunatakiwa kufanya kwa ajili ya Mungu, na zaidi ya hayo amewataka vijana wengi kuhakikisha wanatumia muda wao katika kumtumikia Mungu.
kwa yeyote atakayeguswa na mwenye nia ya kutaka kumsaidia Magdallena anaweza kuwasiliana kupitia namba ya Meneja wake +255-767-869133.
No comments:
Post a Comment