TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Tuesday, February 17, 2015

MAKALA YA SHERIA:USINUNUE KIWANJA/NYUMBA YA MIRATHI BILA KUPATA FOMU HII.

12
Kusoma makala zaidi ingia hapa:sheriayakub. blogspot. com

Na Bashir Yakub
Nimeandika makala nyingi kuhusu namna ya kisheria ya kuepuka kununua nyumba/viwanja vyenye migogoro kwakuwa migogoro ya vitu hivi inaumiza sana. Waliokutana na migogoro hii wanajua vyema ninaongea nini. Katika mwendelezo wa kumuepusha mnunuzi na janga hili, leo tena tuangalie taratibu za ununuzi wa nyumba/kiwanja cha mirathi. Nataka ieleweke vyema kuwa taratibu za manunuzi ya nyumba/kiwanja zinatofautiana. Tofauti kubwa ni za kisheria hasa namna ya uandishi wa mkataba na nyaraka ambazo zitaambatana na mkataba huo. Eneo hili nalo naliongelea kwakuwa ni eneo ambalo kwa upande wake nalo limewaingiza wanunuzi wengi wa nyumba/viwanja katika migogoro ambayo ingeweza kuepukwa mapema iwapo taarifa kama hizi pengine mnunuzi angezipata mapema. Kisheria si kweli kuwa kila aina ya mkataba unaweza kut umika kununua kila aina ya nyumba. Mkataba huandaliwa kutegemea na mazingira ya kitu chenyewe. Nyumba/kiwanja ambacho wauzaji wake ni wasimamizi wa mirathi ni tofauti na nyumba/kiwanja ambacho muuzaji si msimamizi mirathi. Tatizo kubwa ambalo limewasumbua wengi mahakamani ni kununua nyumba/kiwanja cha mirathi kwa kutumia utaratibu uleule wa kununulia kiwanja/nyumba ya kawaida ambayo muuzaji wake ni mmiliki halisi yaani si msimamizi wa mirathi.
( 1 ) UTAJUAJE KAMA NYUMBA/KIWANJA UNACHONUNUA NI CHA MIRATHI.
Niliwahi kuandika katika makala zilizopita wakati nikieleza namna ya kitaalam ya kujua kama eneo unalonunua kama lina mgogoro au hapana kuwa katika ununuzi ardhi, nyumba/viwanja vimegawanyika sehemu kuu tatu. Kwanza kuna vyenye hati, Pili kuna vyenye leseni za makazi na tatu ni vile vyenye mikataba ya kununulia. Hivi ni vile ambavyo havina hati wala leseni za makazi. Sasa ili ujue kuwa nyumba/kiwanja unachouziwa ni cha mirathi au hapana , hatua ya kwanza ni kuwauliza wauzaji au muuzaji kama eneo ni lake au ni msimamizi wa mirathi. Kama atasema yeye ni msimamizi wa mirathi basi hapatakuwa na shida mnunuzi utaendelea na utaratibu nitakaoeleza katika makala haya. Lakini akisema hapana si msimamizi wa mirathi basi utakachokifanya ili kujua ukweli wake ni kuomba nyaraka ya eneo husika zile nilizotaja hapa juu ili uone taarifa za mmiliki. Ukikagua na kugundua kuwa hakuna jina lake basi atatakiwa kutoa maelezo kwanini yeye ni muuzaji na anachouza hakina jina lake.Hii ni rahisi wala haina ufundi sana isipokuwa tu ni katika hatua za mwanzo za kuonesha umakini. Kama nyaraka atakayokuonesha itakuwa haina jina lake na yeye anataka kuuza kama msimamizi wa mirathi basi hakikisha ana nyaraka hii hapa chini.


( 2 ) MUUZA KIWANJA/NYUMBA YA MIRATHI LAZIMA AMPATIE MNUNUZI FOMU HII KISHERIA.
Fomu na 4 ni fomu maalum anayotakiwa kuwa nayo muuzaji wa nyumba/kiwanja cha mirathi kisheria. Kuwa na fomu hii ni lazima kisheria na nitoe angalizo kuwa mnunuzi kamwe asikubali kununua kiwanja/nyumba ya mirathi bila fomu hii. Mnunuzi wa nymba ya mirathi anaponunua bila muuzaji kuwa amempatia fomu hii kisheria ni sawa na hajanunua bila ya kujali gharama alizotoa. Fomu hii ndiyo inayompatia mamlaka muuzaji mali ya mirathi kuuza kwakuwa mali ile inakuwa si yake kwa uhalisi.
( 3 ) FOMU HII HUTOLEWA WAPI.
Fomu hii hutolewa na mahakama za Tanzania. Fomu hii hutolewa baada ya kuwa limefunguliwa shauri la usimamizi wa mirathi ambapo huteuliwa msimamizi wa mirathi ambaye sasa ndiye hustahili kuuza nyumba/kiwanja ikiwemo mali nyingine pia. Aidha mahakama za mwanzo huhusika na kutoa fomu hizi kwa wingi zaidi lakini pia mahakama za wilaya, mahakama za hakimu mkazi na mahakama kuu nazo huwa na mamlaka ya kutoa fomu hizi kutegemeana na matakwa ya kisheria. Suala la msingi kwa mnunuzi wa nyumba anayekagua fomu hii ni kuwa ahakikishe fomu hii imetolewa na mahakama kati ya mahakama nilizotaja.
( 4 ) MNUNUZI WA NYUMBA/KIWANJA KUTHIBITISHA UHALALALI NA UKWELI WA FOMU.
Kutokana kuwapo utapeli na ghushi nyingi hasa katika manunuzi ya viwanja na majumba unaotokana na hamu kubwa ya wauzaji matapeli kutaka kukamata hela nyingi za haraka zitokanazo na mali hizi basi zimekuwapo kesi nyingi ambapo fomu hizi za usimamizi wa mirathi zimeghushiwa na wanunuzi kulazimika kuingia hasara. Kughushi nyaraka hizi ni rahisi mno kwa kuwa kinachotakiwa ni kidogo tu ni sahihi na muhuri wa mahakama vitu ambavyo hutengenezwa halafu mtu anauza nyumba. Kuepukana na hili njia ya uhakika zaidi ni kuomba upate nakala ya fomu hiyo kutoka kwa muuzaji halafu kwenda nayo mpaka mahakama husika ambayo imeandikwa kwenye fomu hiyo na kuomba kuthibitishiwa kama ni kweli mahakama hiyo ilitoa hiyo fomu. Majibu utapata ya uhakika na yenye usalama kwako.
( 5 ) TAARIFA GANI MNUNUZI WA NYUMBA ATEGEMEE KUZIKUTA KWENYE FOMU.
Kwanza kwa juu lazima iwe na picha ya muuzaji(Msimamizi mirathi). Pili itakuwa na jina la mahakama iliyotoa fomu hiyo namba ya usimamizi wa mirathi, tarehe ilipotolewa, jina la msimamizi mirathi ambaye ndiye muuzaji, jina la marehemu ambaye ndiye alikuwa mmiliki mali halisi na tarehe ya kifo chake. Kwa chini mwisho itakuwa na kiapo cha muuzaji sahihi ya hakimu au jaji aliyeiidhinisha, tarehe ilipotolewa , muhuri wa mahakama pamoja na sahihi ya msimamizi mirathi ambaye ni muuzji katika makala haya.Mnunuzi jihadhari , utapeli katika manunuzi ya nyumba na viwanja kwasasa ni janga la kitaifa.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com

No comments:

Post a Comment