\Meneja
Miradi kutoka Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) Mhandisi Khalid James
(kulia) akiieleza Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini hatua
iliyofikiwa ya ujenzi wa miundombinu ya umeme katika mikoa ya
Iringa, Dodoma, Singida hadi Shinyanga inayosimamiwa na Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili. Kamati ya Bunge inafanya ziara
katika mikoa ya Dodoma, Singida, Arusha na Kilimanjaro kwa ajili ya
kukagua miradi ya umeme ili kujionea maendeleo yake pamoja na
kuzungumza na wananchi
Meneja
Miradi kutoka Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) Mhandisi Khalid James
(katikati) akitoa maelezo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati
na Madini kuhusu maendeleo ya ujenzi wa njia kuu za umeme unaofanywa na
kampuni ya Jyoti Structures Limited kutoka India katika eneo la Nara
mkoani Dodoma
………………………………………………………………………….
Na Greyson Mwase, Bahi – Dodoma
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini , Richard Ndassa amewaambia wakazi wa kata ya
Ibihwa iliyopo Bahi mkoani Dodoma kuwa gharama za kuuunganishiwa huduma
ya umeme zimeshuka hadi shilingi 177,000 na iwapo ikatokea wakatozwa
zaidi ya kiwango hicho, na watumishi wasio waaminifu basi wana haki ya
kumfikisha mbele ya vyombo vya kisheria.
Ndassa alisema hayo wakati Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipotembelea wilaya ya Bahi kwa
ajili ya kukagua miradi ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi.
Ndassa alisema kuwa Serikali
imekuwa ikijitahidi kupunguza gharama za kuunganishiwa umeme hasa maeneo
ya vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kuhakikisha
kila mwananchi anapata nishati muhimu na kujiletea maendeleo.
Alisema kuwa kama juhudi ya
Serikali katika kuhakikisha kila mwananchi anaondokana na umasikini,
Serikali kupitia REA iliamua kupunguza gharama za kuunganishiwa umeme
kwa wananchi wanaoishi vijijini ili waweze kupiga hatua kimaendeleo, na
kuwataka kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiandaa na uwekezaji wa viwanda
vidogo vidogo.
Alifafanua kuwa iwapo watatokea
watumishi wasio waaminifu na kutaka kuwatoza fedha zaidi ya kiasi
kinachotakiwa kulipwa, basi wana wajibu wa kuwafikisha katika vyomvbo
vya sheria.
“ Iwapo atatokea mtumishi na
kuwatoza gharama zaidi ya ile inayohitajika kulipwa kisheria, basi mna
haki ya kumfikisha polisi ili afunguliwe mashtaka,” alisema Ndassa
Aliendelea kusema kuwa umefika
wakati wa watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza mara
baada ya kukamilika kwa miradi ya umeme kwani umeme ndio kitovu cha
ukuaji wa uchumi katika nchi yoyote.
“ Kuna vijiji ambayo vimeshaanza
kunufaika na huduma ya umeme, nawasihi muanzishe viwanda vidogo vidogo
vya kukoboa nafaka, kukamua mafuta ya alizeti ili kujiongezea kipato”,
alisema Ndassa.
Wakati huo huo akizungumza kwa
niaba ya wakazi wa kata hiyo , Mtendaji wa Kata, Jenipha William alisema
kuwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme ya REA Awamu ya Pili
pamekuwepo na changamoto ya vijiji vingine kurukwa hali inayopelekea
wananchi wachache kupata umeme.
Alisema kuwa hali hiyo inapelekea baadhi ya vijiji kupiga hatua kubwa kimaendeleo huku vijiji vingine vikibaki gizani
Akifafanua jinsi Shirika la Umeme
Nchini (Tanesco) lilivyojipanga kukabiliana na changamoto hiyo mbele ya
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Meneja wa Tanesco
Dodoma, Zakayo Temu alisema kuwa kazi ya kujenga miudombinu ya umeme
chini ya REA Awamu ya Pili imekuwa ikifanywa kwa awamu kulingana na
fedha na uwiano na mikoa mingine.
Temu alisema ili kukabiliana na
changamoto hiyo, shirika limetenga bajeti ya mwaka ujao wa fedha kwa
ajili ya vijiji vilivyokosa umeme.
No comments:
Post a Comment