Mwenyekiti
wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama (kulia)
akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusiana
na maandalizi ya tamasha hilo litakalofanyika Aprili 5. (Picha na
Francis Dande)
Na Mwandishi Wetu
MWIMBAJI wa nyimbo za injili kutoka Zambia, Ephraem Sekereti yu miongoni mwa nyota wa kimataifa watakaopamba Tamasha la Kimataifa la Pasaka litakaloanzia Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam hapo April 5, kabla ya kuhamia mikoani.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo linalofanyika chini ya uratibu wa kampnuni ya Msama Promotions, Alex Msama, Sekereti anakuwa mwimbaji wa kwanza wa kimataifa kuthibitisha ushiriki.
Alisema mbali ya Sekereti ambaye mara kadhaa aliwahi kushiriki tamasha hilo na kuwa baraka kwa wapendwa na wadau wa Tamasha hilo, tayari ameanza maandalizi ya nguvu ili kuwa fiti katika tamasha hilo ambalo litabeba pia maadhimisho ya miaka 15.
“Kwa upande wa waimbaji wa kimataifa, safari hii watakuwa wengi zaidi kutokana na ukubwa wa tukio lenyewe. Lakini hadi sasa Sekereti ndie wa kwanza kuthibitisha, wengine mazungumzo yanaendelea,” alisema Msama.
Kwa upande wa waimbaji wazawa, Msama alisema nao wameongezeka na kufikia wawili kwani mbali ya Upendo Nkone aliyethibitishwa wiki iliyopita, mwingine ni Jesca Honoli na kusema wengine watazidi kujulikana kwa siku za usoni.
Katika hatua nyingine, Msama alisema kwa vile ni tamasha linalokwenda na maadhimiosho ya miaka 15 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, makundi maalumu katika jamii kama walemavu, yatima na wajane watashiriki katika kufurahia tukio ambalo ni faraja kwao.
“Tamasha la Pasaka limekuwa pia baraka kwa makundi maalumu katika jamii kama walemavu, yatima na wajane, katika kuadhimisha miaka 15, makundi hayo yatakuwa na wawakilishi ili kuleta maana kamili ya nafasi yao katika tukio hilo la kimataifa,” alisema.
Kuhusu mikoa ambayo itafikiwa na tamasha la mwaka huu, Msama alisema suala hilo bado linafanyiwa kazi na kamati yake kutokana na wingi wa maombio yaliyowafikia hadi sasa kwani ni mingi kuliko walivyotarajia kiasi cha kuipa kamati yake kazi ya ziada.
No comments:
Post a Comment