Kaimu
Kamishna Msaidizi wa Madini, Sehemu ya Uchumi na Biashara ya Madini,
Aloyce Tesha (Kulia) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Nishati na
Madini (Madini), Charles Kitwanga (Kushoto) kuhusu utendaji kazi katika
sekta hiyo. Naibu Waziri Kitwanga aliwatembelea Watumishi wa Idara ya
Madini kuzungumza nao na kukagua utendaji kazi wao.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini (Madini), Charles Kitwanga (wa kwanza
Kulia), akifafanua jambo kwa Viongozi wa Idara ya Madini alipokutana nao
kujadili utendaji kazi katika sekta hiyo. Naibu Waziri Kitwanga
aliwatembelea Watumishi wa Idara ya Madini kuzungumza nao na kukagua
utendaji kazi wao.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Madini), Charles Kitwanga (Katikati)
akizungumza na baadhi ya Wafanyakazi wa Idara ya Madini alipowatembelea
kujionea utendaji kazi katika Idara hiyo.
……………………………………………………………………………
Veronica Simba na Rhoda James
Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Madini), Charles Kitwanga
amewataka Maofisa wa Serikali katika sekta ya madini nchini kutumia
kanuni zinazoongoza sekta hiyo kuwabana wachimbaji wadogo wa madini
wanaokwepa kulipa kodi mbalimbali zilizowekwa na Serikali.
Kitwanga ametaka kanuni husika zitumike kuwachukulia hatua kali
wakwepa kodi hao ikiwa ni pamoja na kuwanyang’anya leseni za uchimbaji
madini wanazomiliki.
Aliyasema hayo hivi karibuni alipokutana na Viongozi wa Idara ya
Madini katika Wizara husika hivi karibuni jijini Dar es Salaam kwa
lengo la kuzungumza nao na kujionea utendaji kazi wao.
Akizungumza na Viongozi hao, Kitwanga alisema wachimbaji wadogo
wa madini, kama walivyo wafanyabiashara wengine nchini, wanawajibika
kulipa kodi zote zilizowekwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kodi ya
huduma, mrahaba na nyingine ili kuiwezesha Serikali kupata mapato
stahiki kwa lengo la kuwaletea wananchi wake maendeleo.
“Inabidi tujenge nidhamu katika kazi, vinginevyo hatutafika
kwenye uchumi wa kati tunaoutarajia ifikapo mwaka 2025. Kama mtu anakaa
na leseni bila kulipa, tutumie kanuni kumnyang’anya. Kwa mfano, mtu
asipolipa TRA kwa biashara yake, watamwacha kweli?” alisisitiza Naibu
Waziri.
Akifafanua zaidi, Kitwanga alisema ili kupata matokeo chanya
katika kazi yoyote, inabidi kutenda yale yaliyo sahihi na siyo kutenda
mambo kwa usahihi, akitumia msemo maarufu wa lugha ya kiingereza ‘Do the
right thing, don’t do things right.’
“Inapotokea kuna sheria imepitwa na wakati, si sahihi kuendelea
kuifuata tu bila kutafuta namna ya kuirekebisha kwa manufaa ya
wananchi,” alisisitiza Kitwanga na kuongeza kuwa ni lazima kutumia
kanuni mbalimbali zilizopo kubadilisha mambo inapobidi na kutenda mambo
sawa sawa kwa manufaa ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kitwanga aliwataka Watendaji
katika Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuwasaidia wachimbaji
wadogo wa madini ili watoke katika uchimbaji mdogo na kuwa wachimbaji wa
kati na kuendelea, hivyo kukuza kipato chao na uchumi wa nchi kwa
ujumla.
“Ni lazima ifike mahala madini yetu yachimbwe na Watanzania
wenyewe hali itakayosaidia mzunguko wa fedha nchini kuwa mkubwa zaidi,”
alisema.
Aidha, Naibu Waziri Kitwanga aliwataka Stamico watakapokuwa
wanachimba madini, wahakikishe faida yote inarudi nchini ili kukuza
mzunguko wa fedha na hivyo kuinua uchumi wa nchi. “Hata wenzetu
wanapeleka fedha zote za faida kwao. Wanazobakiza hapa, ni zile tu
wanazohitaji kuendeshea biashara,” alitoa mfano.
Akizungumza na Wafanyakazi wa Wakala wa Ukaguzi Madini Tanzania
(TMAA), Naibu Waziri Kitwanga aliwataka kufanya kazi kwa juhudi ili
kuhakikisha mapato ya Serikali yanakusanywa kikamilifu.
“Leteni maoni kuhusu nini zaidi kifanyike ili kuhakikisha mapato
ya Serikali katika sekta ya madini yanaongezeka,” alisisitiza Kitwanga.
No comments:
Post a Comment