………………………………………………………………..
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Machi 3, 2015,
ameungana na mamia ya waombolezaji kumzika Mbunge wa Jimbo la Nyasa na
msanii mahiri wa muziki nchini, Mheshimiwa Kepteni John Damiano Komba,
kwenye makaburi ya Kanisa Katoliki katika Kijiji cha Lituhi, Wilaya ya
Nyasa, Mkoa wa Ruvuma.
Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Songea,
akitokea Dar es Salaam, kiasi cha saa tano na robo asubuhi, Rais Kikwete
amekwenda moja kwa moja Lituhi, karibu kiasi cha kilomita 140 kutoka
mjini Songea, kwa ajili ya mazishi ya Mheshimiwa Komba ambaye pia
alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi
(CCM).
Rais Kikwete amejiunga na waombolezaji akiwemo Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda kiasi
cha saa tisa mchana kwa ajili ya mazishi ya mmoja wa wasanii ambao
walijijengea heshima kubwa kwa nyimbo zake za uhamasishaji.
Wakati wa shughuli za mazishi ambazo kidini zimeongozwa na
Askofu John Ndimbo wa Jimbo Katoliki Mbinga, waombolezaji walisomewa
salamu za rambirambi ambazo zimetumwa na Rais wa Pili wa Malawi,
Mheshimiwa Bakili Muluzi ambaye sasa amestaafu.
Katika salamu hizo, Mheshimiwa Muluzi amesema: “Nilimjua Komba kama rafiki na taarifa za kifo chake cha ghafla zimenistua sana.”
Mwili wa Marehemu Komba uliteremshwa kaburini saa 9:30 mchana
huku ukishuhudiwa na mjane wa marehemu Salome Komba na watoto wake 11.
Rais Kikwete ameondoka Lituhi mara baada ya mazishi kurejea
mjini Songea kumalizia ziara yake ya siku mbili ya kikazi mkoani Ruvuma.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
3 Machi, 2015
No comments:
Post a Comment