MTANDAO wa Wasanii Tanzania
(SHIWATA) unaungana na watanzania wote kuomboleza kifo cha Makamu
Mwenyekiti wao, John Komba aliyefariki Jumamosi na kuzikwa jana nyumbani
kwao kijiji cha Litui, Mbinga mkoa wa Ruvuma.
Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Taalib katika salamu zake za
rambirambi alisema mtandao huo umempoteza kiongozi mwadilifu aliyetumia
kipaji chake cha usanii kuwaunganisha makundi ya wanamichezo,waigizaji,
wasanii wa luninga, bongo movie,wacheza sarakasi na waandishi wa habari
kuunda mtandao huo.
Alisema Kepteni Komba siku zote za
maisha yake aliamini sanaa ni mkombozi wa wanyonge katika jamii ambako
alitumia fani yake ya ualimu kufundisha wasanii wa fani mbalimbali
alipokuwa na kikundi cha Tanzania One Theatre (TOT), aliunda Kwaya,
maigizo, sarakasi, taarab na muziki wa dansi.
Marehemu Komba akiwa na kikundi
chake cha TOT aliibua vipaji vya wasanii mbalimbali waliotamba zamani na
wengine bado wanaendelea kutamba katika kama Nasma Hamisi Kidogo, Laila
Khatib, Sheba Juma, Selemani Pembe, Banza Stone, Mohamed Mrisho, Badi
Makule, Ali Star, Khadija Kopa, Othman Sudi, Abdul Misambano, Mwanamtama
Hamisi na Haji Boha.
Taalib alisema SHIWATA imempoteza
kiongozi aliyekuwa msaada mkubwa katika kuimarisha mtandao huo kwa hali
na mali na kuwashawishi wasanii wake wa TOT kujiunga na mtandao huo ili
kushirikiana katika kujenga kijiji cha wasanii cha Mwanzega, Mkuranga.
Marehemu Komba ambaye alikuwa
mwanachama mwenye kadi namba moja wa SHIWATA kati ya wanachama 8,000 wa
mtandao huo alikuwa akilipia michango yake na kuwa mfano kwa wengine.
Taalib alisema SHIWATA imewapoteza
wanachama maarufu katika kipindi cha karibuni na hivyo kuongeza pengo
katika utendaji wake kama Ibrahim Muchacho, Fundi Said (Mzee Kipara),
Seteven Kanumba, Hamisi Amigolas na Amina Ngaluma.
Alisema katika uongozi wa marehemu
Komba amesaidia kujengwa kwa nyumba 104 za wasanii katika kijiji cha
Mwanzega ambapo wasanii wanaendelea na ujenzi.
No comments:
Post a Comment