Na: Genofeva Matemu – Maelezo
Maafisa Utamaduni na wadau wa
utamaduni wametakiwa kuuenzi utamaduni wa watanzania kwa kutekeleza na
kusimamia utamaduni ulio sahihi na kuacha kuiga tamaduni zisizokuwa
zetu.
Rai hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na mwakilishi wa
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bw.
Raymond Mushi alipokua akifunga kikao kazi cha kumi cha Maafisa
Utamaduni kutoka Halmashauri zote Tanzania Bara.
Bw. Mushi amesema kuwa kikao kazi hicho kilichosimamia kauli
mbiu isemayo Fani za Sanaa zielimishe Umma Maudhui ya Katiba pendekezwa
kimefanyika wakati muafaka hasa ukizingatia taifa lipo kwenye hatua ya
kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ambalo litatumika pia
kupigia kura katiba pendekezwa.
“Sanaa ni shughuli pana kwa kuwa inaweza kufikisha ujumbe kwa
haraka katika jamii hasa kwa kutumia fani mbalimbali kama muziki,
ngojera, ngoma, maigizo na kadhalika hivyo kwa kupitia fani za Sanaa
Umma utaelewa maudhui ya katiba pendekezwa na kufanya maamuzi sahihi ya
kuipigia kura katiba pendekezwa”, alisema Bw. Mushi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Idara ya Utamaduni Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Afisa Utamaduni Bw. Habibu Msami
amesema kuwa kikao kazi cha kumi cha Sekta ya Utamaduni kimekuwa na
mafanikio chanya kwani washiriki wamepata fursa ya kujadili kwa kina
masuala mtambuko yanayoikabili sekta hiyo.
“Ni hakika kuwa tutakapotoka hapa tutakua mfano mzuri katika
Halmashauri na Asasi zetu kwa kuzingatia mambo ya msingi na kuhakikisha
tunautetea, tunaulinda na kuuendeleza utamaduni wetu kwa ajili ya ujenzi
wa Taifa”, alisema Bw. Msami.
Naye Afisa Utamaduni kutoka Kiteto Bibi. Bihawa Masawika amesema
kuwa kikao kazi cha sekta ya utamaduni kimewawezesha kupata maarifa
yatakayowawezesha kuwa wahamasishaji wakubwa na kuwa chachu na mabalozi
wazuri katika kutekeleza na kuendeleza masuala ya utamaduni nchini.
No comments:
Post a Comment