KAMPUNI ya Furniture Centre
(FCDL), na Shirikisho la Watengenezaji Samani Nchini (TAWOFE), wamesaini
makubaliano (MoU) kuongeza ubora wa bidhaa za samani zinazotengenezwa
nchini na kuzifanya zipate soko ndani na nje ya nchi.
Makubaliano haya yamekamilika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa
Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ikiwa ni mwendelezo wa
Tathimini iliyofanywa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
kwa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani, katika kuiwezesha sekta
ya Samani nchini kupitia vikundi na makampuni ya ndani.
Tathimini hiyo ya Baraza ya mwaka 2008, ilijikita katika kubaini
mahitaji na changamoto zinazoikabili sekta ya samani hapa nchini.
Baraza liliweza kuandaa warsha iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali na
ambapo matokeo ya tathmini hiyo yaliwasilishwa. Wadau kutoka sekta ya
umma na binafsi walishiriki katika mrejesho wa tathmini hiyo na wao pia
kuchangia maoni zaidi kwa ajili ya kuiboresha.
Washirika hao walisaini makubaliano hayo katika hafla
iliyoshuhudiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji wa
Uchumi na Uwekezaji), Dk Mary Nagu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la
Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Dk Anacleti Kashuliza, alisema
pamoja na kuwepo kwa fursa kubwa ya soko la samani hapa nchini bado
ushiriki wa vikundi na makampuni ya ndani katika soko hilo ni mdogo sana
kulinganisha na samani zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.
Alisema tunatoa wito kwa taasisi za Umma na Binafsi ziunge mkono
jitihada hizi kwa kununua samani toka kwa watengenezaji samani wa ndani
na ili kuwapa ushirikiano zaidi utakaowezesha kuimarisha sekta ya
samani zitengenezwazo ndani ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAWOFE, Bw Fredrick Waibi,
alielezea makubaliano kati ya FCDL na TAWOFE ni mkakati mzuri
utaomjengea uwezo fundi seremala kuweza kutengeneza bidhaa zitakazoweza
kukubalika kimataifa, kuongeza tija kazini na kupunguza umaskini kati ya
mafundi seremala.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa FCDL, Bw Shafik Bhatia, alisema kama
wadau muhimu wa samani nchini wameona umuhimu na wanajivunia
kushirikiana na Tawofe katika kuboresha huduma za samani nchini .
No comments:
Post a Comment