HASHIM Lundenga mkurugenzi wa Lino
International Agency inayoaandaa mashindano ya urembo ya Miss Tanzania,
ni mtu ninayemkubali sana katika suala la kujenga hoja na kupangua
changamoto za waandishi wa habari, ni aina ya mtu ambaye utapenda kumsikiliza tena na tena.
Lakini nikiri kuwa kwa mara
ya kwanza ameniangusha - Lundenga ameniangusha kwa namna alivyohodhi
mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika wiki iliyopita ambapo pamoja
na mambo mengine, suala la utata wa umri wa Miss Tanzania 2014, Sitti Abbas Mtevu lilichukua nafasi.
Kabla
sijasonga mbele, napenda niwajulishe kuwa kwa vyanzo vyangu binafsi
ikiwemo ndani ya Idara ya Uhamiaji Tanzania, nimejiridhisha kuwa hati ya
kusafiria iliyozagaa mitandaoni inayoonyesha kuwa Sitti amezaliwa mwaka
1989, si sahihi na hiyo inanifanya niamini kuwa cheti cha kuzaliwa cha
Sitti kilichotengenezwa mwezi Septemba mwaka huu kikionyesha kuwa
amezaliwa mwaka 1991, ni feki.
Kwa
hali hiyo, Sitti anapoteza sifa za kibalozi ambayo ni moja ya vigezo
vikubwa vinavyohitajika kwenye kinyang’anyiro cha Miss Tanzania –
Utakuweje na sifa za kibalozi huku ukiwa kinara wa kughushi nyaraka muhimu kama hizo? Tumewahi kushuhudia watu waking’olewa
kwenye michakato ya uchaguzi wa vyama vya siasa na hata vyama vya
michezo kwa sababu ya kughushi vyeti vya shule – Sitti hatofautiani
kabisa na watu hao.
Katika
mkutano huo wa waandishi wa habari, Sitti alionyesha cheti chake cha
kuzaliwa lakini alipohojiwa kuhusu hati yake ya kusafiria, Sitti akasema
hawezi kujibu mambo ya mitandao na kwamba yeye amekwenda kuzungumzia kuhusu cheti chake cha kuzaliwa tu.
Siiti
alionyesha kupoteza sifa nyingine ya kibalozi kwa kujibu maswali kwa
jazba tena kwa upeo wa kiwango cha chini mno – Unapoolizwa cheti chako
kilipopotea uliripoti wapi halafu ukasema hukujiandaa kujibu swali hilo,
linakuwa ni jambo la kitoto kuliko hata utoto wenyewe.
Unapowaambia
waandishi wa habari eti mmekuwa mkiniandama sana kwa mambo mengi ambayo
mengine si ya kweli maanake ni nini? Maanake ni kuwa kati ya hayo yapo ya ukweli, hakika Sitti ameonyesha uwezo mdogo sana wa kukaa mbele ya waandishi na kujibu hoja, ni mweupe sana.
Kwanini
nimesema Lundenga ameniangusha? Ni kwa sababu alimlinda Sitti asijibu
maswali ya msingi, hakutaka kumbana Sitti atumie fursa hiyo kusafisha
ukungu wote uliomzunguka, inakuweje Sitti akatae kujibu swali kuhusu
cheti chake cha zamani kilichomwezesha kupata hati ya kusafiria? Tena
Sitti anasema kwa macho makavu: “SIWEZI KUJIBU HILO SWALI” kisha Lundenga anamkingia kifua.
Kama
cheti cha zamani ndicho kilichompatia hati ya kusafiria Sitti, hati
inayoonyesha kuwa ana umri wa miaka 25 ambao ni nje ya umri unahitajika
Miss Tanzania na hata Miss World, basi Lungenga pia angehitaji kusikiliza majibu ya msingi kuhusu hoja hiyo na si kulikwepa swali.
Kulikwepa swali hili muhimu ni sawa na kufunika kombe mwanaharamu apite, lakini napenda kumjulisha Lundega, Sitti na washika dau wengine kuwa wako wanaharamu wengine huwa hawapiti nata ufunike vipi kombe.
Ukibahatika kupitia maandishi ya watu kama Godsos Mukama (Mwandaaji wa Miss Mara) na William
J Malecela (mmoja wa waandaji wa Miss Ilala), utagundua kuwa hata watu
walioko jikoni nao pia hawaiungi mkono kamati ya Miss Tanzania juu ya
uhalali wa Sitti kutwaa taji.
Ushindi
wa Sitti umezongwa na mambo mengi yenye utata - Ndugu, jamaa na
mashabiki wake kuingia na mabango yenye maandishi makubwa SITTI, ilikuwa
ni jambo ambalo sikumbuki kuwahi kuliona kabla ya shindano la mwaka
huu, haya ni mashindano ambayo hata kwenda kumtunza pesa mshiriki
jukwaani huwa haikubaliki kwa vile inaweza ikawavuruga majaji, inakuweje
mabango kama yale yatawale ukumbini?
Tunaambiwa
Sitti ajibu kwa lugha mbili – kiingereza na kifaransa, tunajua wazi
kuwa lugha zinazotumika katika ngazi zote za Miss Tanzania ni Kiswahili
na Kiingereza, hiki Kifaransa kilitokea wapi? Yaani mshiriki anaulizwa
atajibu kwa lugha gani, akachagua Kiingereza lakini baada ya kumaliza
kujibu akasema “Najibu na kwa Kifaransa” … mtoto wa kike akatiririka.
Kwa
kuangalia ‘fujo’ zote hizo za Sitti pamoja na tuhuma za rushwa
zilizotajwa juu ya ushindi wake, Lundenga alistahili kumwacha Sitti
ajibu kila utata uliostahili majibu, kumlinda Sitti na maswali ya
wanahabari kunaweza kuwafanya watu wahisi vitu vya ajabu.
Mwisho
napenda kuitahadharisha kamati ya Miss Tanzania kuwa hilo liwe funzo
kwao, ipo haja ya kupitia nyaraka nyingi za washiriki kuanzia vyeti vya
kuzaliwa, vitambulisho vya kupigia kura, passport na leseni za
kuendeshea gari (kwa wenye nazo) ikibidi hata vyeti vya shule. Tukumbuke
kwenye soka letu, Tanzania tuliwahi kuporwa nafasi ya kushiriki fainali
za Afrika kwa vijana kwasababu ya umri wa mchezaji mmoja tu, suala la
umri ni nyeti sana, tusiishie kufunika kombe mwanaharamu apite.
No comments:
Post a Comment