…………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu
Wasanii nchini wameaswa kuzingatia muda wanapohitajika kufanya onesho au kazi yoyote ya jamii ili kuepuka kudharaulika na kuonekana watu wa hovyo na wasiyojali muda.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Sanaa
kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ernest Biseko wakati
akihitimisha Jukwaa la Sanaa la BASATA mapema wiki ambapo Kikundi cha
Wakali Sisi kilichoshinda kwenye onesho la dansi mia mia kilitoa
burudani.
“Hakuna kitu muhimu na cha msingi
kwa msanii kama kuzingatia muda. Wasanii tumekuwa tukilalamikiwa sana
kuchelewa kwenye maonesho au kwenye shughuli za kijamii ambazo
zinatutaka tuwahi. Hii haipendezi” alisema Biseko.
Aliongeza kwamba, wadau wengi wa
Sanaa hawafurahishwi hata kidogo wanapoona msanii anafika kwa kuchelewa
kwenye shughuli hali ambayo imekuwa ikiwafanya wachukie na kuchukua
maamuzi ya kufanya vurugu.
Mdau mwingine wa Sanaa ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Sanaa za Maonesho nchini Nkwama Bhalanga alisema kuwa,
wasanii wamekuwa wakidharaulika na kuonekana wa hovyo-hovyo kutokana na
kutokuzingatia muda hali ambayo inawafanya washindwe hata kufanya vizuri
jukwaani kutokana na muda mfupi wa maandalizi.
“Msanii lazima afike kwenye tukio
walau saa moja kabla ya onesho ili azoee mazingira lakini pia afahamu
wapi pa kubadilishia mavazi, kupumzika na kuoga baada ya onesho lake”
alisisitiza Bhallanga.
Awali katika Jukwaa hilo, Kikundi
cha kudansi cha Wakali Sisi ambacho wiki kadhaa zilizopita kiliibuka
kidedea kwenye onesho la Dansi Miamia kilitoa burudani ya kuvutia kwa
wadau wa Sanaa.
No comments:
Post a Comment