Hivi karibuni kumezuka taarifa za upotoshwaji zilizotolewa kwenye
mitandao ya kijamii kwamba Serikali ya Tanzania imemteua Bw. Salaah,
Mkurugenzi wa Home Shopping Centre, (pichani ) kuwa Konseli wa Heshima
(Honorary Consul) kwenye mji wa Guangzhou kwenye Jimbo la Guandong.
Watoa
taarifa hizo, hawakutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai yao zaidi ya
kutoa picha mbalimbali za Bw.Salaah kutoka kwenye mitandao mingine ya
kijamii.
Taarifa hizo sio za kweli.
Kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za mahusiano ya kidiplomasia ya China, nafasi ya Konseli wa Heshima
haitambuliki 'mainland' China. Kwa maneno mengine hakuna nchi yoyote
duniani inayoweza kuteua mtu kuwa Konseli wa Heshima katika eneo lolote
la China isipokuwa Hong Kong ambako kuna mamlaka huru za utawala
zinazofuata sheria zake.
Kwa
faida ya umma, ni vema kufafanua kwamba Nchi ya China inakubali nchi za
Nje kufungua Ubalozi kamili (Embassy) ambao makao yake yanatakiwa
kuwepo katika mji Mkuu wa China- Beijing na Konseli Kuu ama kwa lugha
iliyozoeleka Ubalozi Mdogo (General Consulate) ambao unaweza kufunguliwa
kwenye makao Makuu ya mji wowote ule katika Majimbo ya China.
Watu
wengi wamekuwa wakichanganya Ubalozi Mdogo au Konseli Kuu (General
Consulate) na Konseli (Ubalozi) wa Heshima (Honorary Consulate).
Konseli Kuu (General Consulate) ni sehemu ya Ubalozi (ndio maana wengi
huuita Ubalozi Mdogo) ambapo kiongozi wake na maafisa wake wote ni
watumishi wa Serikali kutokea Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa. Masharti
ya kuwa Mkuu wa Konseli 'General Consulate' lazima uwe Afisa Mwandamizi
wa Mambo ya Nje mwenye uzoefu usiopungua miaka 10 ya Utumishi katika
Wizara ya Mambo ya Nje.
Kwa
muktadha huo, taarifa kwamba Bw.Salaah ameteuliwa kuwa Balozi wa
Heshima wa Tanzania huko Guangzhou sio kweli kwasababu Sheria za China
haziruhusu uwepo wa nafasi hiyo. Aidha, Bw Salaah hawezi kuwa Balozi
Mdogo (Consul General) kwa kuwa yeye sio mwajiriwa wa Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Hivyo habari zinazosambazwa kwenye
mitandao ya kijamii sio za kweli na zinalenga kuupotosha umma.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA MAMBO YA
NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
OCTOBER 30, 2014
No comments:
Post a Comment