Awali ya yote napenda nichukue
fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kujumuika pamoja leo
hii katika tukio hili muhimu linalohusu mkutano mkuu wa sita wa
mameneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Aidha nichukue nafasi hii pia kuipongeza Menejimeti ya TAA
pamoja na wafanyakazi wote kwa kufanikisha maandalizi ya mkutano huu na
kunipa heshima hii kubwa ya kuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa mkutano
huu. Kwa hili nawashukuru na kuwapongeza sana.
Ndugu Wajumbe,
Pamoja na shukrani zangu za awali, nimefarijika sana kuona
Mkutano huu unawajumuisha Viongozi wa Menejimenti na Mameneja wote wa
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini kote wapatao sitini (60) kama
Mkurugenzi Mkuu alivyoeleza katika hotuba yake. Katika mkusanyiko huu,
ni matarajio yangu kwamba Mkutano huu ulikuwa ni fursa nzuri ya
kubadilishana mawazo kwa ukaribu zaidi na kutafuta ufumbuzi wa matatizo
na changamoto zinazohusiana na shughuli za utoaji huduma katika Mamlaka
yenu. Aidha, hii ni njia mojawapo ya ushirikishwaji na uwajibikaji
katika uendeshaji wa Taasisi hii.
Sambamba na pongezi zangu za awali, nichukue fursa hii pia kwa
kuwapongeza tena juu ya kauli mbiu ya mkutano mliyoichagua ambayo
inaendana na mabadiliko ya huduma za makampuni yaliyoanza kutoa huduma
za usafiri wa anga kwa gharama nafuu ambayo yatakuwa chachu ya ukuaji wa
sekta ya Anga Tanzania. Ukuaji wa “low cost carriers” kwa sasa na kwa
siku zijazo ni wa uhakika, hivyo nawaasa kuwa TAA kama mdau mkuu katika
ukuaji huo, ihakikishe kwamba inajipanga vizuri kwa kuweka mazingira
yanayowezesha kukabiliana na changamoto zitakazotokana na ukuaji huo.
Bila shaka na kama nilivyoarifiwa,
mada mbalimbali zilizoandaliwa zilijadiliwa kwa kina na ufasaha
kutokana na kwamba zote zilijikitika katika kufanikisha lengo la mkutano
huu, ambazo zimeainishwa vizuri katika kauli mbiu yake.
Ndugu Wajumbe,
Wizara tunajivumia sana mafanikio ambayo TAA imeyapata tangu
kuanzishwa kwake, ni dhahiri kwamba mafanikio hayo si tu kwamba
yatatokana na mipango mizuri mliyojiwekea bali pia yanatokana na
usimamizi wenu wa karibu juu ya malengo hayo kwa kuwashirikisha kwa
karibu wafanyakazi walioko chini yenu. Dunia ya sasa ya karne ya 21
katika viwanja vya ndege, inatawaliwa zaidi na utoaji huduma ulio bora
ukilenga kuwavutia wateja na hili linaweza tu kufikiwa iwapo wafanyazi
watahamasishwa na kupewa mafunzo ambayo yatawaongezea ujuzi ukiwemo wa
kiteknolojia, weledi na hamasa ya kufanya kazi kwa bidii zaidi. Na ili
ushirikishwaji huo utoe matunda yanayostahili, mnaaswa mhakikishe kwamba
wafanyakazi hao wanahamasishwa na kupewa mafunzo stahiki na hasa katika
kusimamia miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa sasa katika viwanja
vyenu, inayokuja na inayotarajiwa.
Sanjari na hili mnaaswa pia
mhakikishe kuwa ili kujua na kupima utendaji wao wa kazi, watumishi hao
wapimwe juu ya utendaji wao wa kazi wa kila siku kwa kutumia mfumo ulio
wazi wa kupima utendaji wa kazi wa watumishi wa serikali yaani OPRAS.
Nimefahamishwa kuwa upimaji wa utendaji kazi chini ya OPRS umekuwa na
changamoto nyingi. Hata hivyo, siamini kama changamoto hizo
hazitatuliki, hivyo kwa weledi mlio nao, naomba muendelee kuboresha
mfumo huo kwa lengo la upimaji bora wa watumishi hatimaye ulete matunda
ya pamoja kwa utendaji ulio bora kwa Mamlaka.
No comments:
Post a Comment