…………………………………………………………….
Kamati ya kudumu ya Bunge ya
Kilimo, Mifugo na Maji jana imeanza ziara ya kutembelea miradi
mbalimbali inayotekelezwa chini ya Ushirikiano wa Nchi za Bonde la Mto
Nile (Nile Basin Initiatives) nchini Sudan.
Lengo la ziara hiyo ni kupata
uelewa wa pamoja kuhusu ushirikiano uliopo katika kusimamia na
kuendeleza rasilimali za Bonde la Mto Nile kati ya Nchi wanachama, huku
Tanzania na Sudan zikiwa ni miongoni mwao.
Katika ziara hiyo Waziri wa Maji,
Prof. Jumanne Maghembe ambaye ameambatana na kamati hiyo amesema kwamba,
dhumuni kuu la ziara hiyo ni kwenda kuona na kujifunza namna Sudan
inavyotumia maji ya Mto Nile kwa ajili ya maendeleo yake kiuchumi katika
shughuli za kilimo, ufugaji, utalii na biashara.
“Tanzania inachangia asilimia 28
ya maji ya Mto Nile na ina utajiri mkubwa wa rasilimali hii ya maji,
hivyo hatuna budi kujifunza kutoka kwa wenzetu ili nasi tupate ufahamu
mzuri na tuweze kupata maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali
kupitia rasilimali hii. Na hatua ya kwanza ni kuona wenzetu wa Sudan
wanafanya nini mpaka kufikia hatua kubwa waliyopiga leo hii”, alisema
Prof. Maghembe.
Ziara hiyo ni mwaliko kutoka nchi
ya Sudan na itachukua siku nne, itajumuisha kutembelea Bwawa la Merowe
linalotumika kwa ajili ya kuzalisha umeme na shughuli za kilimo cha
umwagiliaji, inategemewa kuleta tija kwa maendeleo ya Sekta ya Maji
nchini na uchumi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment