|
Rais Jakaya Kikwete |
Said Mwishehe
PANAPO MAJAALIWA ya Mungu, kesho tunaungana na mataifa mengine duniani kusheherekea mwaka mpya wa 2015.
Hivyo, kwa hesabu za kalenda ya mwaka 2014, leo hii tunamaliza muda uliobaki kabla ya kuingia mwaka 2015.
Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kuendelea kutupa pumzi yake. Ametujaalia afya njema. Hili ni jambo la kushukuru.
Pia nitumie nafasi hii kutoa pole kwa ndugu, rafiki na jamii zetu ambao leo hii hatunao tena. Wametangulia mbele za haki.
Hiyo inatokana na mapenzi yake muumba wa mbingu na ardhi. Tuwaombee dua njema huko waliko.Mbele zao, nyuma zetu.
Wakati tunakaribia kuingia mwaka 2015, nitumie nafasi hii kuowambea wale wote wenye kusumbuliwa na magonjwa mbalimbali.
Imani yangu Mungu atawaponya na kuwarejesha kwenye afya njema na hatimaye kuendele na ujenzi wa taifa.
Wakati tunajiandaa kuupokea mwaka mpya, kuna mambo mengi ambayo yametokea kwenye mwaka huu wa 2014.
Yapo ambayo yametunufaisha kama taifa lakini wakati huo huo yapo ambayo yametufedhehesha.
Mwaka 2014 ulikuwa mwaka wa
matukio mengi katika nyanja mbalimbali. Nikiri kuna mambo ya kujivunia
na kuna mambo ya hovyo ambayo yametokea kwenye taifa hili ambalo
linaendelea na juhudi za kusaka maendeleo yake.
Sote ni mashahidi Watanzania kwa
nafasi zao mbalimbali wameendelea na ujenzi wa taifa leo. Wameendelea
kudumisha umoja na mshikamano wao.
Wameendelea kuungana kupigania
maisha yao. Ni watu ambao hawataki kukataa tamaa. Wanafanya kila juhudi
kuhakikisha taifa linasonga mbele.
Nikiri kauli ambayo inaliumiza
taifa hili ni kuendelea kuimba wimbo wa “Sisi maskini”. Wimbo ambao
kwangu mimi unaniumiza kichwa. Sitaki hata kuusikia. Sitaki kuusikia
kwasababu ni sehemu ya adui wetu wa maendeleo yetu.
Sisi maskini ni kauli ambayo
imetukwamisha kwa miaka mingi sasa. Hata mwaka huu wa 2014, kauli ya
sisi maskini imeturudisha nyuma.
Kujiita kila siku maskini ndio matokeo yake tunashinda kuishi maisha ya kuendelea kuomba misaada. Kisa tu nchi yetu eti maskini.
Kwangu naamini sisi si maskini ila
huenda tunakosa mipango na usimamizi mzuri wa kufikia malengo yetu.hili
ndilo tatizo ambalo linatusumbua kwa miaka mingi.
Mwaka 2015 ni mwaka wa kubadili
mitazamo na fikra zetu. Tukitumia vema rasilimali zetu, tutapiga hatua.
Kila kitu tunacho.tunachotakiwa ni mipango na usimamizi mzuri. Tuache
akili za kuwa tegemezi kwa kila jambo.
Inashangaza tunapokuwa na msitu
mkubwa wa misitu kama ule wa Sao hili Iringa halafu kijiti cha
kusafishia meno kinatoka China. Ama kweli!
Inasikitisha kuona imefika mahali
eti kila kitu lazima kitoke nje. Kasumba hii inatokana na yale yale
ambayo wengi yametutawala kwenye akili zetu kuwa lazima tuwe tegemezi.
Hatupaswi kuwa na akili hiyo kwa mwaka 2015. Ni mwaka wa kutafakari kama taifa nini tufanye ili tusonge mbele.
Kwa bahati mbaya tumekuwa na kundi
kubwa ambalo linatumia muda mwingi kupiga soga vijiweni kwa ajenda
ambazo hazina mashiko ya kimaendeleo. Ni rahisi kusikia watu wanajadili
nani kavaa nini. Fulani analula nini?
Wanaojadili tunapigaje hatua kama
taifa ni wa chache. Hata hao tunaowategemea kutupigania wamekuwa wa
kuishi kwa matukio. Likija tukio hili wamo, likija lingine wamo.Mafundi
wa kuongoa kuliko kutenda.
Inasikitisha sana.Tumeyaona hayo
mwaka 2014.Si vizuri yakajirudia tena mwaka 2015. Kufanya kosa si kosa
ila kurudia kosa, ndio kosa. Tusimamie kama nchi tuangalie maisha yetu.
Tumetoka wapi na tunakwenda wapi.
Tukisoma vitabu vya historia
tunaambia Tanzania na China zilianza harakati za kusaka maendeleo mwaka
mmoja. Nenda leo China kaingalie.
Hatufanani nayo kwa namna yoyote
ile.Watu tulianza nao kwenye harakati za kutafuta maendeleo, eti leo
tunawapigia magoti kuwaomba msaada.
Wachina wameijenga nchi
yao.Wameamua kusimama kidete kuhakikisha taifa lao linapiga hatua na
kuwa lenye nguvu duniani. Sishangai Marekani inapokwenda kuomba misaada
ya kifedha China.
Kwetu sisi maendeleo yetu yamekuwa
ya mwendo wa kinyonga. Wananchi wamekata tamaa ya maisha. Kila kukicha
wanasema afadhali ya jana. Ndio maisha ambayo tumeamua kuishi.
Imefika mahali Wachina wameamua
kuja nchini kwetu na kufanya kazi ambazo tumeshindwa kuzifanya. Nenda
Kariakoo jijini Dar es Salaam, Wachina wanauza maua.Wanauza karanga.
Inasikitisha inapofika mahali hata
karanga tunashindwa kuuza. Tunasibiri Wachina waje wauze. Halafu
tumebaki kupiga kelele tu.Tumefika mahali pabaya.
Sifa ya taifa kupiga hatua za maendeleo linahitaji kuwa na siasa safi, utawala bora, ardhi na watu.
Nikiri tunaweza kuwa tumekosa
siasa safi na uongozi bora lakini tuna ardhi ya kutosha na watu. Kwa
bahati mbaya watu wapo lakini kasi ya maendeleo haiendani na idadi yetu.
Kitendo cha kukosa siasa safi
imefika mahali, wanasiasa wengi wametugeuza kama vile kichwa na
mwendawazimu. Wanatuongopea watakavyo.
Wanajua hatuna tunaloweza
kulifanya. Hakika mwaka 2014, licha ya kufanya mambo ya maendeleo, yapo
ambayo tunapaswa kujiepusha nayo mwaka 2015.
Msomaji wa safu hii, baada ya
kutoa maelezo hayo ambayo kwangu mimi kwa siku ya leo ni kama utangulizi
sasa nije kwenye ajenda yangu ya Jumatano ya leo.
Ajenda yenyewe ni hili sakata la
Escrow.Sakata ambalo limekuwa gumzo kwenye kila kona ya nchi yetu.
Limekuwa likizungumza na kila mtu. Kama hulizungumzi wewe basi
analizungumza mwenzio.
Sakata la Escrow limetikisa nchi
yetu kwa sehemu kubwa. Sote tunafahamu mjadala huo wa Escrow unatokana
na utata wa fedha wa sh. bilioni 306 zilizopo kwenye akaunti ya Tegeta
Escrow, wajanja kuamua kuzichukua.
Wanasiasa wa kada mbalimbali
wamekuwa wakilizungumza hilo kwa kina. Wamekuwa wakipambana kwa hoja.
Wamekuwa wakijadili na kuelezea umma kuhusu fedha hizo.
Nikiri mwaka 2014, mjadala wa
Escrow kwangu mimi naona ulikuwa ni mjadala uliochokuwa sehemu kubwa ya
mazungumzo kuliko mijadala mingine.
Ni kweli kulikuwa na mjadala
kuhusu Katiba mpya lakini ujio wa sakata la Escrow umefunika kabisa
mazungumzo ya Katiba inayopendekezwa.
Kwa kuwa hata wanasiasa wetu nao
wanaishi kwa matukio. Wengi wao wameachana na ajenda ya Katiba mpya
ambayo wananchi wanahitaji kuelimisha licha ya wao wenyewe kujisomea
Katiba inayopendekezwa kabla ya kufanya uamuzi kwa kupiga kura ya ndio
au hapa.
Leo hii ili mwanasiasa aonekane amezungumza jambo la maana basi anaamini akizungumzia Escrow ndio nyota ya siasa inasafishika.
Sina tatizo na wanasiasa ambao
wamelizungumzia sakata hilo hadi hapa lilipofikia. Tunajua Bunge limetoa
maazimio nane kwa Serikali.
Maazimio ambayo kwa sehemu kubwa
Serikali ya Rais Jakaya Kikwete inatakiwa kuamua kwa kuchukua hatua
dhidi ya wanaohusishwa na uchotaji fedha wa Escrow.
Ndio maana aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema ameamua kuachia ngazi.
Uamuzi huo unatokana na ukweli kwamba ushauri wake kisheria hakueleweka. Jaji Werema anasema amechafua hali ya hewa.
Pia tunafahamu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi naye amsimamishwa kazi ili
kupisha uchunguzi. Kisa sakata hilo hilo la Escrow.
Nani ambaye hafamu kama aliyekuwa
Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka
naye ametemwa kwenye baraza la mawaziri.
Kilichomuondoa ni kupokea fedha za Escrow.Prof. Tibajuka aliwekewa kwenya akaunti yake binafsi sh. bilioni 1.6.
Wakati mjadala huo unaendelea,
hakuna mwanasiasa ambaye ameweza kupata ujasiri wa kuliambia taifa fedha
hizo ni za umma au si za umma. Nani mwenye fedha hizo?.
Ujasiri ambao wanasiasa wetu walio
wengi wanao hadi sasa ni kwamba sh. bilioni 306 za Escrow ni za umma.
Wamesema hivyo wakiwa bungeni na wanaendelea kusema hivyo nje ya Bunge.
Kwangu mimi na hata kwa Watanzania
wengine, nimefurahishwa na hotuba ya Rais Kikwete.Hotuba ambayo aliitoa
Desemba 22 mwaka huu. Alikuwa anazungumza na wazee wa mkoa wa Dar es
Salaam.
Kama kiongozi wa nchi ameonesha kulifahamu vema suala hilo. Akatumia nafasi hiyo kuelezea historia nzima ya sakata la Escrow.
Akaeleza namna ambavyo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na IPTL walivyokuwa wanalipa.
Pia, akaeleza namna ambavyo
akaunti ya Tegeta Escrow iliovyofunguliwa hadi hatua ya IPTL na wanahisa
wenzake kuuziana hisa na kisha kufunga akaunti ya Tegeta Escrow na
kuchukua fedha zilizomo.
Rais Kikwete baada ya kutoa
maelezo mengi ya kueleweka pengine kuliko yale yaliyokuwa yanatolewa na
wanasiasa walio wengi akatumia nafasi hiyo kuwahakikishia Watanzania
kuwa fedha hizo ni za IPTL.
Rais Kikwete katika hotuba yake
alisema”Fedha hizo ni za IPTL maana ni malipo ambayo yalikuwa yanalipwa
kutoka Tanesco ambazo ni tozo la uwekezaji, lakini toafuti yake fedha
zilikuwa zinawekwa kwenye akaunti maalumu”.
Kimsingi hotuba ya rais imejibu
swali la msingi ambalo Watanzania wengi walikosa kulisikia.Pamoja na
kusema fedha hizo ni za IPTL bado akauthibitisha umma kuna kodi ya
Serikali ndani yake.
Hivyo tunapoumaliza mwaka 2014,
naamini rais amesema kile ambacho wengi tulipaswa kukisikia.Akasisitiza
uchunguzi ufanyike na kisha sheria ichukue mkondo wake.
Akaagiza mamlaka zinazohusika na uchunguzi zitakapokamlisha taarifa , yeye atakuwa na uamuzi wa kufanya.
Baada ya kulifafanua kwa kina
suala hilo, rais akatumia nafasi hiyo kuweka wazi Waziri wa Nishati na
Madini Profesa Sospeter Muhongo amemuweka kiporo.
Bwana we! kauli hiyo ya Prof.Muhongo kuwekwa kiporo imeamsha hasira za wanasiasa hasa za wapinzani.
Wametoa matamko ya kumtaka Rais Kikwete kumuwajibisha Prof.Muhongo kwa kumuondoa kwenye nafasi hiyo.
Wengine wametangaza kufanya maandamano nchi nzima.Najiuliza sababu za msingi za kufanya maandamano hayo.
Najiuliza hivi wanaotaka
Prof.Muhongo aondolewe kwenye nafasi hiyo ni kweli wanashinikiza kwa
maslahi ya Taifa au kwa maslahi binafsi.
Hapa kuna siri kubwa, ambayo wenye
kumshinikiza rais amuondoe Prof.Muhongo kwenye nafasi ya uwaziri
wanaijua. Nani ambaye hajui kazi ambayo imefanywa na Prof.Muhongo kwenye
wizara hiyo.
Amefanya mambo makubwa kwa maslahi
ya nchi.Waziri Muhongo kwa usimamizi wake mzuri umeme umekwenda kwenye
vijiji mbalimbali vya nchi yetu.
Nimezunguka wilaya za nchi hii 129 hadi sasa.Naiona kazi ambayo Prof.Muhongo ameifanya katika nishati ya umeme.
Nani ambaye hajui umuhimu wa
nishati ya umeme kwa wananchi. Misimamo yake katika wizara hiyo
imefanikisha ujenzi wa bomba la gesi.Angekuwa Waziri legelege , bomba la
gesi kutoka Mtwara kuja(kwenda) Dar es Salaam lisingejengwa.
Alijua anasimamia maslahi ya
taifa.Pia najua kwenye eneo la gesi amekasirisha wengi.Wapo ambao
hawataki hata kumsikia.Leo si wakati wake kuzungumzia hilo.
Wanasiasa wanataka rais amuondoe
Prof.Muhongo, hivi waziri mwingine ambaye atakwenda kwenye wizara hiyo
na kukaa kwa miezi nane iliyobaki ya utawala wa rais Kikwete anakwenda
kufanya jambo gani kubwa.
Kuna dhambi gani Waziri Muhongo akiachwa amalizie muda ambao Rais Kikwete ameubakisha.
Kwa kuwa tunaingia mwaka 2015, ni
bora niseme ukweli maana utaniweka huru.Naamini sioni sababu ya
kumuondoa Waziri Muhongo Wizara ya Nishati na Madini.
Tangu amekuwa Waziri wa Nishati na Madini Waziri Muhongo amefanya kazi kubwa na nzuri.Hata hao ambao leo wanamuandama wanajua.
Nikiri najua, haya ninayoeleza kuna watu nawakera lakini ni bora niwe huru kwenye kile ninachoamini.
Kauli ya Mwishehe, kaushauri Rais
wangu, Rais Jakaya Kikwete , nakuomba umuache Waziri Muhongo amalizie
kazi anayoifanya kwenye wizara hiyo.Binafsi sioni mahali ambapo Waziri
Muhongo amechukua fedha za Escrow.
Sioni mahali ambapo Waziri Muhongo ameshauri fedha zitoke. Waziri Muhongo msimamo wake unajulikana wazi kuhusu fedha hizo.
Kwa bahati mbaya wanasiasa wetu
wameng’ang’ania tu kumtaka rais amuondoe Muhongo badala ya kutoa suluhu
ya nini kifanyike ili hayo ambayo yanatokea na kusababisha taifa
kushindwa kuchukua kodi yake yasijirudie.
Wanasiasa wanashindana kuita vyombo vya habari kumshinikiza rais kumuondoa Waziri Muhongo.
Naamini na ndio ukweli wanafanya
hivyo si kwasababu ya maslahi ya taifa , bali wanafanya hivyo kwa msuko
mwingine. Ipo siku nitausema.Kwenye hili nitasimamia ukweli.
Kwenye siasa za Tanzania kuna
mambo huwa yanakera sana. Moja ya mambo yanayokera ni pale mtu
anaposimama kujifanya anapigania maslahi ya taifa kumbe, kichwani kwake
anawaza tofauti.
Kuna wakati huwa najiuliza kwanini
, wanashinikiza Prof. Muhongo aondolewe. Nawaza weee , lakini napata
majibu tofauti tofauti. Moja ya jibu ambalo huwa nalipata ni kwamba
wanaogombea urais nao wana yao kwenye hilo.
Tena si wa CCM tu, bali hata wa upinzani. Wanaona sakata la Escrow ni karata ya mwisho ya kufanikisha malengo yao.
Wengine wanaamini kupitia sakata hilo itakuwa njia rahisi ya kuiangusha Serikali ya Rais Kikwete bungeni.
Hivyo, kila mmoja analiangalia
kivyake na si kweli wote wanaopigania hilo ni kwa ajili ya maslahi ya
taifa. Ingekuwa ni maslahi ya taifa wangetuambia kwenye sh. bilioni 306
za Escrow za umma ziko sh. ngapi?
Nimalizie kwa kueleza tunaingia
mwaka 2015, tudumishe upendo, umoja na mshikamano wetu. Najua wapo ambao
watakaosema nimetumwa. Sijatumwa. Sitajali.
Kubwa zaidi kila Mtanzania ana
haki ya kutoa maoni yake kwa kile anachokiamini anaweza kuchangia alau
kidogo hasa kwa kuzingatia mwaka 2014 umebakisha saa chache tu wa uhai
wake.
Karibu mwaka 2015, nitumie nafasi
hii kuwataka mafanikio mema kwenye mwaka wa uchaguzi wanasiasa wote.
Mwaka ambao kila anayetaka kugombea udiwani, ubunge au urais anarudi
kuomba kura kwetu.
Nawaheshimu wanasiasa wote na wa vyama vyote. Kwenye ukweli nipo pamoja nanyi na kwenye uongo nitakuwa kando yenu.
Tuwasiliane 0713833822