NA MWANDISHI WETU
HATIMAYE Mkurugenzi wa Kampuni
ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam, Alex Msama, ameibuka na
kutamka yeye si Meneja wa malkia wa nyimbo za injili nchini, Rose
Muhando akisema amekuwa akishirikiana naye katika mazingira ya kawaida
kama ilivyo kwa waimbaji wengine.
Kwa mujibu wa taarifa ya Msama
kwa vyombo vya habari jana, yeye akiwa mlezi wa waimbaji wote wa muziki
wa Injili, amekuwa akishirikana nao kwa karibu kutokana
na nafasi yake katika huduma hiyo ya uimbaji kwa kipindi cha miaka 15.
Msama, mtu aliyechangia kwa
kiasi kikubwa maendeleo ya muziki wa injili nchini kutokana na kuandaa
matukio ya muziki huo kama Tamasha la Pasaka, uzinduzi wa albamu na
Tamasha la Krismas, alisema ameamua kutoa tamko hilo kutokana na
malalamiko ya muda mrefu ambayo amekuwa akipata juu ya Rose.
“Nimekuwa nikipokea malalamiko
mengi ikiwemo kutoka kwa viongozi wa kiroho wakiwemo wachungaji, kwamba
pengine nimekuwa nikimzua Rose (Muhando) katika mtamasha wanayomualika
na kushindwa kutokea.
“Lakini, naomba watumishi wa
Mungu wanielewe katika hili, sipokei mialiko wala simzuii Rose. Mimi
ninapokuwa na matamasha, nimekuwa nikimualika kama wafanyavyo wengine.
“Nimekuwa nikimlipa kiasi cha
fedha anachotaka na hakuna zaidi, hivyo mimi sio Meneja wake,” alisema
Msama katika taarifa hiyo na kuongeza:
“Agosti mwaka huu, kampuni yangu
ilidhamini uzinduzi wa albamu yake ya Kamata Pindo la Yesu, haikuwa na
maana kwamba ni Meneja wake.
“Nilimualika uzinduzi wa albamu
ya Uko Hapa ya msanii John Lissu Oktoba mwaka huu, nilimlipa fedha,
lakini hakutokea kama ambavyo amekuwa akifanya kwa wengine ambao
wamekuwa wakilalamikia tabia hiyo,” alisema Msama.
“Pia wiki iliyopita nilikuwa na
Tamasha la Krismasi tulikubaliana aje katika maonesho hayo, lakini
hakutokea na tulishamlipa,” alisema Msama kwa masikitiko na kuongeza
kuwa amemsamehe na anamuombea kwa Mungu aweze kubadilika.
Alieleza kuwa hana tatizo na
mwimbaji huyo, wala hana ugomvi naye, lakini amekuwa akipata taabu
kutoka kwa baadhi ya wachungaji pale Rose anapoalikwa halafu hatokei na
inaonekana yeye ndiye amemzuia.
“Sijawahi kupokea mialiko kwa
niaba ya Rose, kila kitu anafanya mwenyewe, hivyo ni vyema wadau
wakafahamu hilo,” alisema Msama na kusema angekuwa mwepesi wa
kulalamika, angeshafanya hivyo muda mrefu dhidi ya Rose.
Aidha, Msama amekana kuhusiana
na madai ya Rose kutumia dawa za kulevya na kusisitiza kuwa hajawahi
kumuona akijidunga kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa
vikiripoti na kuongeza kama ikiwa ni kweli, hilo pia ni suala binafsi.
“Baadhi ya vyombo vya habari
vinaandika ni mjamzito, nafikiri pia hayo ni mambo yake binafsi na
hakuna mtu mwenye haki au uhalali wa kuhoji hilo.Yule ni mtu mzima na
mwenye kujielewa,” alisema Msama.
Rose ni mwimbaji mahiri wa
muziki wa injili nchini aliyejipatia sifa ndani na nje ya ukanda wa
Afrika Mashariki ambaye mwishoni mwa mwaka 2013, alisaini mkataba
wa kufanya kazi na kampuni ya muziki ya Sony ya Afrika Kusini.
Miongoni mwa albamu zilizompa
umaarufu Rose kiasi cha kuwa alama ya mafanikio ya muziki wa injili
nchini, ni ‘Uwe Macho,’ Nyota ya Ajabu (Zawadi ya Krismasi), Jipange
Sawasawa, Kitimutimu, ‘Mungu Anacheka’ na Wololo na Kamata Pindo la Yesu
aliyoachia hivyo karibuni.
No comments:
Post a Comment