Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Damian Lubuva
akizunguza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya tume ya
uchaguzi jijini Dar es salaam wakati alipozungumzia maandalizi ya
uboreshaji wa daftari la wapiga kura, kura ya maoni ya Katiba mpya na
uchaguzi mkuu mwezi oktoba mwaka huu, kulia ni Mkurugenzi wa Tume ya
Uchaguzi Bw. Julius Mh.Julius Mallaba.
Baadhi ya waadishi wa habari wakiwa katika kutano huo.
…………………………………………………………………………………………………..
Ndugu Waandishi wa Habari,
Mkurugenzi wa Uchaguzi,
Watendaji wa Tume,
Mabibi na Mabwana.
Kwa niaba ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisheni kwa mara nyingine
katika Mkutano huu. Nawashukuru kwamba, pamoja na majukumu mengi mliyo
nayo, mmeweza kuupa umuhimu wa pekee mkutano wetu huu na kuhudhuria kwa
wingi. Kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, nasema Ahsanteni na
Karibuni sana.
Katika mkutano huu, Tume inalenga
kutoa taarifa kuhusu tathmini ya utekelezaji wa zoezi la majaribio ya
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (Pilot Registration) kwa
mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR) zoezi ambalo lilikamilika
wiki iliyopita.
Ndugu Wanahabari,
Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imepewa jukumu la kisheria
Kuandikisha Wapiga Kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na
kuliboresha Daftari hilo kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani. Kwa mujibu wa Sheria ya Kura
ya Maoni, Daftari hili la Kudumu pia litatumika katika Kura ya Maoni
kuhusu Katiba Inayopendekezwa.
Ndugu Wanahabari; mtakumbuka kuwa,
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa katika mchakato wa Maandalizi ya
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia Teknolojia
Mpya ya ”Biometric Voter Registration” (BVR) na mara kwa mara imekuwa
ikiomba kukutana nanyi ili kuwapa taarifa kuhusu hatua mbalimbali ambazo
Tume imekuwa ikizipitia.
Kwa kuwa Uboreshaji huu ulihusisha
matumizi ya vifaa vya teknolojia ya kisasa, vifaa ambavyo vilikuwa
havijawahi kutumika katika Uboreshaji nchini, tuliona si vyema kuagiza
vifaa vingi kabla ya kuvifanyia majaribio. Zoezi la majaribio
lilifanyika ili kuwa na uhakika kuwa vifaa hivi vya Biometric
Registration vina uwezo wa kuandikisha Wapiga Kura katika mazingira ya
nchi yetu. Zoezi hili liliangalia uwezo wa watendaji kutumia BVR katika
uandikishaji na pia uwezo wa vyombo vyenyewe katika Software na Hardware
kwenye uandikishaji. Katika zoezi hili tuliangalia changamoto
zilizojitokeza ili kuzipatia ufumbuzi kabla ya kuanza Zoezi halisi la
Uandikishaji wa nchi nzima.
Ndugu Wanahabari,
Kama nilivyosema, Tume inakutana nanyi ili kuwapa taarifa kuhusu
Tathmini ya Utekelezaji wa zoezi la Majaribio la Uboreshaji wa Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika kwa siku saba (7) katika Kata za
Bunju na Mbweni katika Jimbo la Kawe, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar
es salaam; Kata za Ifakara, Kakingiuka, Ipangala, Mlabani na Viwanja
Sitini katika Jimbo la Kilombero Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero,
mkoani Morogoro; na Kata za Ikuba, Usevya na Kibaoni katika Jimbo la
Katavi, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi.
Tume kwa namna ya pekee,
inawashukuru sana Waandishi wa Habari kwa kujitokeza na kufuatilia zoezi
hili la majaribio ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Waandishi wa Habari wamesaidia sana katika kuhamasisha Wananchi wa
Majimbo husika kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura. Vilevile, Waandishi wa Habari wamesidia katika
kutoa taarifa za maendeleo ya zoezi hili kitu ambacho kimesaidia
kufanikisha zoezi hili.
Jumla ya BVR Kits 250 zilitumika
katika Uboreshaji huo kwa mgawanyo ufuatao:- Halmashauri ya Kilombero
BVR Kits 80, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele BVR Kits 80 na Halmashauri
ya Manispaa ya Kinondoni BVR Kits 90. Vituo katika Kata zote vilikuwa
vinafunguliwa saa 2.00 asubuhi na kufungwa saa 12.00 jioni.
No comments:
Post a Comment