Na Abdulla Ali-Maelezo Zanzibar
Chama cha mchezo wa mazoezi ya
viungo Zanzibar (ZABESA) kwa kushirikiana na Wizara ya Habari Utamaduni
Utalii na Michezo kimeandaa maadhimisho ya siku ya mazoezi ya kitaifa
yatakayofanyika Januari 1 mwaka 2015 katika uwanja wa Amani.
Maadhimisho hayo yatakayofanyika
majira ya Asubuhi yatahudhuriwa na watu mbalimbali ambapo Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Moh’d Shein
anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi.
Akizungumza na waandishi wa habari
katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Kikwajuni mjini Zanzibar, Katibu
mtendaji wa ZABESA Ameir Mohammed Makame amesema maadhimisho hayo
yatafuatiwa na matembezi yatakayoanzia Uwanja wa Tumbaku, Miembeni
kupitia Ng’ambu stesheni, Mfereji wa wima, Mikunguni na kumalizia uwanja
wa Amani.
Amesema lengo la maadhimisho hayo
ni kuwahamasisha wananchi kufanya mazoezi, kwani ni muhimu kwa mwanadamu
kimwili na kiakili na husaidia kuimarisha afya zao kwa ujumla.
Akitaja miongoni mwa faida hizo
katibu huyo amesema ni pamoja na kutanua mifumo ya mishipa ya damu,
kupunguza mafuta na sukari iliyozidi mwilini na kuimarisha misuli yote
ya mwili.
“Vyakula tunavyokula mara nyingi
vinakua havina ubora kwani vinakua na mafuta mengi na kemikali na
kusababisha matatizo mengi kiafya ikiwemo maradhi ya shindikizo la damu,
kensa, uzito uliokithiri na mengne mbalimbali” amesema Katibu Ameir.
Aidha alisema matumizi ya
teknolojia na kukua kwa uchumi kumesababisha watu kukaa kitako kwa muda
mrefu kuangalia television, kutopenda kutembea na matumizi holela ya
vyombo vya usafiri hupelekea kupata maradhi yasiyoambukiza kama vile
presha na kisukari.
Katika shamrashamra ya maadhimisho
hayo Vilabu vya mazoezi zaidi ya 70 kutoka Tanzania Bara na Visiwani
vinatarajiwa kuungana pamoja katika maadhimisho hayo.
Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed
Shein ameiasisi Januari mosi kuwa siku ya mazoezi ya kitaifa Zanzibar
ambapo Wananchi hujumuika na kufanya mazoezi mbalimbali ya Viungo
ikiwemo kutembea na kukimbia.
Kikundi cha ZABESA kilianzishwa
rasmi mwaka 2010 na kusajiliwa na mrajisi mkuu wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar ambapo ujumbe wa mwaka huu ni;“Fanya mazoezi, imarisha afya
yako na epuka maradhi yasiyo ya kuambukiza”.
No comments:
Post a Comment