Napenda nichukue fursa hii kutoa
ufafanuzi wa taharuki iliyotokea jana tarehe 02 Januari, 2015 katika
jiji la Dar es Salaam ikiwahusisha baadhi ya vijana wanaojikusanya
kwenye vikundi na kujiita Panya road na pengine kusababisha hofu kubwa
kwa wananchi.
Chanzo cha taharuki hiyo,
kulitokana na kuuawa kwa kijana mmoja ajulikanae kwa jina la Mohamed
Ayub na wananchi tarehe 01/01/2015 katika maeneo ya Tandale kwa Mtogole
kwa tuhuma za wizi wakati wa mkesha wa sikukuu ya mwaka mpya. Tarehe
02/01/2015 majira ya saa tisa mchana yalifanyika mazishi ya kijana huyo
katika makaburi ya Kihatu Kagera Mikoroshini na taarifa zilizokuwa
zimelifikia Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam ni kwamba baada ya
mazishi hayo vijana wenzake na marehemu walijipanga kufanya fujo ili
kulipiza kisasi cha mwenzao kuuawa. Aidha, kabla vurugu hizo
hazijafanyika na kwa vile Polisi walishaona dalili ya vurugu hizo,
tayari walifanikiwa kuzidhibiti.
Baada ya vurugu hizo kudhibitiwa
na Polisi, vijana hao walitawanyika kwa kukimbia katika maeneo
mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kuzua taharuki kubwa kwa wananchi
kwamba huenda kila walipokimbilia wanampango wa kuwafanyia fujo raia
wema, jambo ambalo wasingeweza kulifanya kwa vile Polisi walikuwa
wameimarisha ulinzi katika maeneo yote ya jiji.
Kufuatia hali hiyo na Jeshi la
Polisi nchini likiwa linaendelea na msako mkali wa kuwabaini na
kuwakamata wote wanaojihusisha na uhalifu huo, tunawaomba wananchi
watulie, wasiwe na hofu na waendelee na majukumu yao kama kawaida. Mpaka
sasa tunawashikilia watuhumiwa 36 kwa mahojiano na uchunguzi
utakapokamilika tutawafikisha mahakamani mara moja.
Aidha, Jeshi la Polisi linatoa
onyo kwa vijana hao wananojihusisha na vikundi hivyo kuacha tabia hiyo
mara moja. Tumejipanga vizuri katika mikoa yote kuhakikisha kwamba nchi
inaongozwa kwa kufuata utawala wa sheria, hatutamwonea muhali mtu yeyote
ama kikundi cha watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi na kutia hofu
wananchi.
Wananchi waendelee kutupa
ushirikiano kwa kutoa taarifa kupitia namba ya simu 0754 78 55 57, namba
za makamanda au katika kituo chochote cha Polisi.
Imetolewa na:-
Advera John Bulimba – SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
No comments:
Post a Comment