Katika
gazeti la NIPASHE la Jumatatu tarehe 08 Desemba, 2014 ziliandikwa
habari kuhusu Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (Mb)
chini ya kichwa cha habari “Wanaomtetea Muhongo Wajibu haya”. Hoja
zilizotolewa katika gazeti hilo zililenga kupotosha ukweli. Wizara
inapenda kutoa maelezo kuhusu hoja zilizotolewa kama ifuatavyo:
Utendaji wa Wizara chini ya Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (Mb)
Taarifa
za gazeti hilo zilieleza kuwa utendaji wa Wizara ya Nishati na Madini
hasa katika uongozi wa Waziri Muhongo umekuwa ni wa kukatisha tamaa.
Moja ya mifano iliyotolewa ni kuendelea kuwepo kwa wachimbaji madini
wanaozidi kutorosha madini kwa nia ya kukwepa kodi. Hoja hii haina
ukweli wowote kwani chini ya uongozi wa Waziri wa Nishati na Madini,
Prof. Sospeter Muhongo (Mb) utendaji wa Wizara umeimarika kwa kiasi
kikubwa. Chini ya Uongozi wake kumekuwepo na uwajibikaji mkubwa kwa
watumishi wa wizara ili kuhakikisha kuwa wanawatumikia wananchi
ipasavyo. Ni katika kipindi chake kumekuwepo na uanzishwaji wa madawati
ya ukaguzi wa madini katika viwanja vikubwa vya ndege vya JNIA, KIA na
Mwanza chini ya Wakala wa Ukaguzi wa madini (TMAA) ili kudhiditi
wachimbaji madini na watu wengine wenye nia ya kutorosha madini nje ya
nchi bila kuzingatia sheria. Kutokana na hatua hiyo madini mbalimbali
yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 15 yameweza kukamatwa. Madini
yaliyokatwa bila kuwa na vibali halali yametaifishwa na Serikali.
Serikali ilianza kuuza baadhi ya madini yaliyokamatwa kwa njia ya mnada
kwenye Maonyesho ya Vito yaliyofanyika Mjini Arusha kuanzia tarehe 18 –
20 Novemba, 2014. Katika mnada huo jumla ya zaidi ya shilingi milioni 70
zilipatikana na kuingia Serikalini. Serikali itaendelea kupiga mnada
madini mengine yaliyokamatwa kwa manufaa ya taifa. Wizara inaendelea
kuimarisha udhibiti ili kuhakikisha kuwa mtu yeyote anayekusudia
kutorosha madini anakamatwa na kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na
madini yake kutaifishwa na Serikali. Katika kusimamia sheria na
taratibu, chini ya Uongozi wa Prof.Muhongo, Wizara imedhibiti tabia ya
kuchukua vitalu vya madini na kuhodhi ili wale tu wanaozingatia masharti
ya leseni ndio waendelee kuvifanyia kazi vitalu. Hili limewaumiza
waliokuwa na tabia hiyo ambao kimsingi walikuwa wanavunja sheria. Baadhi
ya vitalu vilivyopokonywa vimekuwa vikigawiwa kwa wachimbaji
wadogo.Hivyo, si kweli kwamba utendaji wa Wizara ya Nishati na Madini
chini ya Prof. Sospeter Muhongo (Mb) ni wa kukatisha tamaa katika
kudhibiti utoroshaji wa madini nje ya nchi na katika ukiukwaji wa
masharti ya leseni mbalimbali za madini kama ilivyodaiwa.
Upitiaji Mikataba ya Madini
Taarifa
za gazeti hilo la NIPASHE la Jumatatu tarehe 08 Desemba, 2014 zilieleza
kuwa chini ya Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (Mb)
Serikali imeshindwa kupitia mikataba ya madini ili taifa linufaike
zaidi. Taarifa hizo si za kweli zinalenga kupotosha umma.
Ukweli
ni kuwa chini ya Uongozi wa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter
Muhongo (Mb), Wizara imepitia mikataba ya madini kwa kufanya
majadiliano na Kampuni za uchimbaji madini zenye mikataba ili
kurekebisha vipengele vya mikataba ambavyo vinalenga kuleta manufaa
zaidi kwa Taifa. Kazi hiyo imefanyika kwa Kampuni zote zenye mikataba na
tarehe 9 Oktoba, 2014 Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) imetiliana saini
mkataba wa kurekebisha vipengele katika mkataba uliosainiwa huko nyuma
baada ya majadiliano kukamilika. Aidha, majadiliano na Kampuni ya ACACIA
(zamani Kampuni ya African Barrick Gold –ABG) yamekamilika na
kilichobaki ni pande mbili (Serikali na Kampuni) kusaini marekebisho
yaliyofanyika kwa ajili ya mikataba ya migodi yake ya Bulyanhulu,
Buzwagi na North Mara.
- KUKATIKA KWA UMEME
Kukatika
kwa umeme kunasababishwa na kuzeeka kwa miundombinu ya usafirishaji na
usambazaji umeme. Ikumbukwe kuwa, kwa kipindi cha karibu miaka kumi
TANESCO iliwekwa chini ya PSRC kwa nia ya kubinafsishwa mwaka 1997 –
2007. Katika kipindi hiki TANESCO haikuruhusiwa kuwekeza wala kufanya
ukarabati wa miundombinu yake hivyo hali hiyo ilipelekea kuchakaa kwa
miundombinu hiyo ikiwemo mfumo wa usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Hata hivyo baada ya Serikali kubadili mtazamo wake wa kulibinafsisha
Shirika, TANESCO mipango kabambe ya kufanya ukarabati wa miundombinu
hiyo na kujenga mipya ili kuwa na mfumo wa usafirishaji na usambazaji
umeme ulio wa uhakika. Kazi hiyo inaendelea katika sehemu mbalimbali
nchini ikiwemo jiji la Dar es Salaam ambako kazi ya kukarabati na
kupanua miundombinu ya usambazaji umeme inaendelea. Aidha, TANESCO
ilishaelekezwa kutoa taarifa kwa umma kuhusu katizo lolote la umeme
lililopangwa kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya umeme. TANESCO
imekuwa ikifanya hivyo kwa kutumia vyombo vya habari vikiwemo
televisheni, radio na magazeti na pia kwa kutumia magari ya TANESCO
kufikisha taarifa kwa maeneo yanayoathirika. Kwa upande wa katizo la
umeme usiotarajiwa, TANESCO inacho kikosi cha dharura ambacho watumishi
wake wanafanya kazi masaa ishirini na nne kwa zamu ili kuhakikisha kuwa
hitilafu ndogondogo zinatatuliwa mara moja zinapojitokeza. Jamii ya
Watanzania wanalishuhudia hilo.
- DENI LA TANESCO LAPAA.
Mpaka
kufikia mwanzoni mwa mwaka 2014, deni la TANESCO lilikuwa limefikia
takribani Shilingi bilioni 695.30. TANESCO kwa kutumia vyanzo vyake vya
fedha kutokana na ukusunyaji wa maduhuli ndani ya kipindi cha miezi 11
imepunguza deni hilo mpaka kufika takribani Shilingi bilioni 355.11.
Kukua kwa deni la TANESCO kulisababishwa na hali ya ukame uliolikumba
taifa kuanzia miaka ya 2011 ambapo TANESCO ililazimika kununua umeme
aghali kutoka kwa wazalishaji wa umeme binafsi ikiwemo mitambo ya kukodi
ya dharura. Deni hilo lilikua kama ifuatavyo:
Mwaka Deni (Bilioni Sh.)
2011 538.47
2012 563.02
2013 695.30
2014 (9 Disemba) 355,11
TANESCO
imeongeza ufanisi wake katika kukusanya maduhuri na kufikia kiwango cha
asilimia 97 na fedha inayopatikana inatumika kupanua huduma ya umeme
nchini, kuendesha Shirika na kulipa madeni inayodaiwa.
Ukweli
ni kwamba deni la TANESCO limeshuka kwa kiasi kikubwa na kwa sasa
TANESCO imeweka mkakati maalumu wa kuwalipa wadeni wake wakubwa kiasi
cha Shilingi bilioni tatu kwa wiki kwa kila mdai, hivyo ni matarajio ya
Shirika kumaliza deni hilo mwaka kesho (2015).
- NCHI ITASONGA MBELE
Wazo
la kuanzishwa kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) lilibuniwa na
watumishi na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini mwaka 2005/6 chini
ya uongozi wa Nazir Karamagi akiwa Waziri wa Nishati na Madini. Taratibu
za kuanzishwa kwa REA zilikamilika mwaka 2007 ambapo REA ilianza
kutekeleza majukumu yake.
Mheshimiwa
Sospeter Muhongo baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini
ameisaidia REA kupata fedha kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo na
hivyo amesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kwa kasi ya kupeleka huduma
ya umeme vijijini.
Aidha,
Ili kufikia lengo la kuwaunganishia umeme asilimia 30 ya watanzania
ifikapo mwaka 2015, Chini ya uongozi wa Waziri Muhongo Serikali kupitia
TANESCO, ilipunguza gharama za kuunganisha umeme wa njia moja (single
phase) kwa wateja wadogo kwa wastani wa kati ya asilimia 30 na 77 kama
ifuatavyo:
-
Kwa wateja watakaojengewa njia moja (single phase) kwenye umbali usiozidi mita 30 bila kuhitaji nguzo, katika maeneo ya vijijini watalipa Shilingi 177,000 na wa mijini watalipa Shilingi 320,960 badala ya Shilingi 455,108 zinazolipwa na wateja hao kwa sasa.
-
Kwa wateja watakaojengewa njia moja (single phase) na kuwekewa nguzo moja, katika maeneo ya vijijini ni Shilingi 337,740 na wa mijini ni Shilingi 515,618 badala ya Shilingi 1,351,884 zinazolipwa na wateja hao kwa sasa.
-
Kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili katika maeneo ya vijijini ni Shilingi 454,654 na wa mijini ni Shilingi 696,670 badala ya Shilingi 2,001,422 zinazolipwa na wateja hao kwa sasa.
Kwa
ujumla katika kipindi hiki huduma ya umeme nchini imepanuka na kuwa
bora zaidi kuliko siku za nyuma. Ni matarajio ya Serikali kuwa huduma
hii itazidi kuwa bora zaidi katika siku chache zijazo kutokana na juhudi
kubwa zinazoendelea katika sekta ndogo ya umeme.
- DALALI WA FEDHA ZA ESCROW
Waziri
wa Nishati na Madini ndiye msimamizi mkuu wa masuala yanayohusu sekta
za Nishati na Madini nchini. Mtambo wa IPTL ulijengwa kwa ajili ya kufua
umeme unaotumiwa na jamii ya watanzania. Kuwepo kwa mgogoro kungeweza
kuondoa azma ya uwepo wa mtambo huo ya kufua umeme ili kuliepusha Taifa
kuingia katika mgawo wa umeme kutokana na upungufu wa upatikanaji wa
nishati hiyo, hivyo lilikuwa ni jukumu lake kuona kuwa mgogoro wa
wawekezaji wa mitambo ya IPTL unakwisha ili mitambo iendelee kutoa
huduma ya umeme kwa Taifa. Jukumu la Waziri ni kusimamia Sera, Sheria na
taratibu katika sekta anazozisimamia. Katika kufanya hivyo, Waziri
hukutana na wadau na kujadili masuala kwa uwazi bila kificho kwa nia ya
kujenga nchi na kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa ndiyo kipaumbele. Kwa
hiyo mikutano na Wadau ikiwa ni pamoja na wawekezaji hufanyika si kwa
udalali. Suala la fedha za akaunti ya Escrow lilihusu uamuzi wa mahakama
iliyojiridhisha kuwa mnunuzi wa hisa zote za VIP na MECHMAR ni halali
na alitakiwa kukabidhiwa mali na madeni ya IPTL. Mali ni pamoja na kiasi
cha fedha stahiki kwenye Akaunti ya Escrow ambazo hata hivyo
ilidhihirika kuwa hazitoshi kukidhi deni halali.
Akaunti
hiyo ilikuwa na Sh. 182 bilioni wakati malipo yaliyokubalika kwa pande
zote (IPTL na TANESCO) kwa mujibu wa maamuzi ya ICSID I yalikuwa Sh. 306
bilioni. Kumwita Waziri wa Nishati na Madini kuwa ni dalali ni
kupotosha ukweli.
No comments:
Post a Comment