BENKI ya Posta Tanzania (TPB),
Tawi la Tunduma imetoa mafunzo kwa wajasiriamali wa Tunduma, wilayani
Momba. Semina hiyo iliyohudhuriwa na wajasiriamali wapatao 100, ililenga
kuwaelimisha wafanyabiashara hao kuhusu matumiza mazuri ya huduma za
kibenki, hususan mikopo inayotolewa na benki hiyo.
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa
Wilaya ya Momba Abiudy Saideya, aliipongeza Benki ya Posta kwa kutoa
mafunzo ambayo alisema yanawasaidia wafanyabiashara wa Tunduma kukuza
uelewa wa matumizi sahihi ya huduma zinazotolewa na taasisi za fedha.
Aliwashauri wafanyabiashara
wachukue mikopo ili kukuza mitaji yao na kuongeza uzalishaji, lakini
bila kuwa na elimu sahihi juu ya matumizi ya mikopo hiyo faida yake
inaweza isipatikane. “Nawashauri wafanyabiashara mnaohudhuria semina hii
kutimia fursa hii kujadiliana na benki ya Posta ili mfikie muafaka
katika huduma mnazozitaka,” alisema Mkuu wa Wilaya hiyo.
Aidha aliwaasa wafanyabiashara
kujiepusha na biashara haramu zitokanazo na bidhaa haramu zilizozagaa
mpakani mwa wilaya yao, kwani kufanya hivyo bishara zao zinaweza
kutaifishwa na hivyo kupoteza mitaji yao bila kujua.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Mikopo wa Benki ya Posta, Henry Bwogi iliwasisitiza wafanyabiashara hao
kutembelea tawi la benki hiyo lililopo Tunduma ili kujipatia huduma zote
za kibenki hususan mikopo itakayowawezesha kukuza mitaji yao. Pamoja na
hayo aliongeza kuwa benki ya TPB inatoa mikopo ya aina nyingi, kuanzia
ile ya vikundi hadi ya wafanyabiashara wakubwa, huku riba zinazotozwa na
benki hiyo ni nafuu sana.
No comments:
Post a Comment