CHAMA cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kimewatimua wanachama wake 42 wakiwemo wagombea
walioshindwa kupita kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa hivi
karibuni.
Kwa mujibu wa taarifa ya
chama hicho, kutimuliwa kwa wanachama wake hao ni hatua ya chama hicho
kujisafisha kutokana na kile kinachodaiwa kwamba baadhi ya wagombea hao
wanatuhumiwa kufanya hujuma wakati wa mchakato wa uchaguzi serikali za
mitaa, vitongoji na vijiji uliofanyika Desemba 14, mwaka huu.
Akitangaza uamuzi huo
mjini humo, Katibu wa Chadema Jimbo la Korogwe Mjini, Ezekiel Mbwilo
alisema wahusika waliotimuliwa uanachama wanatuhumiwa kwa kukubali
vitisho na wengine kurubuniwa kwa fedha za wapinzani wao, hatua
iliyowalazimu kwenda kuondoa majina yao katika hatua za mwisho kuelekea
kwenye kinyang’anyiro hicho.
“Tuligundua kuwa baadhi
ya wahusiska walijihusisha na hujuma mbalimbali dhidi ya chama chetu,
ikiwamo kukubali kupewa fedha na wapinzani wao ili wajiondoe. Tangu
awali, tulishakubalina kwamba ikibainika watu waliofanya hujuma
tutawatimua kundini na hapa ndipo tunahitimisha lile tulilokubaliana,”
alisema.
Mbwilo alitaja maeneo
wanayotoka wanachama hao waliotimuliwa na idadi yao kwenye mabano ni
Kwamsisiwatu (6), Mahenge (10), Kitifu (25) pamoja na mmoja kutoka
Manundukati ambaye alidai kwamba mhusika huyo aliamua kujitoa kwenye
kinyang’anyiro cha uchaguzi ukiwa katika hatua za mwisho baada ya
kurubuniwa na wapinzani wa chama hicho.
Akizungumzia vitisho
alivyodai vilitolewa baadhi ya wanachama wa vyama vingine dhidi ya
wagombea wa Chadema, Mbwilo alisema tayari amewasilisha taarifa hizo
kwenye vyombo vya usalama na katika jeshi la Polisi kwa ajili ya
uchunguzi.
No comments:
Post a Comment