Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja akitoa hotuba yake
fupi katika Baraza la kufunga Mwaka 2014 na kuukaribisha Mwaka Mpya 2015
katika Ofisi za Makao Makuu ya Magereza(kulia) ni Kamishna wa Sheria na
Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(kushoto) ni Mnadhimu Mkuu wa
Jeshi la Magereza, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Magereza, Mmeta
Manyala. Baadhi
ya Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza kutoka Ofisi ya Makao Makuu
ya Magereza pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam wakisikiliza kwa makini
hotuba ya Kamishna Jenerali wa Magereza.
Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa akitoa
neno la shukrani kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir
Minja(katikati) mara baada ya kutoa hotuba fupi katika Baraza la kufunga
Mwaka 2014 na kuukaribisha Mwaka Mpya 2015.
Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza kutoka Ofisi ya Makao Makuu ya
Magereza pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa wamesimama kwa ajili ya
kuwakumbuka na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu Watumishi wenzao ambao
wametangulia mbele ya haki kwa mwaka huu 2014.
………………………………………………………………………………..
Na Inspekta Lucas Mboje, Jeshi la Magereza
Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja amewaasa
Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza nchini kuzingatia Sheria,
Kanuni, Taratibu na Miongozo katika utendaji wao wa kazi za kila siku
ili kuleta ufanisi kazini.
Kamishna Jenerali John Minja
ameyasema hayo leo wakati wa Baraza la Kufunga Mwaka 2014 na
kuukaribisha Mwaka 2015 lililowahusisha baadhi ya Maafisa na Askari
kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Magereza pamoja na Magereza Mkoa wa
D’Salaam.
Aidha, amewataka Maofisa, Askari
na Watumishi wote kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea bali wawe
wabunifu kwa kutumia raslimali zilizopo kwenye maeneo yao ya kazi ili
kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo.
” Kila mmoja wenu atimize wajibu
wake katika eneo lake la kazi kwa bidii, ari na moyo wa kujituma ili
kuliwezesha Jeshi kupata ufanisi unaotarajiwa”. Alisisitiza Jenerali
Minja.
Wakati huo huo Kamishna Jenerali
wa Magereza Nchini, John Casmir Minja pia ametumia fursa hiyo kuelezea
baadhi ya mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kwa Mwaka uliopita 2014
ambapo Jeshi la Magereza limepata jumla ya leseni 102 za uchimbaji wa
madini ya ujenzi kama vile chokaa, mawe, kokoto, mchanga na Murram
katika maeneo mbalimbali ya magereza ambayo ni Gereza Wazo Hill –
D’Salaam, Gereza Msalato – Dodoma, Kambi Bahi – Dodoma, Gereza Maweni –
Tanga, Gereza Lilungu – Mtwara, Gereza Butimba – Mwanza na Gereza
Kalilankulukulu – Katavi. Leseni hizo zitatumika kuingia ubia na
wawekezaji wenye nia ya kushirikiana na Jeshi katika uchimbaji wa
madini.
Pili, Shirika la Magereza
limeeingia Mkataba wa ubia na Kiwanda cha Saruji Wazo (Twiga Cement)
katika uchimbaji wa madini ya ujenzi Gereza Wazo Hill. Aidha, Kiwanda
hicho katika kutekeleza wajibu kwa jamii wametoa msaada wa mifuko ya
saruji 1200 na Tzs.100, 000, 000.00 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za
makazi ya askari Gereza Wazo Hill. Pia Shirika la Magereza limeingia
makubaliano na Mfuko wa Mafao ya Kustaafu wa GEPF kwa ajili ya ujenzi na
uendeshaji wa vituo vya biashara (business malls) kwenye maeneo ya
Gereza Kihonda, Morogoro na Gereza Karanga, Moshi.
Tatu, Rasimu ya kwanza ya Sera ya Taifa ya magereza imekamilika
na tayari imewasilishwa kwenye mamlaka za juu kwa hatua zaidi.
Kukamilika kwa sera hiyo kutawezesha Jeshi kutekeleza Mpango Mkakati wa
Sera na Maboresho ya Jeshi kwa ujumla.
Pamoja na Mafanikio hayo, Kamishna
Jenerali Minja ameelezea maeneo yatakayopewa kipaumbele kwa Mwaka huu
wa 2015 ikiwemo Jeshi litaendeleza jitihada za kuimarisha na kuongeza
uzalishaji kwenye miradi mbalimbali ya Jeshi la Magereza. Jitihada hizi
ni pamoja kutangaza fursa zilizopo ili kuwavutia wawekezaji mbalimbali
wa ndani na nje ya nchi waje kuingia ubia katika miradi hiyo kwa kuleta
mitaji na teknolojia, pia Kuendeleza mikakati ya kupunguza msongamano
magerezani
Baraza la kufunga Mwaka na
kuukaribisha Mwaka unaofuata ni utamaduni wa siku nyingi ambao unaenziwa
na Viongozi Wakuu wa Jeshi la Magereza. Baraza la aina hii hufanyika
kila Mwaka ambapo Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini hupata fursa ya
kuongea na Watumishi wote wa Jeshi la Magereza nchini kupitia Baraza
hilo lengo ikiwa ni kufanya tathmini ya yale yaliyojiri katika Jeshi kwa
kipindi cha Mwaka unaisha kwa kuzungumzia mafanikio na changamoto
zilizojitokeza na kutazama matarajio ya Mwaka mpya.
No comments:
Post a Comment