Kimsingi kuna
mamilioni ya wajasiriamali ulimwenguni ambao baadhi wamebainisha kwamba
vyanzo vikuu vya kupata wazo zuri la biashara ni kama ifuatavyo.
Kitu ukipendacho sana (hobby)
Mara nyingi
watu hupenda kutumia muda fulani katika siku ama wiki kujiburudisha na
vitu wavipendavyo mathalani kuchezea kompyuta, kupika, muziki, safari,
michezo, na kufanya mazoezi.
Kutokana na
kufanya jambo unalolipenda unaweza kuibua wazo la biashara, mathalani
kuna watu wanapenda kunywa vilevi na mwisho wa siku wananzisha biashara
ya baa.
Wengi wanafanya
hivyo kutokana na mtandao mkubwa waliojijengea na kufanikiwa kupata
wateja wengi na biashara kwenda vizuri. Kwa upande mwingine watu
wanaopenda muziki huweza kubadili mapenzi hayo ya muziki na kufanya
shughuli za kimuziki kibiashara.
Ujuzi na uzoefu
Tafiti nyingi
zinaonyesha biashara zilizofanikiwa zimetokana na ujuzi na uzoefu wa
mwanzilishi, mathalani mtu aliyeajiriwa kama mhasibu anaweza baadaye
akafungua biashara ya mambo ya ukaguzi wa mahesabu, daktari anaweza
kuanzisha biashara ya afya (kituo cha afya hadi hospitali) na askari
anaweza kufanya biashara ya ulinzi.
Kutokana na hali hiyo tunajifunza ujuzi na uzoefu unasaidia kuamua kuamua aina gani ya biashara ufanye.
Matumizi ya haki miliki
Kuna biashara
ambazo zinafanya vizuri sokoni na kwa kuwa zimesajiliwa kisheria
zinahaki miliki husika. Kwa mfano, wewe badala ya kufikiria kuanzisha
biashara gani unaweza kuingia mkataba na mmiliki wa biashara hiyo ili
uzalishe bidhaa ama utoe huduma kwa jina la biashara yake na kwa viwango
anavyotumia ilimradi ulipie gharama ya tozo kwa kutumia hati miliki
yake.
Vyombo vya habari
Vyombo vya
habari ni hanzo kikubwa sana cha habari na taarifa kinachoweza kukupa
wazo zuri na fursa mbalimbali za kibiashara. Vyombo vya habari vyaweza
kuhusisha magazeti, runinga na siku hizi mitandao ya kijamii.
Kwa mfano
unaweza kusoma au kuona habari kuhusu biashara fulani inauzwa na wewe
mara moja baada ya kuiona biashara hiyo unashawishika kuinunua. Habari
kwenye vyombo vya habari zinahusu mambo mengi ya kijamii, kisiasa,
kiuchumi na kiteknolojia, hivyo unapozipata ni rahisi kugundua fursa za
kibiashara.
Maonyesho
Maonyesho ya
kibiashara ni sehemu muhimu sana inayokutanisha wagavi, watengenezaji wa
bidhaa mbalimbali, wanunuzi na wasambazaji. Kuhudhuria maonyesho ya
biashara ambayo mara nyingi yanatangazwa kwenye vyombo vya habari
itakusaidia kujifunza mengi kutoka kwa watu wengine na kuvutiwa na
biashara ambayo unaweza kuifanya.
Tafiti
Tafiti ni suala
pana sana ila, unaweza kufanya kwa namna unavyoweza wewe, mathalani
unaweza kuwa na mawazo mengi ya biashara na hujafikia uamuzi wa biashara
ipi ufanye.
Kwanza unapaswa
kupanga mawazo ya biashara kuendana na kipaumbele na ukibakia na mawazo
matatu, jaribu kuuliza kuuliza watu mbalimbali wakiwamo wateja na watu
wanaofanya biashara kama hiyo. Kwa mfano zungumza na watu wanakwenda
safari ndefu kufuata bidhaa za majumbani kwa jumla, ni rahisi kwako
kuanzisha biashara ili uwapunguzie adha watu wa eneo hilo.
Malalamiko
Tumia
malalamiko kama njia ya kupata wazo la kuanzisha biashara mpya. Mara
nyingi tumekuwa tukishuhudia foleni kubwa kwenye benki, kucheleweshewa
mkopo, magari ya abiria kujaza sana na vikwazo vingine vingi, katika
hili pia unaweza kupunguza malalamiko hayo kwa kuanzisha biashara mpya.
Kwa mfano, nina
rafiki yangu alisajili kampuni ya kukopesha baada ya kucheleweshewa
mkopo benki kwa miezi sita. Kampuni yake inatoa mkopo ndani ya muda
mfupi sana ukilinganisha na benki.
No comments:
Post a Comment