LIGI KUU YA VODACOM YAINGIA RAUNDI YA 9.
Wakati raundi ya nane ya Ligi Kuu
ya Vodacom (VPL) inakamilika leo (Desemba 29 mwaka huu) kwa mechi tatu,
ligi hiyo itaingia raundi ya tisa Januari 3 mwakani kwa mechi tano.
Coastal Union itacheza na JKT Ruvu
katika Uwanja wa Mkwakwani, Ruvu Shooting itaikaribisha Kagera Sugar
kwenye Uwanja wa Mabatini, Azam itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika
Uwanja wa Azam Complex, Stand United itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro
kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati Mbeya City na Yanga zitaoneshana kazi
kwenye Uwanja wa Sokoine.
Ligi hiyo ambayo itachezwa
mfululizo (non-stop) hadi itakapomalizika Mei 9 mwakani, itakamilisha
raundi ya tisa Januari 4 mwakani kwa mechi kati ya Mgambo Shooting na
Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani, na Tanzania Prisons itakayokuwa
mwenyeji wa Ndanda kwenye Uwanja wa Sokoine.
Nayo mechi kati ya Mtibwa Sugar na
Stand United ambayo jana ilivunjwa na mvua dakika ya 6 imemaliziwa leo
ambapo timu hizo zimetoka sare ya bao 1-1.
Wakati huo huo, mechi ya ligi
iliyochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex imemalizika kwa
wageni Ruvu Shooting kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu.
Bao hilo lilifungwa kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penalti uliopigwa
na Hamisi Kasanga.
MBAO FC YAKAMATA USUKANI SDL
Timu ya Mbao FC ya Mwanza
imekamata uongozi wa Kundi B la michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL)
baada ya jana (Desemba 27 mwaka huu) kuizamisha JKT Rwamkoma ya Mara
mabao 2-1.
Kwa matokeo hayo katika mechi hiyo
iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mbao FC imeitoa kileleni JKT
Rwamkoma baada ya kufikisha pointi tisa kwa kushinda mechi zote tatu
dhidi ya Arusha FC, Pamba na JKT Rwamkoma.
Mbao FC inafuatiwa na JKT Rwamkoma
yenye pointi sita, Arusha FC pointi sita wakati Bulyanhulu na Pamba
zikiwa za mwisho kwa pointi moja kila moja. Kundi hilo litakamilisha
mzunguko wa kwanza Januari 3 mwakani kwa mechi kati ya JKT Rwamkoma na
Arusha FC, na Bulyanhulu na Mbao FC.
Katika kundi A, Mji Mkuu (CDA) na
Singida United ndizo zinazochuana kileleni kwa kufikisha pointi saba
kila moja. Timu hizo zinafuatiwa na Milambo yenye pointi nne, Mvuvumwa
FC yenye pointi moja wakati Ujenzi Rukwa ni ya mwisho ikiwa haina
pointi.
Hata hivyo, Mvuvumwa FC na Milambo
ziko nyuma kwa mechi moja. Mechi hiyo ya kukamilisha raundi ya tatu
kati ya timu hizo itachezwa kesho (Desemba 29 mwaka huu) kwenye Uwanja
wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Kiluvya United imeendelea
kuchachafya kundi C baada ya kushinda mechi zote ne ilizocheza, hivyo
kufikisha pointi 12. Inafuatiwa na Mshikamano yenye pointi saba huku
Abajalo ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi 6.
Nafasi ya nne inashikwa na Transit
Camp yenye pointi nne, Cosmopolitan yenye pointi mbili ni ya tano
wakati Kariakoo ambayo haina pointi ni ya mwisho. Hata hivyo,
Cosmopolitan na Kariakoo zina mchezo mmoja mkononi.
Mechi zinazofuata za kundi hilo ni
Januari 3 mwakani kati ya Kariakoo na Mshikamano na Mshikamano (Ilulu),
Transit Camp na Abajalo (Mabatini), na Cosmopolitan na Kiluvya
(Karume).
Kundi D, vinara bado ni Njombe Mji
yenye pointi 12 ikifuatiwa na Wenda yenye pointi sita wakati Volcano FC
iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi tano. Mkamba Rangers ina pointi nne,
Town Small Boys ina pointi moja wakati Magereza FC haina pointi.
Katika kundi hilo leo (Desemba 28
mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Town Small Boys na Magereza
itakayochezwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea. Januari 3 mwakani
kutakuwa na mechi kati ya Town Small Boys na Njombe Mji, Volcano FC na
Magereza, na Wenda na Mkamba Rangers.
No comments:
Post a Comment