MALINZI AZINDUA KAMPENI YA ISHI HURU
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amezindua
programu ya kutoa elimu ya kupambana na matumizi ya dawa za kulevya kwa
vijana iitwayo Ishi Huru.
Programu
hiyo iliyozimduliwa jana (Januari 10 mwaka huu) jijini Dar es Salaam
iko chini ya taasisi ya Africa Inside Out inayoongozwa na Rebecca Young
wakati washirika (partners) ni TFF na kampuni ya Rhino Resources ya
Marekani.
Rais
Malinzi amesema matumizi ya dawa za kulevya nchini yamekuwa
yakiongezeka, hivyo kuwa kikwazo kwa maendeleo ya vijana ambapo
ameipongeza Africa Inside Out kwa programu hiyo kwa vile itazuia vijana
wengi kujiingiza katika matumizi ya dawa hizo.
“Moja
athari kubwa za matumizi ya dawa za kulevya ni kupata maambukizi ya
virusi vya Ukimwi kutokana na kuchangia sindano za kujidunga dawa hizo.
“TFF
tutatoa ushirikiano wa kutosha katika programu hii. Lakini pia
tutaingiza Ishi Huru katika programu zetu za mpira wa miguu kwa vijana.
Tutahamasisha jamii katika kupambana na dawa za kulevya,” amesema.
Katika
uzinduzi huo, pia Rais Malinzi alizundua semina ya waelimishaji na
kuwaeleza kuwa wamepata fursa hiyo kwa vile ni vijana wanaojituma, hivyo
watafikisha vizuri ujumbe wa Ishi Huru katika shule na vituo vya vijana
nchini.
CAPTION:
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi
akizungumza kwenye uzinduzi wa programu ya Ishi Huru jijini Dar es
Salaam.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MTANGAZAJI SULTAN SIKILO
Shrikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha
mtangazaji wa michezo wa Radio Abood, Sultan Sikilo kilichotokea jana
alfajiri (Januari 11 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Sikilo
ambaye pia aliwahi kufanyia kazi Radio Times na Radio Kheri na hadi
umauti unamkuta alikuwa Mweka Hazina Msaidizi wa Chama cha Waandishi wa
habari za Michezo Tanzania (TASWA) amezikwa jana jioni katika makaburi
ya Kibada, Kigamboni.
Msiba
huo ni mkubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani kwa
nyakati tofauti Sikilo alifanya kazi na TFF kwa kuripoti shughuli zetu
nyingi za mpira wa miguu, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF
tunatoa pole kwa familia ya marehemu Sikilo, Radio Abood na TASWA na
kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha
msiba huo mzito. Pia TFF imetoa ubani wa sh. 100,000 kwa familia ya
marehemu kama rambirambi zake.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina
No comments:
Post a Comment