Balozi na wageni wote. Kwanza kabisa kulia ni Mkurugenzi wa Biashara Ubalozini, Yusuf Kashangwa- pic by Urban Pulse
Kocha wa Eton, Glen Pierce akizungumza- Pic by Urban Pulse Mkurugenzi wa Safari Hub, Dilip Navapurkar akizungumza
………………………………………………………….
Imeandikwa na Freddy Macha
Mradi
wa majaribio ya mwezi mmoja ulioandaliwa na Waingereza kuendeleza shule
sita wilaya za Arusha na Moshi unatazamiwa kuanza wiki hii, ilitangazwa
London, mwishoni mwa juma.
Mradi
huu unaosimamiwa na kampuni ya kitalii, Safari Hub na Chuo cha Eton
wakisaidiana na Ubalozi wa Tanzania, Uingereza, unatuma Mkuu wa Mafunzo
ya Michezo Eton, Bwana Glen Pierce na wanafunzi watatu waliomaliza
kidato cha sita wanaotarajia kuingia vyuo vikuu baadaye mwakani.
Nchini
shughuli hii itasaidiwa na ushirikiano wa chuo cha michezo Arusha
(Future Stars Academy) na shirika la ufadhili linalopigana kuondoa
umaskini, (ACE Africa).
Akiongea
katika tafrija ndogo iliyofanywa Ubalozini, London kuuaga msafara ,
Mkurugenzi Mkuu wa Safari Hub, bwana Dilip Navapurkar alisema iko haja
ya kujenga ujuzi toka utotoni ili “kuhakikisha timu ya taifa ya Tanzania
inafanya vizuri katika michuano ya Kombe la Afrika na Dunia na kufikia
kiwango cha mafanikio tunayoyaona nchi nyingine mathalan Nigeria, Ghana,
Afrika Kusini na Ivort Coast.”
Mwalimu
Pierce mwenye uzoefu wa Miaka 27 chuo cha Eton aliwafundisha pia
wajukuu wa Malkia Uingereza, William na Harry. Wanafunzi atakaoongozana
nao ni Tom Pearson, 18 ( ulinzi) Nicholas Zafiriou, 18 (kiungo) na Ali
Lyon, 19 (mshambuliaji ). Wamechaguliwa kwa kufanya vizuri katika
michezo mbalimbali ukiwemo mpira waliocheza timu ya shule ya Eton.
Eton
ilianzishwa karne ya 15 na Mfalme Henry wa 6 na ni moja ya shule bora
sana duniani. Mawaziri Wakuu 19 wa Uingereza (akiwemo Winston Churchill,
Tony Blair, David Cameron na Meya wa Jiji la London, Boris Johnson)
walisoma hapa. Wabunge, mawaziri, waandishi maarufu (George Orwell na
Ian Fleming mtunzi wa visa vya James Bond) na watoto wa wafalme
mbalimbali duniani vile vile wamesoma
Eton.
Tafrija ya kuwaaga ilifanywa na Balozi Peter Kallaghe na Afisa
Balozi, Amos Msanjila aliyewakaribisha Tanzania. Mbali na kutoa mafunzo
ya michezo wageni wanatazamiwa kukutana na wanahabari Jumanne,
kutembelea mbuga za wanyama, Zanzibar na kupanda mlima Meru, Arusha.
Lengo
la mradi huu ni safari au mradi mfupi na hatimaye kuendeleza mahusiano
kati ya wanafunzi wa Tanzania na Eton. Iko siku “timu ya mpira ya Eton
itafanya ziara Tanzania na hatimaye Watanzania pia kuitembelea Eton,”
Bwana Navapurkar alisema.
Akihimiza
umuhimu wa safari hii, Balozi Kallaghe aliwaambia wageni kwamba
Watanzania wanapenda sana soka na kuwaahidi wageni kuwa watafaidi uzuri
wa nchi watakapofika kama sehemu ya mafanikio ya kibiashara siku za
mbeleni na kufurahia michezo Tanzania.
Akijibu
maswali ya wanahabari, Bwana Navapurkar alisema gharama za safari na
vifaa vimetokana na michango ya watu binafsi na shule zinazopakana na
Eton ambazo zimefikia shilingi milioni 61 na nusu.
Mbali
na mafunzo ya mpira wanafunzi Arusha na Moshi watapewa vifaa na
kufundishwa maana ya nidhamu, elimu na michezo, aliongeza kocha Glen
Pierce. “Watoto watakaopewa fursa hiyo ni wale tu watakaohudhuria
shule,” alisisitiza.
Akisifia
tabia ya Watanzania, Mkurugenzi wa Safari Hub, yenye makao Tanzania,
Bwana Navapurkar, alisema Tanzania imechaguliwa shauri ni nchi yenye
amani, demokrasia na utulivu wa kisiasa, ukilinganisha na nchi nyingine
za Kiafrika. “Tanzania ni kito cha maendeleo ya Afrika.” Alisema.
No comments:
Post a Comment