Asteria Muhozya ( Mtwara, Lindi na Kilwa)
Kusudi la Wizara ya
Nishati na Madini kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wa dini
katika sekta za gesi na mafuta kwa manufaa ya Watanzania limefikiwa.
Akizungumza baada ya
ziara ya kutembelea Bomba Jipya la gesi asilia Mtwara- Dar es Salaam,
Mtambo wa kusafisha umeme wa Mnazi Bay, na maeneo mbalimbali ya
uendelezaji wa gesi asilia katika Mkoa wa Mtwara na Lindi, Katibu wa
Jumuiya ya Kikrsito Tanzania (CCT) na Mwenyekiti wa Sekretariati ya
kongamano la viongozi wa dini Bw. John Mapesa, alieleza kuwa, viongozi
wa dini wamepata elimu sahihi ambayo hawakuifahamu kabla kuhusu sekta
hizo.
Aliongeza kuwa,
viongozi hao wamekuwa wakipata habari ambazo si sahihi kuhusu rasilimali
hizo lakini baada ya kutembelea, kujifunza, kuona na kusikia kutoka kwa
watalaamu mbalimbali kuhusu namna miradi hiyo inavyofanyika,
wanatarajia kuwa walimu kwa watanzania wengine ili kuwa na uelewa wa
pamoja.
“Sisi tuna nafasi
kubwa sana ya kukutana na wananchi kutoa elimu, kwani wanatuamini na
wanatusikiliza kwa kwasababu tunawasaidia kiroho. Wizara imefanya sehemu
yake na sisi tunayo sehemu yetu ya kuwafikia kupitia umoja wetu”. Alisema.
Aliongeza kuwa,
viongozi wa dini ni sehemu ya jamii na wanaposhirikishwa kwa kuelezwa
mipango mbalimbali ya Serikali ni jambo la muhimu kwasababu wanayo
nafasi ya moja kwa moja ya kuwasiliana na wananchi ikiwemo kushauri.
Hivyo, elimu waliyoipata na taarifa walizozipata zitakuwa na mchango
katika kuleta amani na ustawi wa jamii wakati huu ambapo nchi inaelekea
katika kupokea uchumi mkubwa kupitia rasilimali hizo.
“Nawaambia Watanzania wenzangu tushiriki kikamilifu katika uchumi huu wa gesi na mafuta kila mmoja kwa namna yake kwani
kuna mafanikio makubwa sana yanakuja. Kuna fursa nyingi na Mwenyezi
Mungu hawezi kuleta baraka kwa ajili ya kutuangamiza, analeta kutuletea
furaha ili tufaidike. Juhudi za Serikali kuhakikisha kila mmoja
anafaidika tumeziona”. Alisema.
Kwa upande wake Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini aliyeongoza ujumbe huo,
Mhandisi Ngosi Mwihava alisema kuwa, kufuatia ziara hiyo ya viongozi wa
dini, inaonesha kuwa serikali ni sikivu na inasikiliza matarajio ya
wananchi.
“Tuliona kuwa kuna
uelewa tofauti tofauti katika rasilimali hizi, viongozi waliomba
tuwaelimishe na sisi tumefanya hivyo kwasababu tunajua wanayo nafasi
kubwa ya kuwafikia wananchi na wana mchango mkubwa katika kufikia
maendeleo tunayoyatarajia”. Alisema Naibu Katibu Mkuu.
Aliongeza kuwa, lengo
kubwa la ziara hiyo ya viongozi wa dini ni kutaka kuweka uelewa wa
pamoja kuhusu rasilimali hizo kwa makundi mbalimbali yenye uwakilishi
Kitaifa hali ambayo itasaidia kufahamu fursa zilizopo, mipango ya
serikali na kila mmoja kwa nafasi yake ajue namna fursa zilizopo katika
sekta hiyo zitakavyotumiwa.
“Katika mchakato wa
maendeleo, kuna wadau wengi, hivyo mwanya upo kwa wadau kuchangia katika
uwekezaji inaweza kuwa kuwekeza kwa kushirikiana na serikali au kufanya
binafsi”. Alisema Naibu Katibu Mkuu.
Aliongeza kuwa,
anaamini ziara hiyo imetoa mwanga kwa viongozi wa dini katika kuelekea
kwenye kongamano la kujadili rasilimali hizo na namna
zitakavyowanufaisha watanzania.
Kwa upande wake Mkuu
wa Mkoa wa Mtwara Kanali Mstaafu Mhe. Joseph Simbakalia aliwataka
viongozi hao kuwasaidia wananchi kuyaweka matarajio ya uchumi huo kwenye kiwango halisi kwa
kuzingatia kwamba, uchumi wa gesi ni sekta mpya Tanzania na hivyo,
maandalizi yakutosha yanahitajika ikiwemo kujifunza kwa usahihi kutokana
na ukweli kwamba biashara hiyo ni ghali.
“Mmefanya vizuri sana
kuja, kawaambieni vijana na wananchi wajiandae kujua watafanya nini
katika uchumi huu kuanzia kwenye elimu na uwekezaji ili tufike
tunakotaka kwenda. Msipofanya hivyo, hatutakwenda vizuri”. Alisema
Simbakalia.
Wakati huo huo Mkuu
wa Mkoa wa Lindi Mhe. Ludovick Mwananzila aliwataka viongozi hao
kuwaelimisha wananchi ukweli kuhusu gesi kusafirishwa kwenda Dar es
Salaam, ugunduzi wake na manufaa yake kwa Taifa kwasababu wamepata
nafasi ya kuona yale yanayofanyika na kusikia mipango mbalimbali.
“ Waelimisheni
ukweli, Dar es Salaam ndio kuna viwanda vingi vya uzalishaji tofauti na
Lindi na Mtwara, lakini haimanishi kwamba Mikoa hii itabaki bila
manufaa, tuna kiwanda cha sementi kinatarajiwa kujengwa hapa Lindi
tunatarajia kitatoa fursa nyingi, si hilo tu, tuna mipango mingi ya
kuhakikisha kuwa wananchi wote wananufaika”. Alisema.
Aidha, aliwataka viongozi hao kuwaelimisha
wananchi kuacha kuchukua mifano ya nchi ambazo hazikujiandaa katika
uchumi wa gesi na kuongeza kuwa, ni elimu pekee ndio itasaidia kuleta
mabadiliko kwa wananchi.
“Kilwa kwa mfano,
katika kijiji cha Songosongo wanapata si chini ya milioni 20 kwa mwezi
kutokana na faida za gesi, wanapata umeme bure, maji bure, sasa katika
hayo vurugu za nini? Alisema Mkuu wa Mkoa.
Naye Mkuu wa Wilaya
ya Kilwa Mhe. Abdalah Ulega aliutaka ujumbe huo kuwaeleza wananchi kuwa,
mafanikio katika sekta ya gesi yapo na wananchi wameanza kufaidika
nayo.
No comments:
Post a Comment