Na Asteria Muhozya, Arusha.
Mkurugenzi Mkuu wa Nishati katika Wizara ya Nishati naMigodi
wa Algeria Bw. Bourraondj Mohamed Tawar amesema, Serikali ya Algeria
imejifunza mambo mengi katika sekta ya madini, kufuatia ziara yao nchini
Tanzania.
Aliyasema
hayo jana wakati wakihitimisha ziara yao nchini kwa kutembelea maeneo
mbalimbali ikiwemo ya uchimbaji na uzalishaji wa madini ya Tanzanite
katika migodi ya TanzaniteOne Mererani na katika kiwanda cha kuzalisha
mbolea ya kupanda ya Minjingu, Mkoani Arusha.
Aliongeza
kuwa, ziara hiyo imekuwa ya manufaa kwa Serikali yao kutokana na kwamba
pamoja na kufanikiwa katika sekta ya gesi lakini wamejifunza mengi
katika sekta ya madini na katika mbolea ya kupandia ya Minjingu, hatua
ambayo imewawezesha kujifunza na kuona namna serikali ya Tanzania
inavyoshughulikia sekta hizo kuanzia uchimbaji, teknolojia zinazotumika,
uuzaji, na mambo yote yanayohusu sekta hizo.
Aidha,
alieleza kuwa, wamekutana na mambo mengi mapya likiwemo la uchimbaji wa
mbolea ya kupandia ya minjingu inayochimbwa kutokana na masalia ya
ndege aina ya flamingo ambayo masalia yake yamekuwepo kwa miaka mingi.
“Nilikuwa
nikisoma tu katika vitabu lakini sasa nimeona mwenyewe kwa macho, ni
furaha sana na funzo kwetu, kwasababu tunatumia njia nyingine kuzalisha
mbolea ya kupandia na si kama hii ya masalia ya ndege aina ya flamingo
inayotumiwa na Tanzania”, Alisema.
Aidha,
aliongeza kuwa, anaamini kuwa ushirikiano ulioanzishwa na nchi hizi
mbili utakuwa wa manufaa kwa nchi zote na kuongeza kuwa, anaamini kuwa,
ushirikiano huo utaharakishwa ili utekelezaji wake uanze haraka.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha kuzalisha mbolea ya
Minjingu Bw. Tosky Hans alisema kuwa, ziara hiyo ya wataalamu hao
kutoka Algeria ni mafanikio kwao kwasababu ushirikiano huo utasaidia
kujifunza mambo mengi kutoka Algeria ambao wamepiga hatua kubwa
kiteknolojia na kitaaluma
“Tutaangalia
upande wa teknolojia wanatumia nini na kuzalisha nini, kwasabababu nia
yetu ni kuongeza uzalishaji, kuwafikia wananchi wengi zaidi na kukidhi
mahitaji ya mbolea kwa nchi za Afrika Mashariki”. Alisema Hans.
Akielezea
kuhusu kupata fursa ya kutembelea katika mbuga za wanyama katika bonde
la Ngorongoro Bw. Bourraondj Mohamed Tawar alisema, imekuwa ni furaha
kwao kuona makundi makubwa ya wanyama mbalimbali na ndege katika mbuga
hizo wakiwemo simba ambao walipata nafasi ya kuwaona vizuri.
Vilevile,
alieleza kufurahishwa kwao kufika katika eneo la boma wanapoishi
Watanzania jamii ya Maasai ambapo walishangazwa kuona namna Maasai hao
wanavyoishi jirani na wanyama wa porini.
Wakati
huo huo, Kamishna Msaidizi kanda ya Kaskazini Mhandisi Bw. Benjamini
Mchwampaka anayesimamia shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini
amewataka wachimbaji na wamiliki wa migodi kufuata sheria na taratibu za
leseni ikiwemo kulipa kodi. Aliongeza kuwa, serikali haina ubaguzi kwa
wachimbaji wakubwa au wadogo wote wanapewa fursa sawa.
“Tunawaangalia wachimbaji wote kwa usawa, wafuate sheria, wachimbe kwenye maeneo yao bila kuingiliana”. Alisema Mchwampaka.
Vilevile,
aliwataka wachimbaji kuwa wazalendo kwa kulipa kodi Kama inavyowapasa
bila kufuatiliwa na maafisa madini na kuwataka wakumbuke kuwa, Tanzania
itajengwa na watanzania wenyewe pale wanapotimiza wajibu wao kikamilifu.
No comments:
Post a Comment