
            
Baadhi ya wanawake wa Zanzibar wakiwa kwenye mkutano wa kujitambua.Picha na Salma Said.
    Na:Salma Said, Mwananchi
- Sauti za wanawake hapa Zanzibar ni kama mti ulioanguka mwituni huku kukiwa hakuna mtu aliyesikia au kuona kama unaanguka. Wanawake bado wanaonekana kama ni chombo cha starehe tu, wengine wanawachukulia wanawake kuwa ni sawa na bidhaa mbovu.
 
Wanawake wanachukuliwa kama ni watu wa kubaki 
katika ndoa kutii amri za mume hata kama amri hizo siyo za haki, heshima
 au zinavunja utu wa mwanadamu.
Kwa mfano, gwiji la fasahi ya Kiswahili, marehemu 
Sheikh Shabaan Robert katika kitabu chake “Maisha yangu na baada ya 
miaka hamsini” katika ukurasa wa kumi anatoa wasia kwa bintiye kwa 
kumwambia;
“Fanya kila hali, la mume kulikubali, ila lisilo 
halali, kukataa si hatia” Hapa anampa ujasiri mwanawe wa kike kutokubali
 mambo ya ovyo kutoka kwa mume, ana mjengea uwezo wa kuwa mwanamke na 
mama shupavu katika maisha ya ndoa yake na kuweza kukabiliana na 
familia.
Matukio ya kutendewa isivyo wanawake siyo mageni, 
wanawake wamekuwa wakipata vipigo, kuteswa na wengine kufikia hata 
kujeruhiwa hapa Zanzibar.
Wanawake Zanzibar wamekuwa wakifanya kazi ngumu, 
wana mzigo wa kuhudumia familia, wanafanya biashara, wanafanya kazi 
ofisini huku wakisubiriwa kupika, kuchota maji, wanabeba mimba na 
kujifungua na wakati mwingine hata hayo matunzo ya mama mjamzito 
hayapati hasa wanawake wa vijijini.
Katika sehemu za mashamba Unguja na Pemba, 
wanawake wanalima, wanapanda, wanapalilia, wanachuma karafuu huku 
wengine wakianguka na wasipofikisha vyakula vinavyotakiwa, anapata 
matusi na hatimaye kuambulia kipigo.
Katika utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi 
wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) katika Wilaya ya Mjini, Mkoa wa 
Mjini Magharibi Unguja, kati ya Novemba hadi Desemba mwaka jana, 
Zanzibar kuna matukio kadhaa ya wanawake kupata vipigo kutoka kwa waume 
zao.
Ijapokuwa TAMWA katika utafiti huo wanasema kwamba
 hulka ya kuwapiga wanawake siyo matukio maarufu sana, ukweli ni kwamba 
wanawake wengi wa Zanzibar ni wasiri mno, hata akipigwa au kuteswa hawi 
wazi kutangaza.
Mathalan mmoja ya wanawake aliyehojiwa Mtaa wa 
Kwamtipura, analalamikia hulka ya mumewe ya kumpiga mara kwa mara hasa 
pale anapodai huduma muhimu kama chakula na ikiwa akimweleza upungufu 
basi inakuwa nongwa na sababu ya kuanza kupokea vipigo!
Mwanamke huyu hivi karibuni alipokea kipigo pale 
aliposema kiwango cha chakula alichoachiwa ni kidogo na hakiwezi 
kumtosha, ndipo mume wake alianza kumfokea kwa maneno machafu na kuanza 
kumpiga jambo ambalo lilimfanya mwanamke huyo kukimbilia kwa Sheha 
Machano Khamis kwenda kujisalimisha.
Wanawake wanaopata vipigo kwa hakika ni wengi, 
lakini wamekuwa wakitofautiana kutokana na sehemu hadi sehemu. Wapo 
wanaopigwa kwa madai ya kudai haki za msingi za mke ikiwamo kupatiwa 
huduma za mahitaji ya chakula, mavazi na hata kufanya kazi.
Miongoni mwa sababu za kushamiri kwa vitendo vya 
kupigwa wanawake na waume zao ni pamoja na wivu wa mapenzi, ulevi, 
kugombania watoto na mali na kuporomoka kwa maadili katika jamii.
No comments:
Post a Comment