TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Tuesday, January 28, 2014

Zabuni ya vitalu vya gesi kufungwa mwezi Mei

Na: Teresia Mhagama, Nishati na Madini

 
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameeleza kuwa zabuni ya vitalu vya utafiti wa mafuta na gesi asilia vilivyo bahari kuu na ziwa Tanganyika kaskazini itafungwa tarehe 15 mwezi wa tano mwaka huu.

Waziri Muhongo alisema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Waziri mstaafu wa Nishati na Viwanda kutoka nchini ufaransa Bw.Erick Besson aliyemtembelea wizarani ili kufahamu fursa za uwekezaji zilizo katika sekta za Nishati na Madini akiiwakilisha kampuni ya GDF Suez ya Ufaransa.

“Kampuni unayoiwakilisha ni kubwa, yenye teknolojia ya kisasa na inafanya uwekezaji mkubwa duniani hivyo kama mna nia ya kuwekeza katika uendelezaji wa vitalu vya gesi mnaweza kuingia katika ushindani wa kumiliki vitalu hivyo kwani muda bado unaruhusu”. Alisema Profesa Muhongo.

Waziri Muhongo alimweleza Bw. Besson kwamba Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) linamiliki vitalu viwili vya gesi karibu na mpaka wa Msumbiji lakini linahitaji mbia mwenye nia ya dhati watakayeshirikiana naye katika hatua zote za uendelezaji wa vitalu, kwa sababu TPDC bado inakua, alitoa changamoto kwa kampuni hiyo ya GDF Suez kuingia katika ushindani huo.

Katika suala la usimamizi wa bomba la gesi asilia, Profesa Muhongo alimweleza Bw. Besson kuwa TPDC pia itahitaji kupata uzoefu na pengine mbia aliyebobea katika usimamizi wa bomba hilo atakayeshirikiana na TPDC katika usimamizi wa bomba la gesi nchini.
  
Profesa Muhongo alisema Serikali itasambaza gesi katika makazi ya watu ili kupunguza uharibifu wa mazingira huku akitoa mfano kuwa jiji la Dar es Salaam pekee linatumia si chini ya magunia 50 ya mkaa kwa siku hivyo gesi itapunguza uharibifu wa mazingira.

Alisema huo ni mpango endelevu kwani tayari kuna bomba la urefu wa la 6.3 kilometa kutoka Ubungo hadi Mikocheni linalotoa gesi majumbani na bei yake haizidi shilingi 12,500 kwa mwezi.

Alisema kuwa TPDC itahitaji mbia katika utekelezaji wa mpango huo wa usambazaji gesi majumbani na katika sehemu ambazo bomba la gesi haliwezi kupita kutahitajika mitungi ya gesi ili wananchi wote wafaidi gesi hiyo.

Kuhusu umeme, Waziri Muhongo alimweleza Waziri mstaafu huyo wa Ufaransa kwamba serikali inajikita katika miradi ya usambazaji umeme kwa utaratibu wa ubia au mikopo ya bei nafuu na ina mpango wa kujenga njia ya umeme ya msongo wa 400kv kuelekea ziwa Tanganyika hivyo aliikaribisha kampuni ya GD Suez kuwekeza katika miradi hiyo ya usambazaji umeme.

“Tunatafuta pia wawekezaji katika suala la usambazaji umeme na ujengaji wa vituo vya kupooza umeme na transfoma kubwa kwani tumeamua kufanya uwekezaji mkubwa katika eneo hili mf. jijini Dar es Salaam  tulikuwa na vituo vitano tu vya kupoozea umeme lakini sasa tunajenga vingine vitano vikubwa na vidogo 15 ili kutatua tatizo la umeme jijini Dar es Salaam hivyo unakaribishwa kuwekeza katika eneo hili pia”. Alisema Profesa Muhongo

Aidha Profesa Muhongo alimweleza Bw. Besson kuwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linatafuta mbia watakayeshirikiana naye katika kuendesha mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe Kiwira mkoani Mbeya hivyo kama wana nia ya kuwekeza katika eneo hilo pia wanakaribishwa kuingia katika ushindani wa kupata nafasi hiyo.

Naye Waziri mstaafu wa Viwanda na Nishati kutoka nchini Ufaransa, Bw. Besson alimshukuru Profesa Muhongo kwa  taarifa nzuri kuhusu fursa za uwekezaji nchini na ameahidi kupata taarifa zaidi za uwekezaji katika mashirika ya TPDC, STAMICO na TANESCO ili kuona jinsi kampuni ya Suez itakavyoshirikiana na mashirika hayo katika kuendeleza sekta za Nishati na Madini.
PICHANI JUU: 

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akiwa pamoja na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Marcel Escure (kulia kwa Waziri) pamoja na Waziri Mstaafu wa Viwanda na Nishati wa Ufaransa Bw. Eric Besson (kulia kwa Balozi),  pamoja na watendaji kutoka Ubalozi wa Ufaransa na Wizara ya Nishati na Madini, wakati walipomtembelea wizarani ili kufahamu fursa za uwekezaji katika sekta za Nishati na Madini..

No comments:

Post a Comment