Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi akijibu swali la mbunge Bungeni Dodoma.
…………………………………………………………………………..
Hussein Makame-MAELEZO, Dodoma
BUNGE limeridhishwa na hali ya ulinzi wa nchi, usalama wa raia
na mali zao kwa kipindi cha mwezi Februari mwaka 2014 hadi Januari mwaka
huu kutokana na hali ya ulinzi wa nchi na usalama wa raia kuwa shwari.
Hayo yamesemwa na Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kupitia
Mjumbe wa kamati hiyo Capt. Mstaafu John Chiligati wakati akiwasilisha
taarifa ya kamati hiyo kwa kipindi cha mwezi Februari 2014 hadi Januari
2015, bungeni mjini Dodoma.
Alisema pamoja na hali kuwa shwari kulikuwepo na changamoto
chache za uvunjifu wa amani, vitendo vya uporaji mali na matukio ya
mauaji ya vikongwe na watu wenye ualbino yaliyotokea katika baadhi ya
mikoa.
“Katika ziara ya kamati pamoja na taarifa kutoka kwenye wizara
husika, Kamati ilibaini kuwa kwa ujumla hali ya ulinzi wa nchi na
usalama wa raia katika kipindi hiki ilikuwa shwari” alisema Capt.
Mstaafu Chiligati na kuongeza:
“Ijapokuwa zipo changamoto chache za uvunjifu wa amani na
vitendo vya uporaji mali na matukio ya mauaji ya vikongwe na watu wenye
ualbino yaliyotokea katika baadhi ya mikoa” Capt. Mstaafu Chiligati alilipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi
kwa kazi kubwa na nzuri inayofanya ya kulinda mipaka ya nchi kwani
katika kipindi hiki hali ya mipaka ya nchi imekuwa shwari.
Alibainisha kuwa ili kudumisha hali iliyopo, aliishauri Serikali
itenge fedha za kutosha ili kuviwezesha vyombo vya ulinzi na usalama
kufanya kazi nzuri zaidi na kuifanya hali ya nchi kendelea kutulia na
kuwa na amani na utulivu.
Kwa upande wa masuala ya Ulinzina Usalama wa Mipaka, Capt.
Mstaafu Chiligati alisema katika kipindi hicho hali katika mipaka yote
ya Tanzania imekuwa shwari licha ya kuwepo kwa changamoto ya uingiaji wa
wahamiaji haramu.
Kutokana na hali hiyo Kamati hiyo ililipongeza pia Jeshi la
Polisi nchini kwa jitihada za kudhibiti uhalifu kote nchini na kupunguza
matukio ya uhalifu katika baadhi ya maeneo yaliyokubwa na matukio hayo
hivi karibuni.
“Aidha Kamati ilipotembelea mkoa wa Arusha iliridhika na hali ya
kupungua kwa matukio ya uhalifu na pia ilikuta hali ya utulivu na amani
imerejea katika jiji la Arusha” alisema Capt. Mstaafu Chiligati.
Alieleza kuridhishwa kwa kamati na taarifa za kukamtwa na
kufunguliwa kesi mahakamani kwa baadhi ya watuhumiwa wa matukio ya
kigaidi yaliyotokea katika mkoa wa Arusha.
Hata hivyo kamati alishauri kwamba kesi hiyo isikilizwe haraka na kutolewa hukumu ili ikidhi matarajio ya wananchi.
Kwa upande wa Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu
wa Sheria, kamati iliishauri Serikali kuongeza muda wa mafunzo hayo
kutoka miezi 3 hadi miezi 6 huku ikiitaka Serikali kuwachukulia hatua za
kisheria wanafunzi wanaokwepa kuhudhuria mafunzo bila ya sababu za
msingi.
Aliishauri Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na JKT na ile ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi kukaa pamoja ili kutafuta njia ya kuoanisha
mihula ya vyuo ili isigongane na muda wa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa
sheria.
No comments:
Post a Comment