Na Lorietha Laurence- Maelezo Dodoma
Serikali imeandaa mikakati mbalimbali ya kuboresha afya ya wanawake wajawazito ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Akijibu swali kwa Niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi, katika
kipindi cha maswali na majibu Bungeni mjini Dodoma, Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Dkt. Pindi Chana amesema moja ya
mikakati hiyo ni mpango mkakati ulioboreshwa wa kuendeleza kasi ya
kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi uliozinduliwa na Rais wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete mwaka 2014.
Alisema kuwa mpango huo unawashirikisha wadau mbalimbali ambao
ni World Lung Foundation, Plan International, Care International,
Jhpiego, UNFPA na GIZ wanaochangia katika kupanua vituo vya afya
,kujenga vyumba vya upasuaji na ununuzi wa vifaa na tiba.
“Mkakati huu ni jitihada za serikali katika kuhakikisha afya ya
mama na mtoto inaboreshwa kwa kukomesha vifo vitokanavyo na uzazi na
watoto walio chini ya umri wa miaka mitano” alisema Dkt. Chana.
Alifafanua kuwa Rais Dkt Kikwete ameagiza wakuu wa mikoa
kusimamia masuala ya afya kwa ngazi zote zinahusu afya ya mama na mtoto
na kuhakikisha wanawasilisha taarifa za maendeleo ya utekelezaji kila
baada ya miezi mitatu(3).
Mpango mkakati huo umeanzishwa kutokana na bajeti finyu ya afya
ya mama na mtoto ambayo imekuwa ikipungua kila mwaka wa fedha , hivyo
serikali ikaona umuhimu wa kuangalia njia mbadala ya kuweze kupata fedha
ili kuongeza bajeti.
No comments:
Post a Comment