WAKAZI zaidi ya 7000 wa Kijiji cha Shoga
kata ya Chalangwa Wilaya ya Chunya mkoani hapa wanatarajia kunufaika na huduma
za simu kutoka kampuni ya TTCL baada ya kuzindua mnara wa mawasiliano.
Akizungumza katika sherehe za uzinduzi wa
mnara huo, Mkurugenzi wa Kanda ya Mbeya wa TTCL, Juvenal Utafu, alisema mradi
huo umejengwa kupitia mfuko wa huduma ya mawasiliano kwa wote(UCSAF) uliotolewa
na Serikali.
Utafu alisema Serikali kupitia mfuko huo
umelenga kuleta ushiriki kwa watoa huduma za mawasiliano katika kukuza na
kusukuma maendeleo ya kijamii kwa kutumia TEHAMA hususani katika maeneo ya
vijijini.
Alisema Serikali ilitoa tenda kwa kampuni
ya simu ta TTCL katika awamu ya kwanza iliyoanza kutekelezwa mwaka 2014 kwenye
mikoa 10 ikilenga Kata 20 zenye vijiji 98 vyenye wakazin 160818
ambapo gharama yake ni shilingi Bilioni 3.6.
Alisema katika awamu hiyo Mkoa wa Mbeya
umetekeleza mradi huo wilayani Chunya katika Kata ya Chalangwa kijiji cha Shoga
ambako umejengwa mnara unaotumia teknolojia ya CDMA ambapo mradi huo umegharimu
shilingi 98,515,000 na kuwanufaisha wakazi 7343.
Alisema TTCL imejipanga kuhakikisha huduma
za mawasiliano zinapatikana kirahisi ikiwa ni pamoja na Vocha , simu na vifaa
vyake, Internet na Fax na kuongeza kuwa huduma zaidi zitaendelea kuongezeka.
Baadhi wa Wananchi waliozungumza na gazeti
hili waliipongeza Kampuni ya TTCL kwa kuwajengea mnara wa mawasiliano na kwamba
umewapunguzia gharama kubwa walizokuwa wakizipata awali kabla ya kuwepo kwa
mnara huo.
Nathaniel Nakamia na Lusekelo Lwesha
wakazi wa Kiji cha Shoga walisema kabla ya kujengwa kwa mnara huo na kuanza
kutumika walikuwa wakilazimika kusafiri umbali wa kilomita 6 kufuata vichuguu
ili wapate mawasiliano.
Walisema mbali na kusafiri umbali huo pia
walilazimika kupanda pikipiki kwa gharama ya shilingi 3000 ili kufikia maeneo
ambayo yalikuwa yanamawasiliano ya simu ili kuweza kuwasiliana na ndugu zao
kutoka pande zingine.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika sherehe
hizo, Katibu tawala wa Wilaya ya Chunya, Sosthenes Mayoka, aliyemwakilisha Mkuu
wa Wilaya hiyo, Deodatus Kinawiro, mbali na kuipongeza kampuni hiyo pia alisema
kutokana na kuwepo kwa mawasiliano kijijini hapo kutasaidia kurahisisha
shughuli za maendeleo na suala la ulinzi.
Alisema hivi sasa wananchi waweza kupiga
simu moja kwa moja wilayani endapo kutatokea tatizo lolote hivyo kuifanya
kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya kuchukua hatua za haraka.
Aidha alitoa wito kwa Wananchi kuutunza
mnara huo kwani Kampuni hiyo imeonesha mfano wa kuigwa kwani makampuni mengine
yameshindwa kupeleka huduma za mawasiliano vijijini wakihofia kupata hasara
lakini wakasahau kuwa vijiji hivyo vinarasilimali za madini na mifugo ambapo
wanauwezo wa kununua huduma za simu.
Hata hivyo Kampuni hiyo ilitoa simu mbili
za mezani kwa Serikali za Vijiji vya Shoga na Sangambi ili zisaidie katika
kurahisisha shughuli za maendeleo pamoja na mawasiliano kati ya viongozi na
wananchi wao.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment