Waziri wa Habari ,
Utalii , Utamaduni na Michezo Said Ali Mbarouk ameiagiza kamati ya
utalii ya wilaya ya wete kurejea katika mazungumzo na wananchi wa Kisiwa
cha Fundo na kuwaelimisha faida na umuhimu wa Sekta ya Utalii katika
kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla .
Amesema kuwa bado
wananchi wa Kisiwa hicho wanahitaji elimu zaidi na kuongeza kwamba
kamati ya utalii ya Wilaya ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha kwamba
wakaazi wa Kisiwa hicho wanatambua faida ya Sekta hiyo .
Kauli hiyo ameitoa
wakati akizungumza na wajumbe wa kamati ya Utalii ya Wilaya hiyo pamoja
na Viongozi wa kutoka Taasisi zinazohusika na masuala ya Uwekezaji
ikiwemo ZIPA , Kamisheni ya Utalii na Idara ya ardhi na kuwataka
kuongeza uhamasishaji wa wawekezaji kuwekeza ili kuitangaza wilaya hiyo
kupitia sekta ya utalii .
Amesema kuwa kitendo
cha baadhi ya wananchi wa Kisiwa cha Fundo cha kutoshirikiana na
mwekezaji kunaweza kuitoa dosari sekta hiyo ambayo imekuwa tegemeo la
taifa katika kuimarisha uchumi wake ambapo suluhisho lake ni kamati
kuwaelimisha wananchi hao .
“Pamoja na elimu
mnayoitoa lakini iko haja kwa kamati kurejea kwenye meza ya mazungumzo
na wakaazi wa kisiwa hicho ili kuwaelimisha umuhimu wa sekta na kuwataka
kushirikiana na mwekezaji ambaya ana nia ya kuboresha uchumi wa nchi ”
alieleza .
Aidha mesema kuwa
kamati hiyo inajukumu la kuwasikiliza wananchi pamoja na kuchukua
changamoto zao na kisha kuzifikisha kwa mwekezaji ili kutafuta ufumbuzi
kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla .
Hata hivyo Sheha wa
Shehia ya Fundo Khamis Abeid amesema kuwa mgogoro huo wa wananchi wa
Kisiwa hicho pamoja na mwekezaji unachangiwa na wanasiasa ambao wamekuwa
wakipita na kuwashawishi wananchi kutokubaliana na mradi huo .
Amesema kuwa iwapo
wanasiasa watakuwa tayari kufika katika Kisiwa hicho na kisha kuzungumza
na wananchi juu ya mradi huo na umuhimu wake wananchi wako tayari kutoa
ushirikiano kwani wanatambua faida za Sekta ya Utalii .
“Mgogoro huu
unachangiwa na wanasiasa , kwani wananchi wanasema kuwa Viongozi wao wa
Jimbo ndio wanaowaambia kuukataa mradi huu na hapa mimi biko tayari
tufuatane nao hadi kwa wananchi wakawaambie faida ya mradi huu ”
alifahamisha .
Mapema mwenyekiti wa
kamati hiyo Hassan Khatib Hassan amemhakikishia waziri kuwa mradi wa
ujenzi wa hoteli katika Kisiwa hicho utatekelezwa vyema kwani kamati
inaendelea kutoa elimu kwa wakaazi wa Kisiwa hicho .
Amesema kuwa kamati
yake imeshafika katika kisiwa hicho na imewahai kufanya vikao na
wananchi wa Kisiwa hicho na katika vikao hivyo mazungumzo yao
yameonyesha kukubalika kwa mradi .
Katika Kisiwa cha
Fundo jumla ya miradi miwili ya ujenzi wa Hoteli inatarajia kujengwa
ambapo mmoja kati ya hiyo ni mradi wa mwekezaji mzalendo .
No comments:
Post a Comment